Sunday, 28 June 2015

PROFESA HAROUB: KIONGOZI MAKINI ALIEPENDA WATU NA KUSAIDIA WANYONGE


“NIKIWA hai nataka kushuhudia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,ambao ambao unafuata misingi yote ya demokrasia zaidi kwa vyombo vya habari,”.
Hiyo ni miongoni mwa kauli alizowahi kuzitoa katika uhai wake Marehemu Profesa Haroub Othman kwenye moja ya semina ya uzinduzi wa kitabu hapa visiwani Zanzibar.

Tarehe kama ya leo mwaka 2009,Tanzania iliingiwa na simanzi kubwa baada ya kuondokewa na mpiganaji na mtetezi wa haki za wanyonge Marehemu Professa Haroub Miraji Othman.

Ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ni kweli wakati ulifika,Mwenyezi Mungu (SW) alimwita nae akaitika kutokana na wito ambao mwanadaamu yoyote hana budi kuuitika.

Siku iliyofuata ya Juni 29 mwaka 2009  Watanzania walio wengi na hasa wasomi wa nchi hii waliungana na familia ya marehemu katika mazishi yake yaliofanyika nyumbani kwao Baraste na kuzikwa katika makaburi yaliopo katika kijiji cha Chuwini.

Kuondoka katika dunia hii kwa kipenzi cha wengi ilikua ni vigumu kuaminika kutokana na kuwepo kwake karibu na wanajamii pamoja na kazi yake ya kutetea haki na maslahi ya wanyonge.

Ni ukweli usiofichika kwamba marehemu Profesa Haroub ni nguzo kuu iliyo katika ghafla katika ujenzi wa demokrasia,haki,amani na utengamano Zanzibar,Tanzania,Afrika na dunia kwa ujumla.

Marehemu Profesa Haroub atakumbukwa daima kutokana na michango yake mingi ikiwemo kuhubiri haja ya kuwepo kwa mabadiliko na kuwa mwanaharakati mahiri wa sharia na haki za binaadamu na utawala bora.

Pia atakumbukwa kwa mengi mazuri hasa katika mchango wake kwa jamii akiwa ni mpiganaji wa haki za binaadamu pamoja na alikuwa anapenda kusema ukweli.

Nanukuu ile kauli ambayo nakumbuka aliitoa katika siku ya kumkumbuka aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Walemavu marehemu Maalim Khalfan Hemed Khalfan.

Marehemu Profesa Haroub alisema ‘Kama utakuwa humkumbuki mwenzako ambae ameshafika mbele ya haki,basin a wewe uhakikishe kwamba hutokumbukwa,”.


Kutokana na kauli hiyo ambayo imenivutia sana na kujaza hamasa ya kuandika makala hii,na kwa umuhimu aliokuwa nao marehemu katika nchi yetu hatuna budi sote Watanzania tumkumbuke.

Kwa mujibu wa kitabu maaraufu cha ‘Haroub Othman Farewell to the Chairman ‘kilichotungwa takriban miaka sita iliyopita mara baada ya kifo chake kutokea.

Wanasiasa,viongozi,wanasheria, wanahabari pamoja na wanafunzi wake waliweza kutoa maoni yao kutokana na umuhimu aliokuwa nao kwa nchi yake Marehemu.

Hii inaonesha wazi kuwa ni pengo kubwa sana ambalo ni gumu kuzibika kwa kipindi kifupi kutokana na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu na kuwa na umuhimu katika jamii nzima na sio kifamilia pekee.

Kitabu hicho kimemnukuu Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda alivyomueleza Profesa Haroub kuwa mtaalamu aliyebobea katika mitaala ya maendeleo nani mwanaharakati  wa haki za binaadamu ambae anafahamika ndani nan je ya nchi.

  Waziri mkuu huyo ambae alisema marehemu alikuwa mwalimu wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970 pia alimuelezea kuwa ni mtu ambae ndani na nje ya chuo hakuwa mchoyo wa kutoa elimu yake na wala ushauri wa kitaalamu.

Kutokana na kauli ya Waziri Mkuu wetu wa Tanzania kuwa marehemu alitumia vyema sana vipaji alivyokuwa navyo na karama alizojaaliwa na Mwenyezi  Mungu kwa ukamilifu bila ya majivuno,woga wa wivu.

Nae mwanahabari wa siku nyingi Salim Said Salim alimuelezea marehemu Profesa  Haroub kuwa ni mwanaharakati asiye na shaka na aliyetukuka nan i mtu wa kupigiwa mfano.

Pia alimuelezea kwamba aliweza kumfunza mambo mengi sana pamoja na kumuonesha njia ambayo anaamini kuwa ni sahihi katika maisha yake ya kila siku.
Umuhimu wa marehemu Profesa Haroub haukuonekana kwa mwanahabari Salim Said Salim,bali kwa wanahabari wengi sana miongoni mwao ni mwanahabari Haura Shamte .
Haura alimuelezea marehemu kuwa ni alama ya fikra pevu,mahiri na yenye busara pamoja na wadhifa aliokuwa nao na heshima kubwa katika jamii ya Watanzania.

Haura alimsifia marehemu kuwa pamoja na usomi aliokuwa nao,lakini hakujitenga na watu wa kawaida na alishiriki katika shughuli mbali mbali alizoarifiwa.

“Marehemu aliamini kwamba watu wote ni sawa  hakujikweza wala hakutakabari,binafsi Profesa alikuwa chanzo changu cha habari  kila nilipotingwa na jambo hasa katika masuala ya kisiasa,”alisema Haura.

Kwa upande wa kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) hawakuwa nyuma kutoa sifa njema za Marehemu Profesa kutokana na umuhimu wake katika kituo hicho akiwa akiwa mmoja wa waanzilishi wa kituo hicho.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho Iss-haq Ismail Shariff,alieleza kwamba ukweli usiofichika kuwa marehemu aliitaka Zanzibar wanaondokana na shida za kutafuta haki zao za msingi katika wakati mgumu walihitaji.


“Profesa Haroub atakumbukwa kwa dhamira yake njema ya kutaka kuwa Wazanzibari wana  uwelewa katika masuala yote ya sheria,haki za binaadamu na maendeleo,”alisema Mkurugenzi huyo.

Mbali na wasomi lakini kwa upande wa familia yake,haukuwa nyuma kutoa maoni au wasifu mzuri wa marehemu ndugu yao ambapo ndugu yake Othman Miraji Othman alimuelezea kwa kina kaka yake.

Kitabu kimefafanua kuwa Miraj alisema,Marehemu Profesa Haroub alikuwa nguzo ya familia ya ukoo wao na haikutetereka hadi mwisho wa maisha yake.

Alisema jambo lolote litakalomfikia ndugu yake au rafiki yake likiwa la furaha au msiba,marehemu ingawa alikuwa anaishi Dar es Salaam,lakini alikuwa nahudhuria katika shughuli hiyo.

Aidha ndugu huyo alimuelezea kaka yake kuwa alikuwa akiipenda sana Zanzibar na ndio sehemu aliyokuwa  akiipendelea sana kuvutia pumzi yake ya mwisho kuliko sehemu nyengine.

Mmoja wa watu waliotoa ujumbe kwa njia ya mashairi ni Jenerali Ulimwengu ambae alisema katika mashairi yake .
Haroub kenda harudi,Ndiyo yetu sote sudi
Kifo kwetu sote budi,Ahadi ikiwadia
Ela tuko kulia,Mataka kujishikia
Haroub alo azizi,katimiza yake kazi
Bila kufanya ajizi,Sote tumemridhia.


Hizi ni baadhi ya beti za utenzi uliotungwa na Jenerali Ulimwengu kwa ajili ya marehemu Brofesa Haroub Othman .

Hakuna jambo lisilokuwa muhimu kwa wananchi wa Tanzania kukumbuka mchango wa marehemu Profesa Haroub katika taaluma yake ikiwemo kufundisha taaluma ya maendeleo na mambo ya sheria kwa muda wa miaka 41.

Pia alitoa elimu katika maeneo makubwa ya ufundishaji ikiwemo haki za binaadamu,Ujenzi wa Demokrasia na utawala bora,historian a falsafa ya siasa na siasa za kusini mwa Afrika na Mashariki ya kati.

Ni vigumu kueleza mambo mengi kuhusu mchango wake kama mwanataaluma katika wasifu huu ambapo eneo moja kubwa la utafiti na ushauri,aliweza kuchapisha vitabu vingi na makala nyingi katika vitabu na majarida ya kitaifa na kimataifa.

Ni machache niliyoyaeleza kuhusu marehemu Profesa Haroub Miraj Othman ambae kwa anaemjua na asiemjua ataamini kwamba Profesa alikuwa kiungo mahiri katika jamii ya Kitanzania.

Hivyo basi hakuna budi kwa wasomi na wasiowasomi kufuata nyayo za marehemu kutokana na kuwa mhamasishaji na mpiganaji wa haki za binaadamu hasa wanyonge.

Marehemu Profesa Haroub alizaliwa Novemba 30 mwaka 1942 katika mtaa wa Baraste Kipande na kuanza masomo yake katika skuli ambayo ikijulikana kwa jina la French Comorian School ilioko katika mtaa wa Kajificheni mnamo mwaka 1949.

Mwaka 1958 marehemu alichaguliwa kujiunga na chuo cha UwalimuBeit el Rass ambapo baadae ambapo baadae alijiunga na elimu ya juu Urusi katika chuo kikuu cha Moscow ambapo huko alipata shahada hya uzamili wa sheria (LLM) mwaka 1967.

Mwaka 1969 alipata shahada ya Diploma ya sheria katika chuo kikuu cha Hague,Uholanzi na mwaka 1980 alipata shahada ya uzamivu (PHD) chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Marehemu aliajiriwa katika chuo kikuu cha Afrika Mashariki mwaka 1969 ambapo mwaka 1970 aliajiriwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam hadi pale Mwenyezi Mungu alipochukua roho yake .

Alianza kazi katika kitivo cha sheria kwa muda mfupi na baadae alihamia katika taasisi ya taluma na maendeleo.

Marehemu aliweza kushika nyadhifa mbali mbaliikiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi mwaka 1981-1982 na baadae alikuwa Mkurugenzi kamili kwa vipindi viwiwli mfululizo 1982-1988.

Pia marehemu aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UDASA pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi.

Marehemu alikuwa ni mchapa kazi,alikuwa ni mtu aliejitolea katika maisha yake na kutetea wanyonge ndani na nje ya nchi.

Marehemu Profesa Haroub kabla ya kifo kumkuta Juni 27 mwaka 2009 alishiriki katika uzinduzi wa kitabu cha ‘Race Revolution and the  Struggle’ kinachozungumzia maisha ya kisiasa ya Makamo wa Kwaza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad.

Kitabu hicho pia kinazungumzia maisha ya mwanasiasa mkongwe na Waziri wa Elimu wa zamani Ali Sultan Issa ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Baytul-Yamin uliopo Funguni mjini Unguja.

Aidha marehemu usiku wa Juni 27 hiyo hiyo alishiriki uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu kwa Nchi za Jahazi(ZIFF) ambapo mwandishi wa makala hii alibahatika kumuona siku hiyo marehemu akisalimiana na Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar,Shamsi Vuai Nahodha ambae alikuwa mgeni rasmin siku hiyo.

Profesa Haroub ambae ameacha mke ambae nae ni Profesa Saida Saleh Yahya na mtoto wao Mmoja Tahir Haroub Othman.

Alifariki dunia asubuhi ya Juni 28 mwaka 2009 kama leo na kuzikwa Juni 29 katika makaburi yaliopo kijijini kwao Chuwini.


Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amlaze mahali pema peponi Aamin.

Makala hii imepatikana kupitia kitabu maarufu cha ‘Haroub Othman Farewell to the Chairman’ kwa msaada  wa kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar 

No comments:

Post a Comment