Friday, 4 September 2015

MOHAMMED AHMED:GWIJI WA MUZIKI WA TAARAB TANZANIA


“MAPENZI yangu pokea,kwa moyo wa ukunjufu
Wewe nnakulete,usiwe mbabaifu
Kama utayagomea,nitakujua dhaifu”.
Hio ni moja kati ya beti ya wimbo maarufu wa taarab asilia unaojulikana kwa jina la ‘Mapenzi yangu pokea’ulioghaniwa na mutrib mashuhuri na mkongwe ambae ameshastaafu,Maalim Mohammed Ahmed Mohammed.

Thursday, 16 July 2015

ZANTEL YATOA MSAADA WA VYAKULA KWA JUMUIYA YA WAZEE ZANZIBAR



Na Haroub Hussein


 Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel leo imetoa msaada wa vyakula kwa ajili ya mwezi wa Ramadhani kwa makundi maalumu ya wazee hapa visiwani Zanzibar.

Msaada huo unajumuisha sukari, unga wa ngano pamoja na mchele umetolewa katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika leo.

Kampuni ya Zantel upande wa Zanzibar imeainisha wazee zaidi ya 120 wenye uhitaji wa vyakula kwenye mwezi huu wa Ramadhani walio chini ya jumuiya ya wazee hapa Zanzibar.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa wazee, Mkurugenzi wa Biashara wa Zantel-Zanzibar, bwana Mohammed Mussa, amesema ni kawaida kwa kampuni ya Zantel kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii katika kipindi hiki cha Ramadhani.


'Tuna furaha sana leo kuweza kusaidia jamii hii ya wazee ambao mara nyingi wamekuwa wanasahaulika, kwani tunaamini wazee ni sehemu muhimu sana ya jamii ndio maana Zantel leo tumeamua kutoa msaada huu ambao unatutofautisha sana na makampuni mengine katika vipaumbele vyetu' alisema Mussa.

Mussa aliongeza kuwa kama kampuni ya simu inayoongoza Zanzibar, Zantel mara zote imekuwa mfano katika shughuli zake za kijamii na vipaumbele vyake kiujumla.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, mgeni rasmi ndugu Msham Abdallah, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar, alisema anaipongeza Zantel kwa kushirikiana na serikali kuyasaidia makundi ya wazee.


‘Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali katika kulisaidia kundi hili la wazee, kwahiyo ni furaha kwetu leo kuona Zantel imekuwa ya kwanza kusaidia kundi hili leo’ alisema bwana Abdallah.

Akitoa neno la shukrani kwa kampuni ya Zantel, naibu mwenyekiti wa jumuiya ya wazee Zanzibar, Bwana Mwadini Kutenga, alisema anawashukuru Zantel kwa msaada huo, akisema umekuja kwa wakati mufaka hasa ukizingatia kuwa wanakaribia kuadhimisha sikukuu ya Idi.

'Kwa misaada hii, Zantel inawafanya wazee nao wajiskie sehemu ya jamii, kwani mara nyingi wamekuwa wakisahaulika sana na kwa hakika hatutawasau kwa ukarimu wao huu' alisema bwana Kutenga.


Kampuni ya Zantel imekuwa msitari wa mbele katika kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani, na msaada huu ni maalumu kwa kundi la wazee ambalo mara nyingi linasahaulika katika jamii.

Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na lengo la kuwaunganisha na kuwasaidia wazee Zanzibar na sasa ina wanachama zaidi ya 1000.





Wednesday, 15 July 2015

AL MARHUM SHEIKH MOHAMMED MAJID;MIONGONI MWA WANAZUONI WALIOITANGAZA VYEMA DINI YA KIISLAMU


“INALILAHI wa Ina Ilayhi Rajiuun yaani hakika sisi ni waja wa Mwenyezi Mungu na sisi kwake tutarejea,”hiyo ni kauli ambayo kila muumini wa dini ya Kiislamu anaifahamu kwa kuwa ina maana ya kukumbuka kila kilichoumwa na Allah (SW) basi hakina budi kurejea kwake kwa maana ya kufa.

Kwa kila muislamu akiisikia kauli hii huwa anafahamu kwamba ameletwa duniani kwa ajili ya kumuabudu Allah (SW) basi iko siku atarudi kwake.

Naweza kuinasibisha kauli hii kwa Al marhum Sheikh Mohammed Majid ambae ni mmoja wa maulamaa wa dini ya kiislamu waliokuwepo hapa Zanzibar katika kuitangaza dini ya Mwenyezi Mungu(Uislamu).

Marehemu Sheikh Mohammed Majid ni miongoni mwa wanazuoni maarufu wenye maarifa makubwa ya dini ya kiislamu waliotangulia mbele ya haki ambao walikuwepo Zanzibar katika kuitangaza dini ya Mwenyezi mungu.

Sheikh Majid atakumbukwa maisha kutokana na uwezo wake na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika kulingania dini ya Kiislamu na kuisambaza kupitia njia tofauti ili iwafikie wale waliokusudiwa.

Marehemu Mohammed Majid alizaliwa Juni 5 mwaka 1956 katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja,ambapo elimu yake ya awali alianza kuipata kisiwani Pemba kijiji cha Mchakaeni.

Marehemu Sheikh Mohammed Majid alikuwa akiishi kisiwani humo kutokana na baba yake kuhamia kwa shughuli za uvuvi akitokea kijijini kwao Matemwe.

Mwaka 1965 marehemu alihamia kisiwani Zanzibar na kuanza elimu yake ya Maahad Islamia ambayo kwa sasa inajulikana kama Chuo cha Kiislamu Mazizini ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni elimu ya sekondari.

Mara baada ya kumaliza elimu ya sekondari Sheikh huyo alikwenda nchini Sudan mwaka 1984 katika chuo kikuu cha kimataifa cha Afrika kuchukua elimu ya dini ya kiislamu pamoja na lugha ya kiarabu .

Baadae alikwenda nchini Saudi Arabia kuchukuwa shahada ya kwanza ya dini ya Kiislamu na Kiarabu.

Mwaka 1992,Marehemu alirudi Sudan kuchukua shahada ya Uzamili yaani ‘Masters Degree’ ya lugha ya Kiarabu na dini ya Kiislamu na mara baada ya kumaliza elimu hiyo alirudini nyumbani Zanzikbar.

Marehemu Sheikh Mohammed Majid hakuwa nyuma katika maswala ya kutafuta elimu ya dini nay a dunia kutokana na kwamba alikuwa akijua umuhimu wa elimu.

Alikaa Zanzibar kwa muda mfupi na baadae alirudi nchini Sudan kuchukuwa elimu ya udaktari wa Falsafa “PHD” ya dini ya Kiislamu pamoja na lugha ya Kiarabu.

Elimu alizozipata nchi mbali mbali na aliyoipata hapa nchini kupitia walimu waliomsomesha dini aliweza kuongeza dini kipaji chake na kuwa na hamu kubwa ya kuitangaza dini ya kiislamu.

Marehemu Dr Mohammed Majid baada ya kumaliza elimu hiyo na kurudi nyumbani alisomesha lugha ya Kiarabu katika kituo cha Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Pia marehemu Dk  Mohammed Majid ni miongoni mwa waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Kiislamu Chukwani na pia aliwahi kuwa msaidizi Mwalimu Mkuu Madrassat Noor mpaka mwaka 2000 baada ya kufariki marehemu Maalim Bakathir.

Marehemu Sheikh Mohammed Majid alitawazwa rasmin kuwa mwalimu mkuu wa Madrassa hiyo iliyopo katika mtaa wa Ukutani mjini Unguja.

Mnamo mwaka 2002 sawa na mwaka 1423,Marehemu Sheikh Mohammed Majid alifariki dunia na kuzikwa kijijini kwao Matemwe Mnazimmoja Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk Mohammed Majid atakumbukwa maisha na waislamu wote wa hapa visiwani Unguja na Pemba kwa ujumla kwa kuwa na changamoto kubwa ya kuanzisha kipindi cha Jiongezee Maarifa kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC).

Kipindi hicho kimeweza kuvutia vijana wengi kutaka kuifahamu na kusoma zaidi mwenendo wa dini yao ya kiislamu pamoja na kitabu kitukufu cha Quraan.

Baadhi ya masheikh waliokuwepo hapa Zanzibar wanamzungumzia kwamba marehemu huyo atakumbukwa sana katika kipindi chake hicho cha Jiongezee Maarifa ambacho hupendwa na waislamu wengi kwa kuwafanya vijana wengi kuwa na hamu ya kuijua dini yao.

“Marehemu Sheikh Mohammed tunamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoyafanya wakati alipokuwa yuhai kwa kuanzisha kipindi cha Jiongezee maarufa ambacho kimewaongoa vijana wengi  wa Kiislamu na kufanya kipindi hicho kikauwa mpaka kufikia kisiwani Pemba.

Katika kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,Marehemu Sheikh Mohammed Majid alikuwa akisomesha somo la Fiqhi na Quraan katika msikiti wa Jongeani na msikiti wa Mchangani yote ya mjini Unguja.

Marehemu ameweza kujijengea jina lake kwa kuweza kuitangaza dini ya Kiislamu kupitia Nyanja mbali mbali kwa vijana na watu wazima ili kuzidi kukuwa kwa jamii ya Kiislamu kwa kufuata maadili mema ya dini yao.

Aidha Marehemu atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri mbali ya kulingania dini ya Kiislamu,lakini pia mapenzi yake kwa watu wote wa rika tofauti,ucheshi na pia hakuwa mtu mwenye majivuno.

Marehemu aliacha wake watatu na watoto 11,wanawake 10 na mwanamme mmoja.

Kwa niaba ya makala haya na mafundisho yake mema  ya hapa duniani kwa ajili ya Akhera, Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amlaze mahali pema peponi Aamin.

Saturday, 4 July 2015

DR OMAR: NGUZO IMARA ILIYOKATIKA GHAFLA


SIKU kama ya leo miaka kumi nan ne iliyopita.Tanzania iligubikwa na simanzi isiyokuwa na mfano baada ya kupokea taarifa za kifo cha aliyekuwa Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Marehemu alifariki ghafla siku moja tu baada ya kushiriki katika ufunguzi wa maduka ya biashara ya sabasaba katika maeneo ya Mtoni jijini Dar es Salaam.

Wananchi wa Tanzania hawatoweza kumsahau marehemu kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kwa Watanzania.

Akiwa katika ufunguzi huo ambapo alionekana kuwa ni mtu wa kawaida kwa kuwa na afya aliwahutubia wananchi kwsa kuwapa moyo wananachi wa Tanzania na Zanzibar kwa jumla kutokana na kupendelea kusema ukweli na hata kupiga vita tabia ya ubaguzi.

Katika hotuba zake ambazo alizowahi kuzitoa katika kazi zake za kawaida ilikuwa ni kukemea tabia ya baadhi ya watu kubaguana kwa misingi ya rangi zao na maeneo ya asili.

Utekelezaji wa majukumu yake katika kukemea tabia hiyo uliweza kumjengea sifa kwa wananchi na watu wengi kwa kuwa na nia ya kutaka na Mikoa mengine ya Tanzania na kuondosha ubaguzi kwani aliamini kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Kwake maumbile au asili tofauti na mwengine kwani halikuwa jambo la kujadiliwa ila watu walipaswa kuwa kitu kimoja kwa ajili ya maendeleo yao kwani wapo kwa kutambuana tu.

Lakini kauli ya marehemu Dr Omar Ali Juma,aliyoitoa mara baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri kiongozi wa Zanzibar alisema kwamba ni vyema Wazanzibari wakasahau yaliopita na kuangalia mbele.

Marehemu aliamini kuwa kauli hiyo ni muhimu kwa kuwaunganisha wananchi wao na ni vyema kukumbukwa kwani amewahi kushuhudia matatizo mengi yanayowakumba watu waliotilia maanani tofauti zao na kuacha kushirikiana katika mambo muhimu ya kimaisha.


Kutojali ukabila,rangina uzawa kutasaidia kuimarika kuimarika kwa Taifa la Zanzibar.

Marehemu atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri na wananchi wa Tanzania kupitia hotuba zake zilizojaa nasaha juu ya watu wa Zanzibar na kuamini kuwa Zanzibar inaweza kuwa imara na mshikamano.

Pia marehemu Dr Omar atakumbukwa sana kutokana na mpango wa kusimamia kujitosheleza kwa chakula uliojulikana kama ‘Mtakula’.

Mpango huo ambao ulianzishwa na Serikali ya awamu ya nne ya Marehemu Sheikh Idrissa Abdulwakil,ambapo ulileta mageuzi makubwa ya kilimo hapa visiwani .

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa makala haya walisema Mtakula ulisaidia sana kuamsha ari ya wananchi kupenda kilimo hapa visiwani na mlezi mkuu alikuwa Dr Omar Ali Juma.

Kwa upande wa siasa,Marehemu alikuwa ni mwanasiasa mashuhuri na mahirina aliwapenda sana watu wote hii inaonesha kuwa kauli zake alikuwa akizitekeleza kwa vitendo na kuwaona watu wote ni sawa bila ya kujali itikadi zao kisiasa na ulua aliokuwa nao.


Dr atakumbukwa kwa mambo yake yote mema ambayo alihakikisha wananchi wanayaendeleza kwa ufasaha na mambo yote amabayo ni msingi wa maendeleo ya nchi.

Alipokuwa Makamo wa Rais marehemu atakumbukwa sana kwa juhudi zake kuimarisha Muungano na pale matatizo yanapoibuka hakuwa nyuma kwa kusaidiana na viongozi wenzake wa ngazi za juu kutatua matatizo hayo.

Pia aliweza kusaidia kuleta umoja kwa wananchi wa Tanzania bila ya woga wowote.
Aidha wananchi wao walizungumza na mwandishi wa makala hii walisema siku zotemarehemu alisimamia maslahi ya Zanzibar kwa wakati wote wa uongozi wake.

“Dk Omar ni mwanangu,alikuwa akija Pemba basin a nyumbani kwangu huwa anakuja namjua vizuri sana alikuwa hodari katika kusimamia maslahi yetu sisi Wazanzibari,”alisema Mzee Kassim Haji mkaazi wa Wawi Pemba.

Saleh Amir ni rafiki wa karibu na marehemu Dr Omar Ali Juma anaeleza kuwa alikuwa ni mtu mwenye kupenda watu na hata kusaidia alikuwa hodari sana.

“Marehemu alikuwa ni mtu wa karibu sana na mimi alikuwa ni mpenda watu,hodari anapenda masihara na mwenye kupenda kusaidia wengine,alisema Saleh Amir.

Dr Omar pia katika uhai wake alikuwa ni mpenzi mkubwa wa michezo hususan mpira wa miguu ambapo alipokuwepo visiwani Unguja huhudhuria katika kiwanja cha Amaan kuangalia mchezo wa soka.

Kwa upande wa burudani Dr Omar alikuwa ni mpenzi mkubwa wa Maulid ya homu na katika shughuli zake nyingi alikuwa lazima yakuwepo maulidi hayo.

Bila shaka hii ni sifa njema ya marehemu katika kudumisha utamaduni,mila na desturi za Kizanzibari.

Marehemu   Dr Omar hatoweza kusahauli hatoweza kusahaulika katika mioyo ya wapenda amani na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hayo yanatokana na juhudi alizokuwa akizichukuwa katika kuhakikisha  maendeleo yanapatikana katika nchi.


Pia  hatoweza kusahaulikwa kwa imanina roho yake nzuri katika kusaidia wananchi katika Nyanja mbali mbali za kutatua matatizo ya kimaisha.

Marehemu alizaliwa Juni26 mwaka 1942 Chake Chake kisiwani Pemba,elimu yake aliianzia mnamo mwaka 1949 hadi mwaka 1957 katika skuli ya Haile Selassie wakati huo ikifahamika kwa jina la Euan Smith Secondary School.

Mwaka 1960 alijiunga katika chuo kikuu cha Moscow nchini Urusi na kupata stashahada ambapo aliendelea na masomo yake katika chuo hicho hicho kwa muda wa miaka saba.

Baadae pia alipata masomo katika vyuo vikuu vyengine katika taaluma ya utibabu wa wanyama ikiwemo chuo kikuu cha Cairo nchini Misri,pia alipata taaluma nyengine katika mwaka 1969 katika vyuo mbali mbali ikiwemo nchini Marekani na kile cha Kivukoni nchini Tanzania.

Mwaka 1988alifanikiwa kushika wadhifa wa Waziri Kiongozi wa Zanzibar hadi mwaka 1995 aliposhika wadhifa wa Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hadi kufariki kwake mwaka 2001 siku kama ya leo.


Tuesday, 30 June 2015

AL-MARHUM SHEIKH BAKATHIR: NGUZO IMARA ILIYOITANGAZA VYEMA ZANZIBAR KATIKA MWASWALA YA DINI YA KIISLAM


ZANZIBAR ni moja ya nchi maarufu zilizobarikiwa kuwa na wanazuoni wengi ambao waliweweza kuitangaza vyema nchi hii kutokana na kutoa elimu ya dini ya Kiislamu kwa vijana nwa ndani na nje ya nchi hii.

Kama utataka kutaja majina yao pamoja na sifa walizokuwa nazo katikamkutekeleza na kuutangaza Uisalmu,basi huwezi kuwamaliza kutokana na wingi wao ambao ndio ulioifanya Zanzibar kuwa mashuhuri katika maswala ya dini ya Kiislamu.

Miongoni mwa wanazuoni hao ni pamoja na Marehemu Sheikh Abdallah Abubakar Abdalla Muhammad Bakathir,ambae nae ni mmoja wa wanazuoni maarufu visiwani Zanzibar ambae ameshafika mbele ya haki lakini bado mafunzo yake aliyokuwa akiyatoa yanaendelea kufanyiwa kazi.
“Rabananfaa nabimaa lamtana,Rabi alli nalladhian fahuna,Rabi fakih na wafakih ahlana,Wakaraba tilanafai didinaa,Maahli kutri untha wazaka,Rabi wafiq na wawafiq hulima,Trtadhika huwalwafiila lkarama.

Hii ni dunia maarufu katika kipindi hichi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo mara baada ya kumaliza kwa darsa ya tafsiri ya Quraan kipindi hicho kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC) husomwa dua hiyo.

Dua hiyo ambayo ni maarufu sana kwa waumini wa dini ya Kiislam katika masikio yao,ambapo kama huwezi kujua kwamba dua hiyo ilirekodiwa na marehemu Maalim Abdalla Abubakar Bakathir.

Maalim Bakathir ni mmoja wa wanazuoni maarufu ambao ametoa elimu ya dini ya Kiislamu ikiwemo kitabu cha Quraan kwa vijana wengi ambao hivi sasa wameweza kushika nafasi yake kuwa walimu maarufu.

Mwandishi wa makala hii alibahatika kukutana na mmoja wa wanafunzo wake ambae kwa sasa ni Mwalimu mkuu wa Madrasat Noor ambayo ilianzishwa na yeye marehemu,Maalim Abdulrahman Sheikh Al-habshi na kumuelezea historia ya marehemu Maalim Bakathir.

Marehemu Maalim Abdalla Bakathir alizaliwa mwaka 1941 hapa hapa Zanzibar akiwa ni mtoto pekee wa mwanachuo maarufu Marehemu Sheikh Abubakar Abdalla Bakathir ambapo pia babu wa marehemu alikuwa mwanachuoni.

Baada ya kutimiza miaka miwili baba wa marehemu Maalim Bakathir alifariki duni na kulelewa na aliekuwa mwanafunzi wa baba yake marehemu Sheikh Muhammad Bin Omar Al-Khatib maarufu ‘Bwana wa Shangani’ pamoja na mkewe Bi Khadija Bint Abdalla ambae alikuwa shangazi wa Maalim Bakathir.

Kuhusu maisha yake ya elimu ya dini marehemu Maalim Bakathir alianza akiwa na umri mdogo ambapo elimu hiyo aliipata kutoka kwa wlaimu wake wakiwemo akina marehemu Maalim Himid Hajj Abdalla,Maalim Abdalla Muadhin na Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka).

Baadae marehemu Maalim Bakathir alipata nafasi ya kwenda kuongeza elimu ya dini ya Kiislamu huko Lamu Mombasa Kenya ambapo pia alibahatika kupata elimu kutoka kwa wanazuoni maarufu akiwemo Sayyid Bahasany,Shariff Al-Aididi na Sayyid Ally Badawi.

Baada ya kupata elimu kwa wanazuoni mbali mbali wa ndani nan je ya Zanzibar kuanzia miaka ya 1960,marehemu Maalim Bakathir alianza kusomesha Quraan Madrassat Sunni Cuth ambapo kwa sasa unajulikana kwa jina la Masjin Hanaffy uliopo Mkunazini ambapo aliajiriwa kusomesha watoto wenye asili ya kihindi.

Mnamo Machi 1 mwaka 1967 Marehemu alianzisha Madrassat Noor hapo hapo Masjid Hanafy na kuanza kusomesha watoto wa makabila mbali mbali yalioko visiwani Zanzibar.

Mbali na kuwa mwalimu wa Madrassa,Marehemu pia aliweza kufungua Darsa baina ya Sala ya Magharib na Isha huko Masjid Jibril mnamo miaka ya 1991 na 1992.

Marehemu aliendelea na darsa hiyo pamoja na madrassa hiyo hadi mwaka 1988 alipostaafu na kuwaachia wanafunzi wake wakiwemo marehemu Mohammed Majid,Ustadh Khalid Mohammed Mrisho na Maalim Abdulrahman Sheikh Al-habshi nay eye alibakia kuwa mlezi.

“Mimi na wenzangu ndio tuliokuwa wanafunzi wake ambapo alituachia darsa pamoja na chuo kwa ajili ya kuendeleza na kwa uwezo wa Allah (S.W) bado tunaendeleza elimu hiyo aliyotupa kuwapa na wengine ,”alisema Maalim Abdulrahman.
Pia marehemu Maalim Bakathir aliwahi kuwa mwalimu wa Quraan kwa wanafunzi wenye asili ya Kibohora.


Aidha mbali ya kuwa mwalimu wa Madrassa,lakini pia marehemu aliwahi kuwa mwalimu wa skuli mnamo mwaka 1970 ambapo alisomesha katika skuli ya Hamamni akiwa mwalimu wa dini.

Marehemu Maalim Bakathir aliweza kusimamia mambo mengi ya kheri ikiwemo kusimamia maswala ya sadaka,kujenga miskiti na vyuo vya quraan,aliwahi kuwa Mjumbe wa kamati nyingi za kidini ikiwemo kamati ya Zaka pamoja na kuwa Mjumbe wa bodi ya Wakfu na mali ya amana.

Ilipofika Juni 4 mwaka 2000 Maalim Bakathir alifariki dunia huko nchini India ambapo alikwenda kwa ajili ya matibabu na kuzikwa katika makaburi ambayo wamezikwa wazee wake hapo Ukutani mjini Unguja.

Marehemu Maalim Abdalla Bakathir atakumbukwa kwa mambo mengi ya kheri aliyoyafanya katika visiwa vya Zanzibar ikiwemo kusomesha na kutoa wanafunzi mbali mbali waliotawanyika ndani nan je ya Zanzibar.

Pia alikuwa msimamizi wa Masjid Jibril baada ya kuondoka Maalim wake Maalim Himid kwa kuhamia jijini Dar es Salaam.

Marehemu Bakathir ni mtu mmoja ambae anaendelea na ataendelea kukumbukwa kutokana na mambo mengi ya kheri ikiwemo utenzi wa Miraj ambao ulirekodiwa na kusomwa kila mwaka ifikapo siku hiyo na ZBC Radio.

Aidha katika fani nyengine aliwahi kuwa mtunzi wa mashairi ya kidini ambayo alikuwa akisoma yeye mwenyewe na pia alikuwa mtunzi wa mashairi ya kisiasa lakini hayo alikuwa hasomi mwenyewe.

Marehemu Maalim Bakathir aliwahi kuoa na kupata mtoto mmoja wa kiume ambapo mtoto huyo alifariki akiwa na umri wa miaka 18 mwaka 1991 hivyo marehemu mpaka anakufa hakua na mtoto .

Hii ni faraja kwa Wazanzibari kupata mambo mengi ya dini ambayo yameweza kusaidia kudumisha na kuendeleza uislamu katika vuisiwa hivi.

Kutokana na baadhi ya mamabo aliyoyafanya katika kulingania dini ya kiislamu na kuitangaza Zanzibar kwa kutoa vijana wengi ambao bado wanaendeleza mambo ya kheri aliyoyaacha,Inshaallah Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amuondoshee kiza cha kaburi Aamin


Wabilahi Taufiq. 

Sunday, 28 June 2015

PROFESA HAROUB: KIONGOZI MAKINI ALIEPENDA WATU NA KUSAIDIA WANYONGE


“NIKIWA hai nataka kushuhudia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,ambao ambao unafuata misingi yote ya demokrasia zaidi kwa vyombo vya habari,”.
Hiyo ni miongoni mwa kauli alizowahi kuzitoa katika uhai wake Marehemu Profesa Haroub Othman kwenye moja ya semina ya uzinduzi wa kitabu hapa visiwani Zanzibar.

Tarehe kama ya leo mwaka 2009,Tanzania iliingiwa na simanzi kubwa baada ya kuondokewa na mpiganaji na mtetezi wa haki za wanyonge Marehemu Professa Haroub Miraji Othman.

Ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ni kweli wakati ulifika,Mwenyezi Mungu (SW) alimwita nae akaitika kutokana na wito ambao mwanadaamu yoyote hana budi kuuitika.

Siku iliyofuata ya Juni 29 mwaka 2009  Watanzania walio wengi na hasa wasomi wa nchi hii waliungana na familia ya marehemu katika mazishi yake yaliofanyika nyumbani kwao Baraste na kuzikwa katika makaburi yaliopo katika kijiji cha Chuwini.

Kuondoka katika dunia hii kwa kipenzi cha wengi ilikua ni vigumu kuaminika kutokana na kuwepo kwake karibu na wanajamii pamoja na kazi yake ya kutetea haki na maslahi ya wanyonge.

Ni ukweli usiofichika kwamba marehemu Profesa Haroub ni nguzo kuu iliyo katika ghafla katika ujenzi wa demokrasia,haki,amani na utengamano Zanzibar,Tanzania,Afrika na dunia kwa ujumla.

Marehemu Profesa Haroub atakumbukwa daima kutokana na michango yake mingi ikiwemo kuhubiri haja ya kuwepo kwa mabadiliko na kuwa mwanaharakati mahiri wa sharia na haki za binaadamu na utawala bora.

Pia atakumbukwa kwa mengi mazuri hasa katika mchango wake kwa jamii akiwa ni mpiganaji wa haki za binaadamu pamoja na alikuwa anapenda kusema ukweli.

Nanukuu ile kauli ambayo nakumbuka aliitoa katika siku ya kumkumbuka aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Walemavu marehemu Maalim Khalfan Hemed Khalfan.

Marehemu Profesa Haroub alisema ‘Kama utakuwa humkumbuki mwenzako ambae ameshafika mbele ya haki,basin a wewe uhakikishe kwamba hutokumbukwa,”.


Kutokana na kauli hiyo ambayo imenivutia sana na kujaza hamasa ya kuandika makala hii,na kwa umuhimu aliokuwa nao marehemu katika nchi yetu hatuna budi sote Watanzania tumkumbuke.

Kwa mujibu wa kitabu maaraufu cha ‘Haroub Othman Farewell to the Chairman ‘kilichotungwa takriban miaka sita iliyopita mara baada ya kifo chake kutokea.

Wanasiasa,viongozi,wanasheria, wanahabari pamoja na wanafunzi wake waliweza kutoa maoni yao kutokana na umuhimu aliokuwa nao kwa nchi yake Marehemu.

Hii inaonesha wazi kuwa ni pengo kubwa sana ambalo ni gumu kuzibika kwa kipindi kifupi kutokana na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu na kuwa na umuhimu katika jamii nzima na sio kifamilia pekee.

Kitabu hicho kimemnukuu Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda alivyomueleza Profesa Haroub kuwa mtaalamu aliyebobea katika mitaala ya maendeleo nani mwanaharakati  wa haki za binaadamu ambae anafahamika ndani nan je ya nchi.

  Waziri mkuu huyo ambae alisema marehemu alikuwa mwalimu wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970 pia alimuelezea kuwa ni mtu ambae ndani na nje ya chuo hakuwa mchoyo wa kutoa elimu yake na wala ushauri wa kitaalamu.

Kutokana na kauli ya Waziri Mkuu wetu wa Tanzania kuwa marehemu alitumia vyema sana vipaji alivyokuwa navyo na karama alizojaaliwa na Mwenyezi  Mungu kwa ukamilifu bila ya majivuno,woga wa wivu.

Nae mwanahabari wa siku nyingi Salim Said Salim alimuelezea marehemu Profesa  Haroub kuwa ni mwanaharakati asiye na shaka na aliyetukuka nan i mtu wa kupigiwa mfano.

Pia alimuelezea kwamba aliweza kumfunza mambo mengi sana pamoja na kumuonesha njia ambayo anaamini kuwa ni sahihi katika maisha yake ya kila siku.
Umuhimu wa marehemu Profesa Haroub haukuonekana kwa mwanahabari Salim Said Salim,bali kwa wanahabari wengi sana miongoni mwao ni mwanahabari Haura Shamte .
Haura alimuelezea marehemu kuwa ni alama ya fikra pevu,mahiri na yenye busara pamoja na wadhifa aliokuwa nao na heshima kubwa katika jamii ya Watanzania.

Haura alimsifia marehemu kuwa pamoja na usomi aliokuwa nao,lakini hakujitenga na watu wa kawaida na alishiriki katika shughuli mbali mbali alizoarifiwa.

“Marehemu aliamini kwamba watu wote ni sawa  hakujikweza wala hakutakabari,binafsi Profesa alikuwa chanzo changu cha habari  kila nilipotingwa na jambo hasa katika masuala ya kisiasa,”alisema Haura.

Kwa upande wa kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) hawakuwa nyuma kutoa sifa njema za Marehemu Profesa kutokana na umuhimu wake katika kituo hicho akiwa akiwa mmoja wa waanzilishi wa kituo hicho.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho Iss-haq Ismail Shariff,alieleza kwamba ukweli usiofichika kuwa marehemu aliitaka Zanzibar wanaondokana na shida za kutafuta haki zao za msingi katika wakati mgumu walihitaji.


“Profesa Haroub atakumbukwa kwa dhamira yake njema ya kutaka kuwa Wazanzibari wana  uwelewa katika masuala yote ya sheria,haki za binaadamu na maendeleo,”alisema Mkurugenzi huyo.

Mbali na wasomi lakini kwa upande wa familia yake,haukuwa nyuma kutoa maoni au wasifu mzuri wa marehemu ndugu yao ambapo ndugu yake Othman Miraji Othman alimuelezea kwa kina kaka yake.

Kitabu kimefafanua kuwa Miraj alisema,Marehemu Profesa Haroub alikuwa nguzo ya familia ya ukoo wao na haikutetereka hadi mwisho wa maisha yake.

Alisema jambo lolote litakalomfikia ndugu yake au rafiki yake likiwa la furaha au msiba,marehemu ingawa alikuwa anaishi Dar es Salaam,lakini alikuwa nahudhuria katika shughuli hiyo.

Aidha ndugu huyo alimuelezea kaka yake kuwa alikuwa akiipenda sana Zanzibar na ndio sehemu aliyokuwa  akiipendelea sana kuvutia pumzi yake ya mwisho kuliko sehemu nyengine.

Mmoja wa watu waliotoa ujumbe kwa njia ya mashairi ni Jenerali Ulimwengu ambae alisema katika mashairi yake .
Haroub kenda harudi,Ndiyo yetu sote sudi
Kifo kwetu sote budi,Ahadi ikiwadia
Ela tuko kulia,Mataka kujishikia
Haroub alo azizi,katimiza yake kazi
Bila kufanya ajizi,Sote tumemridhia.


Hizi ni baadhi ya beti za utenzi uliotungwa na Jenerali Ulimwengu kwa ajili ya marehemu Brofesa Haroub Othman .

Hakuna jambo lisilokuwa muhimu kwa wananchi wa Tanzania kukumbuka mchango wa marehemu Profesa Haroub katika taaluma yake ikiwemo kufundisha taaluma ya maendeleo na mambo ya sheria kwa muda wa miaka 41.

Pia alitoa elimu katika maeneo makubwa ya ufundishaji ikiwemo haki za binaadamu,Ujenzi wa Demokrasia na utawala bora,historian a falsafa ya siasa na siasa za kusini mwa Afrika na Mashariki ya kati.

Ni vigumu kueleza mambo mengi kuhusu mchango wake kama mwanataaluma katika wasifu huu ambapo eneo moja kubwa la utafiti na ushauri,aliweza kuchapisha vitabu vingi na makala nyingi katika vitabu na majarida ya kitaifa na kimataifa.

Ni machache niliyoyaeleza kuhusu marehemu Profesa Haroub Miraj Othman ambae kwa anaemjua na asiemjua ataamini kwamba Profesa alikuwa kiungo mahiri katika jamii ya Kitanzania.

Hivyo basi hakuna budi kwa wasomi na wasiowasomi kufuata nyayo za marehemu kutokana na kuwa mhamasishaji na mpiganaji wa haki za binaadamu hasa wanyonge.

Marehemu Profesa Haroub alizaliwa Novemba 30 mwaka 1942 katika mtaa wa Baraste Kipande na kuanza masomo yake katika skuli ambayo ikijulikana kwa jina la French Comorian School ilioko katika mtaa wa Kajificheni mnamo mwaka 1949.

Mwaka 1958 marehemu alichaguliwa kujiunga na chuo cha UwalimuBeit el Rass ambapo baadae ambapo baadae alijiunga na elimu ya juu Urusi katika chuo kikuu cha Moscow ambapo huko alipata shahada hya uzamili wa sheria (LLM) mwaka 1967.

Mwaka 1969 alipata shahada ya Diploma ya sheria katika chuo kikuu cha Hague,Uholanzi na mwaka 1980 alipata shahada ya uzamivu (PHD) chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Marehemu aliajiriwa katika chuo kikuu cha Afrika Mashariki mwaka 1969 ambapo mwaka 1970 aliajiriwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam hadi pale Mwenyezi Mungu alipochukua roho yake .

Alianza kazi katika kitivo cha sheria kwa muda mfupi na baadae alihamia katika taasisi ya taluma na maendeleo.

Marehemu aliweza kushika nyadhifa mbali mbaliikiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi mwaka 1981-1982 na baadae alikuwa Mkurugenzi kamili kwa vipindi viwiwli mfululizo 1982-1988.

Pia marehemu aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UDASA pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi.

Marehemu alikuwa ni mchapa kazi,alikuwa ni mtu aliejitolea katika maisha yake na kutetea wanyonge ndani na nje ya nchi.

Marehemu Profesa Haroub kabla ya kifo kumkuta Juni 27 mwaka 2009 alishiriki katika uzinduzi wa kitabu cha ‘Race Revolution and the  Struggle’ kinachozungumzia maisha ya kisiasa ya Makamo wa Kwaza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad.

Kitabu hicho pia kinazungumzia maisha ya mwanasiasa mkongwe na Waziri wa Elimu wa zamani Ali Sultan Issa ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Baytul-Yamin uliopo Funguni mjini Unguja.

Aidha marehemu usiku wa Juni 27 hiyo hiyo alishiriki uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu kwa Nchi za Jahazi(ZIFF) ambapo mwandishi wa makala hii alibahatika kumuona siku hiyo marehemu akisalimiana na Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar,Shamsi Vuai Nahodha ambae alikuwa mgeni rasmin siku hiyo.

Profesa Haroub ambae ameacha mke ambae nae ni Profesa Saida Saleh Yahya na mtoto wao Mmoja Tahir Haroub Othman.

Alifariki dunia asubuhi ya Juni 28 mwaka 2009 kama leo na kuzikwa Juni 29 katika makaburi yaliopo kijijini kwao Chuwini.


Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amlaze mahali pema peponi Aamin.

Makala hii imepatikana kupitia kitabu maarufu cha ‘Haroub Othman Farewell to the Chairman’ kwa msaada  wa kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar 

Friday, 12 June 2015

KARIBUNI WOLVERHAMTOM CAFE










WATANZANIA WATIKWA KUENDELEZA UTAMADUNI WAO

Na Aboud Mahmoud,Zanzibar
IPO haja kwa wananchi wa Tanzania kuendeleza na kudumisha utamaduni wao ili kuweza kujitangaza kitaifa na kimataifa pamoja na kuvuta watalii wengi ili kuja kuona tamaduni zao.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Uswiss ambae amemaliza muda wake Olivier Chave, katika sherehe za kutimiza miaka 14 ya Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi Zanzibar (DCMA)  pamoja na kumuaga yeye mwenyewe ambae ni mfadhili  mkuu wa chuo hicho.
Alisema kwamba utamaduni wa nchi ndio kitu muhimu ambacho watu wengi kutoka nchi mbali mbali hupenda kukijua na kuvutia watalii wengi ambao huongeza mapata ya nchi.
Alisema kwamba zipo nchi nyingi duniani zimekuwa zikipata wageni wengi kupitia kukuza utamaduni wao pamoja na kuutangaza ndani na nje ya nchi kutokana na kushirikiana baina ya wananchi na Serikali.
“Nawaomba wafanyabiasha, na wadau wa sekta mbali mbali kuunga mkono utamaduni wa Zanzibar kwani tukiiwachia Serikali na wasanii peke yake nchi hii haitoweza kujitangaza na kupata mafanikio ya aina mbali mbali,”alisema.
Aidha balozi Chave aliikisifia chuo cha DCMA kwa kuwa mstari wa mbele kuwarithisha vijana wa Kitanzania katika utamaduni wa mambo mbali mbali ikiwemo ngoma za asili.
Hivyo aliwashauri walimu na uongozi wa bodi hiyo kutochoka katika kuwarithisha vijana hao na sanaa ambayo inahitaji kuendelezwa katika kuitangaza Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kitaifa na kimataifa.

Katika sherehe hizo mabzo zilifanyika katika chuo hicho kulifuatiwa na burudani  mbali mbali ikiwemo taarab, na ngoma za asili. 

BALOZI SEIF: DUMISHENI NIDHAMU KWENYE MICHEZO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amehimiza umuhimu wa wanamichezo kuendelea kudumisha nidhamu michezoni ili kulijengea sifa
Bora Taifa katika sekta hiyo kwa kuwa na wanamichezo walishiba maadili na heshima iliyotukuka.

Balozi Seif Ali iddi alitoa himizo hilo wakati alipokuwa akizungumza na wachezaji pamoja na Viongozi wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe { Wakombozi wa Ng’ambno } katika hafla ya kukabidhiwa Kikombe cha ubingwa baada ya Timu hiyo kupanda Daraja la kwanza Kanda mwaka huu.
Alisema nidhamu na heshima ndio kitu pekee kilichosababisha wachezaji wa enzi zilizopita hapa Zanzibar kuwika na hatimae kuiletea sifa Zanzibar katika ulimwengu wa kabumbu.

Balozi Seif alieleza kwamba Vijana wa sasa wana nafasi pana ya kuendelea kujifunza mbinu mbali mbali za michezo na hatimae kuwa mastaa ambazo hupatikana kupitia kwenye vipindi vya Televisheni pamoja na mitandao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wachezji pamoja na Viongozi wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe kutokana na kazi kubwa waliyoifanya na hatimae kuchukuwa ubingwa kwa kuingia daraja la Kwanza Kanda.

Balozi Seif alisema juhudi za wachezaji hao kwa upande mwengine zimeanza hatua mpya ya kujijengea uwezo wa kupata ajira kupitia mchezo wa soka ambao unaonekana kupendwa sana Duniani.

“ Wapo wachezaji maarufu wanaochezea timu zinazotajika Duniani katika ulimwengu wa kabumbu ambapo wengine wanatokea hata mataifa ya Afrika yanayolingana kiwango cha soka na Tanzania “ Alisema Balozi Seif.

Katika kuunga mkono wanamichezo hao wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe Balozi Seif ameahidi kuisaidia Timu hiyo Seti mbili za Jezi pamoja na Mipira Minne na akawataka wajiwekee malengo zaidi ya kufanikiwa katika fani yao hiyo kwa siku zijazo.

“ Wale Jamaa wakikuoneni mnavyolisakata soka sawa sawa kikweli watafikia hatua ya kukununueni tuu na kwa upande mwengine Zanzibar tutakuwa na haki ya kujigamba kwamba tumetoa wachezaji wanaouwezo wa kuchezea timu za Kimataifa “. Alisema Balozi Seif.

Akizungumzia suala ya ujenzi wa Jengo la kudumu la Timu hiyo ya Taifa ya Jang’ombne Balozi Seif aliwashauri Viongozi na wachezaji hao kuanza ujenzi wa msingi na yeye atakuwa tayari kusaidia matofali kwa hatua ya kunyanyua.


Alisema uwezo wa kujenga jengo lao uko mikononi mwao ambapo viongozi wao jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kwamba wanasaidia nguvu na maarifa ili kuona malengo waliyojipangia yanakwenda hatua baada ya hatua.

Mapema Rais wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe Salim Ridhiwani alisema Uongozi wa Klabu hiyo umeamuwa kuimarisha Timu hiyo ili kurejesha heshima na hadhi ya klabu hiyo iliyopotea katika miaka ya hivi karibuni.

Ridhiwani alisema Wanachama wa klabu hiyo wanajivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya klabu hiyo hasa kutokana na wachezaji wa timu hiyo kuiwezesha timu yao kuyakabili mashindano makubwa ya Kombe la Mapinduzi na kutoa upinzani mkubwa kwa timu zenye uzoefu wa mashindano ya soka Kimataifa.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mohammed Said Dimwa alisema Uongozi wa Jimbo hilo umeifufua tena Timu hiyo ndani ya Kipindi cha miaka Miwili iliyopita baada ya kufifia kutokana na changamoto kadhaa zilizokuwa zikiikabili timu hiyo katika miaka ya nyuma.

Dimwa aliahidi kwamba yeye pamoja na viongozi wenzake watasimama imara katika kuhakikisha Timu hiyo inarejea katika hadhi yake iliyopewa na wapenzi wa timu hiyo ya kuitwa wakombozi wa Ng’ambo.

Timu ya Taifa ya Jang’ombe { Wakombozi wa Ng’ambo } ilipanda Daraja na kushiriki mashindano ya Daraja la Kwanza Kanda mwaka huu baada ya kuifunga Timu ya Soka ya Maungani Goli 1-0 katika mchezo wa Mwisho wa mashindano ya Ligi Daraka la Pili.







RUKIA RAMADHANI: MSANII ASIEPENDA KUITWA MALKIA WA MIPASHO


“NIKUMBATIE mwenye wivu atazame,Nikumbatie roho yake imuume
Nikumbatie mwenye  wivu alalame,Nikumbatie akujue wangu mume
Njiani nikipita arudi kinyume nyume,Kata kiu yeye Fanta mi sina habari nae
Ajijue cheo chake mina yeye hatufanani,Atuone ashituke anijue mimi nani
Cheza na mimi mpenzi cheza name kwa helenzi,Mambo mazuri laazizi ndo hayataki haraka”
Ni moja ya beti katika nyimbo maarufu za muziki wa taarab visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wa wimbo unaojulikana kwa jina la ‘Nikumbatie’ ambao uliimwa katika kundi maarufu la East African Melody.
Maneno hayo ni miongoni mwa wimbo mzima ulioghaniwa na mwanadada mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni sie mwengine bali ni bibie Rukia Ramadhani Ali.
Rukia ni msanii mahiri katika anga la muziki wa taarab ndani nan je ya Tanzania ambae kila kona ya dunia anajulikana kutokana na kipaji chake alichojaaliwa na muumba wake.

Msanii huyo ambae hapendelei kuitwa malkia wa mipasho  kutokana na kutopendelea kuimbwa nyimbo za kupashana na kuelekeza zaidi nguvu zake katika nyimb o za mahaba na kubembeleza.
Nilipomuuliza anajiskiaje kuitwa jina hilo la malkia wa mipasho,hakuonesha bashasha wala haiba yake ya kawaida ya kutabasamu na akajibu ‘sitaki kuitwa malkia wa mipasho kwa sababu siimbi wala sifikirii kuimba mipasho’.
Jibu hilo lilinifanya nishangae kidogo kwa vile nyimbo za mipasho ndio zaidi hivi sasa zinazowapa umaarufu mkubwa  waimbaji wake kiasi cha kumuuliza nini sababu ya msimamo wake huo.
“Mimi ni msanii ninaependa zaidi taarab asilia ambayo lugha ya mashairi yake ni ya kiungwana,haina maneno makali tofauti na taarab ya kisasa,wanaimba tu lakini haina maadili ya Kizanzibari au taarab kwa ujumla,”alisema bila ya kutaka kuingia ndani zaidi.
Nilipotaka kujua alipoanzia hadi alipofikia,Rukia hakukataa tulikwenda hatua kwa hatua hadi mwisho wa mazungumzo yetu,alipoanzia alipofikia na matarajio yake ya baadae.
Msanii huyo alisema alijitosa rasmin katika fani ya muziki mwaka 1974 katikam kikundi cha Tawi la Afro Shirazi Party la Mwembeshauri chini ya mwalimu wake Marehemu Khamis Shehe.
Alisema wakati huo walikusanywa watoto wengi wa mtaani hapo kwa ajili ya kufundishwa masuala ya uimbaji na baada ya mafunzo ya muda walipelekwa majaji wenye uelewa mpana wa muziki huo na uimbaji kwa kuwachuja vijana hao.
Rukia alikuwa miongoni mwa vijanan waliopenya katika mchujo wa majaji hao na hapo ukawa mwanzo wa mafanikio  yake kwa vile kupita huko kulimfanya apelekwe katika klabu maarufu ya tab visiwani humu ya Culture Musical Club yenye maskani yake katika mtaa wa Vuga mjini Unguja.
Alianza mazoezi katika klabu hiyo na hatimae kuanza kuimba akiwa bado mwanafunzi wa shule na hivyo kuweza kubeba majukumu yake yote ya usanii na masomo shuleni.
Alisema alianza rasmin kuanza kupanda jukwaani akiwa na kundi lake la Culture na nyimbo yake ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Kukupenda sana ndilo kosa langu sitofanya tena naapa kwa Mungu,Nilioyaona yanatosha kwangu’.
Kutoka kwake huko kuliwashtua wazazi wake ambao waliona kwamba anajikita zaidi katika maswala ya nuimbaji,badala ya kuzingatia masomo yake hivyo  ilimsababishia kuhamishwa Zanzibar na kupelekwa  Dar es Salaama kuendelea na masomo.
Msanii huyo mahiri alieleza kwamba alikaa jijini humo kwa muda wa miaka minne na kuendelea na masomo katika shule ya msingi ya Temeke kabla ya kurejea Unguja kuendelea na masomo yake katika shule ya Rahaleo,Kidutani ndogo na kubwa ambapo alimalizia kidato cha nne.

Kurejea kwake Unguja kulimfanya arudie tena kwenye muziki wa taarab na kwa bahati mbaya au nzuri hakurejea tena katika kundi lake la awali bali alihamia kwenye kundi mama la Nadi Ikhwan Safaa.
Alisema akiwa ndani ya kundi hilo,lenye maskani yake katika mtaa wa Kokoni mjini Unguja alikweza kuimba nyimbo kadhaa ambazo ziliweza kumjengea  jina na kumpa umaarufu zaidi.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Nnazama, Nadra na Sadfa,Hidaya, Baada ya dhiki faraja,Niapishe na nyiengine nyingi ambazo zote hizo zinaendelea kupendwa hadi hivi sasa.
Rukia alisema kuanzishwa kwa kundi jipya la taarab la Bwawani ambalo lilikuwa linamilikiwa na hoteli ya Bwawani kulimfanya ahame katika kundi lake hilo na kuhamia katika kundi la Malindi chini ya msanii mahiri Marehemu Mwalimu Abdallah .
Alisema kikundi hicho cha Bwawani hakikudumu muda mrefu sana kwa vile kilivunjika,lakini kabla ya kuvunjika msanii huyo alifanikiwa kukiimbia kikundi hicho nyimbo kadhaa zikiwemo Nidhibiti,na Nadekea change.
Baadhi ya maneno yaliokuwemo katika nyimbo ya Nidhibiti ni kama hivi
Nidhibiti unitunze,Nitunze nihifadhike
Nihifadhi wanyamaze,Nipoe nitononoke
Raha zako nieneze,Milele milele nifarijike
Miti shamba wamalize,Halafu waweweseke.
Rukia ambae ni miongoni mwa wasanii waanzilishi wa kundi la ‘The East African Melody’ ambalo llilianzishwa nchini Dubae mwaka 1992,akiwa na wasanii kadhaa.
Akiwa nchini humo nyimbo za mwanzo alizoimba ni pamoja na Karibu habibi,Nimesharidhika na Nasubiri miujiza na baadae kundi hilo lilihama nchini Dubae na kuhamia visiwani Zanzibar.
Katikati ya mwaka 2000 msanii huyo alipumzika kuimba kwa muda wa mwaka mmoja hadi mwaka 2001 aliporejea tena kwenye ulingo wa taarab na kundi lake hilo la East African Melody.

Mara baada ya kurejea tena msanii huyo alionekana kuendelea kuvutia zaidi  kutokana na kuimba nyimbo zake kadhaa ambazo zilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi wa muziki wa taarab .
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Njoo Habibi,Nani kama wewe,Wastara hasumbuki,Kufa na tai shingoni,Nataka ridhaa yako,pamoja na nyimbo ya Nikumbatie.
Mbali na kuimba Rukia anamudu saana sanaa ya uigizaji ambapo aliwahi kuigiza mchezo wa ‘Mkombozi wa Mwafrika’ambapo alisema kwamba uimbaji uliweza kumletea matatizo kutoka kwa watu mbali mbali ikiwemo kumtishia kumpiga na hata wengine kutaka kumuwekea sumu kwenye chakula.
Pamoja na kutishiwa huko na vitisho hivyo msanii huyo alikabiliana na changamoto hizo ambazo hazikumkatisha tama na kuendelea na shughuli yake hiyo aliyokiri kuipenda ndani ya damu yake.
Rukia hakufafanua kwa nini alitishiwa,lakini alisema hayo ni mambo ya zamani na kwa sasa ayameshapita.
“Kwa kweli nilipokuwa najiunga na mambo ya sanaa nilipata tabu saana kwani nilitishiwa kupigwa na hata kuambiwa nitatiliwa sumu kwenye chakula lakini hayo yalikua mambo ya zamani sasa hivi hayapo,”alisisitiza.
Kuhusu maswala ya faida katika fani ya sanaa,Rukia alisema muziki wa taarab umeweza kumsaidia kupata faida nyingi ikiwemo umaarufu,kuheshimiwa na watu wa rika mbali mbali pamoja na kusafiri.

Alizitaja nchi alizotembelea kupitia muziki wa taarab ni pamoja na Mikoa mbali mbali ya Tanza nia,Kenya,Msumbiji,Comoro,Nigeria,Misri,Dubae,Oman,Abu Dhabi,Jamhuri ya Dominica,Ufaransa,Uswiss,Ubelgiji,Italia,Uholanzi,Slovenia,Ujerumani,Japan,Marekani na Uingereza.
Rukia alisema mpaka sasa kwa yeye ni taarab asilia ambayo ndio mwalimu wake katika fani hiyo lakini pia hiyo haimzuii kuimba taarab ya kisasa.
“Taarab asilia ndio taarab hizi nyengine tunaimba tu kufuata wakati,mimi siwezi kuidharau kwa kuwa ndiko nilipoanzia,”alifahamisha.
Akizungumzia juu ya tabia ya wasanii kuhama hama vikundi mara kwa mara ,alisematabia hiyo sio nzuri ,lakini ijulikane kwamba msanii hawezi kuhama bila ya sababu maalum.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuhama kwake hakutokani na maslahi,bali kutokana na matatizo mbali mbali yaliokuwa yakijitokeza.
Msanii huyo hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa wasanii mbali mbali ambao walimuwezesha kudumu katika fani hiyo akiwemo marehemu Asha Simai,marehemu Khamis Shehe na Mohammed ilyas.
Kwa  vile hakuna msanii yoyote ambae hana msanii anaemvutia ,kwa upande wake Rukia alisema anavutiwa na uimbaji wa wasanii wengi akiwemo marehemu Asha Simai,Marehemu Abdulaziz Yussuf na Profesa mohammed Ilyas.
“Marehemu Bi Asha Simai alikuwa akinivutia mno katika fani yake ya uimbaji hasa nyimbo ya iwapi ile ahadi, inanisuuza roho yangu Namuomba Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake,”alisema msanii huyo.
Hivi sasa Rukia Ramadhani ni muimbaji huru ambae anaimbia vikundi tofauti anapopata mualiko kikiwemo kikundi cha Zanzibar One Modern Taarab na vikundi vyengine.
Pia msanii huyo ni mwalimu wa sauti(kuimba) katika Chuo cha Muziki wa nchi za Jahazi(DCMA) ambapo aliwataka wasanii kujifunza zaidi  mara wanapoingia katika fani hiyo.
“Nawashauri wasanii kujifunza zaidi kusoma muziki ili waweze kujifahamu na kuelewa nini wanachokifanya jukwaani kwani wasanii wengi hawataki kujifunza.
Rukia Ramadhani Ali ni mtoto pekee wa bwana Ramadhani Ali na Bi Zuhura ambapo mbali na fani ya usanii lakini pia ni muajiriwa wa serikali katika Wizara ya Katiba na Sheria.