Friday, 12 June 2015

RUKIA RAMADHANI: MSANII ASIEPENDA KUITWA MALKIA WA MIPASHO


“NIKUMBATIE mwenye wivu atazame,Nikumbatie roho yake imuume
Nikumbatie mwenye  wivu alalame,Nikumbatie akujue wangu mume
Njiani nikipita arudi kinyume nyume,Kata kiu yeye Fanta mi sina habari nae
Ajijue cheo chake mina yeye hatufanani,Atuone ashituke anijue mimi nani
Cheza na mimi mpenzi cheza name kwa helenzi,Mambo mazuri laazizi ndo hayataki haraka”
Ni moja ya beti katika nyimbo maarufu za muziki wa taarab visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wa wimbo unaojulikana kwa jina la ‘Nikumbatie’ ambao uliimwa katika kundi maarufu la East African Melody.
Maneno hayo ni miongoni mwa wimbo mzima ulioghaniwa na mwanadada mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni sie mwengine bali ni bibie Rukia Ramadhani Ali.
Rukia ni msanii mahiri katika anga la muziki wa taarab ndani nan je ya Tanzania ambae kila kona ya dunia anajulikana kutokana na kipaji chake alichojaaliwa na muumba wake.

Msanii huyo ambae hapendelei kuitwa malkia wa mipasho  kutokana na kutopendelea kuimbwa nyimbo za kupashana na kuelekeza zaidi nguvu zake katika nyimb o za mahaba na kubembeleza.
Nilipomuuliza anajiskiaje kuitwa jina hilo la malkia wa mipasho,hakuonesha bashasha wala haiba yake ya kawaida ya kutabasamu na akajibu ‘sitaki kuitwa malkia wa mipasho kwa sababu siimbi wala sifikirii kuimba mipasho’.
Jibu hilo lilinifanya nishangae kidogo kwa vile nyimbo za mipasho ndio zaidi hivi sasa zinazowapa umaarufu mkubwa  waimbaji wake kiasi cha kumuuliza nini sababu ya msimamo wake huo.
“Mimi ni msanii ninaependa zaidi taarab asilia ambayo lugha ya mashairi yake ni ya kiungwana,haina maneno makali tofauti na taarab ya kisasa,wanaimba tu lakini haina maadili ya Kizanzibari au taarab kwa ujumla,”alisema bila ya kutaka kuingia ndani zaidi.
Nilipotaka kujua alipoanzia hadi alipofikia,Rukia hakukataa tulikwenda hatua kwa hatua hadi mwisho wa mazungumzo yetu,alipoanzia alipofikia na matarajio yake ya baadae.
Msanii huyo alisema alijitosa rasmin katika fani ya muziki mwaka 1974 katikam kikundi cha Tawi la Afro Shirazi Party la Mwembeshauri chini ya mwalimu wake Marehemu Khamis Shehe.
Alisema wakati huo walikusanywa watoto wengi wa mtaani hapo kwa ajili ya kufundishwa masuala ya uimbaji na baada ya mafunzo ya muda walipelekwa majaji wenye uelewa mpana wa muziki huo na uimbaji kwa kuwachuja vijana hao.
Rukia alikuwa miongoni mwa vijanan waliopenya katika mchujo wa majaji hao na hapo ukawa mwanzo wa mafanikio  yake kwa vile kupita huko kulimfanya apelekwe katika klabu maarufu ya tab visiwani humu ya Culture Musical Club yenye maskani yake katika mtaa wa Vuga mjini Unguja.
Alianza mazoezi katika klabu hiyo na hatimae kuanza kuimba akiwa bado mwanafunzi wa shule na hivyo kuweza kubeba majukumu yake yote ya usanii na masomo shuleni.
Alisema alianza rasmin kuanza kupanda jukwaani akiwa na kundi lake la Culture na nyimbo yake ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Kukupenda sana ndilo kosa langu sitofanya tena naapa kwa Mungu,Nilioyaona yanatosha kwangu’.
Kutoka kwake huko kuliwashtua wazazi wake ambao waliona kwamba anajikita zaidi katika maswala ya nuimbaji,badala ya kuzingatia masomo yake hivyo  ilimsababishia kuhamishwa Zanzibar na kupelekwa  Dar es Salaama kuendelea na masomo.
Msanii huyo mahiri alieleza kwamba alikaa jijini humo kwa muda wa miaka minne na kuendelea na masomo katika shule ya msingi ya Temeke kabla ya kurejea Unguja kuendelea na masomo yake katika shule ya Rahaleo,Kidutani ndogo na kubwa ambapo alimalizia kidato cha nne.

Kurejea kwake Unguja kulimfanya arudie tena kwenye muziki wa taarab na kwa bahati mbaya au nzuri hakurejea tena katika kundi lake la awali bali alihamia kwenye kundi mama la Nadi Ikhwan Safaa.
Alisema akiwa ndani ya kundi hilo,lenye maskani yake katika mtaa wa Kokoni mjini Unguja alikweza kuimba nyimbo kadhaa ambazo ziliweza kumjengea  jina na kumpa umaarufu zaidi.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Nnazama, Nadra na Sadfa,Hidaya, Baada ya dhiki faraja,Niapishe na nyiengine nyingi ambazo zote hizo zinaendelea kupendwa hadi hivi sasa.
Rukia alisema kuanzishwa kwa kundi jipya la taarab la Bwawani ambalo lilikuwa linamilikiwa na hoteli ya Bwawani kulimfanya ahame katika kundi lake hilo na kuhamia katika kundi la Malindi chini ya msanii mahiri Marehemu Mwalimu Abdallah .
Alisema kikundi hicho cha Bwawani hakikudumu muda mrefu sana kwa vile kilivunjika,lakini kabla ya kuvunjika msanii huyo alifanikiwa kukiimbia kikundi hicho nyimbo kadhaa zikiwemo Nidhibiti,na Nadekea change.
Baadhi ya maneno yaliokuwemo katika nyimbo ya Nidhibiti ni kama hivi
Nidhibiti unitunze,Nitunze nihifadhike
Nihifadhi wanyamaze,Nipoe nitononoke
Raha zako nieneze,Milele milele nifarijike
Miti shamba wamalize,Halafu waweweseke.
Rukia ambae ni miongoni mwa wasanii waanzilishi wa kundi la ‘The East African Melody’ ambalo llilianzishwa nchini Dubae mwaka 1992,akiwa na wasanii kadhaa.
Akiwa nchini humo nyimbo za mwanzo alizoimba ni pamoja na Karibu habibi,Nimesharidhika na Nasubiri miujiza na baadae kundi hilo lilihama nchini Dubae na kuhamia visiwani Zanzibar.
Katikati ya mwaka 2000 msanii huyo alipumzika kuimba kwa muda wa mwaka mmoja hadi mwaka 2001 aliporejea tena kwenye ulingo wa taarab na kundi lake hilo la East African Melody.

Mara baada ya kurejea tena msanii huyo alionekana kuendelea kuvutia zaidi  kutokana na kuimba nyimbo zake kadhaa ambazo zilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi wa muziki wa taarab .
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Njoo Habibi,Nani kama wewe,Wastara hasumbuki,Kufa na tai shingoni,Nataka ridhaa yako,pamoja na nyimbo ya Nikumbatie.
Mbali na kuimba Rukia anamudu saana sanaa ya uigizaji ambapo aliwahi kuigiza mchezo wa ‘Mkombozi wa Mwafrika’ambapo alisema kwamba uimbaji uliweza kumletea matatizo kutoka kwa watu mbali mbali ikiwemo kumtishia kumpiga na hata wengine kutaka kumuwekea sumu kwenye chakula.
Pamoja na kutishiwa huko na vitisho hivyo msanii huyo alikabiliana na changamoto hizo ambazo hazikumkatisha tama na kuendelea na shughuli yake hiyo aliyokiri kuipenda ndani ya damu yake.
Rukia hakufafanua kwa nini alitishiwa,lakini alisema hayo ni mambo ya zamani na kwa sasa ayameshapita.
“Kwa kweli nilipokuwa najiunga na mambo ya sanaa nilipata tabu saana kwani nilitishiwa kupigwa na hata kuambiwa nitatiliwa sumu kwenye chakula lakini hayo yalikua mambo ya zamani sasa hivi hayapo,”alisisitiza.
Kuhusu maswala ya faida katika fani ya sanaa,Rukia alisema muziki wa taarab umeweza kumsaidia kupata faida nyingi ikiwemo umaarufu,kuheshimiwa na watu wa rika mbali mbali pamoja na kusafiri.

Alizitaja nchi alizotembelea kupitia muziki wa taarab ni pamoja na Mikoa mbali mbali ya Tanza nia,Kenya,Msumbiji,Comoro,Nigeria,Misri,Dubae,Oman,Abu Dhabi,Jamhuri ya Dominica,Ufaransa,Uswiss,Ubelgiji,Italia,Uholanzi,Slovenia,Ujerumani,Japan,Marekani na Uingereza.
Rukia alisema mpaka sasa kwa yeye ni taarab asilia ambayo ndio mwalimu wake katika fani hiyo lakini pia hiyo haimzuii kuimba taarab ya kisasa.
“Taarab asilia ndio taarab hizi nyengine tunaimba tu kufuata wakati,mimi siwezi kuidharau kwa kuwa ndiko nilipoanzia,”alifahamisha.
Akizungumzia juu ya tabia ya wasanii kuhama hama vikundi mara kwa mara ,alisematabia hiyo sio nzuri ,lakini ijulikane kwamba msanii hawezi kuhama bila ya sababu maalum.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuhama kwake hakutokani na maslahi,bali kutokana na matatizo mbali mbali yaliokuwa yakijitokeza.
Msanii huyo hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa wasanii mbali mbali ambao walimuwezesha kudumu katika fani hiyo akiwemo marehemu Asha Simai,marehemu Khamis Shehe na Mohammed ilyas.
Kwa  vile hakuna msanii yoyote ambae hana msanii anaemvutia ,kwa upande wake Rukia alisema anavutiwa na uimbaji wa wasanii wengi akiwemo marehemu Asha Simai,Marehemu Abdulaziz Yussuf na Profesa mohammed Ilyas.
“Marehemu Bi Asha Simai alikuwa akinivutia mno katika fani yake ya uimbaji hasa nyimbo ya iwapi ile ahadi, inanisuuza roho yangu Namuomba Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake,”alisema msanii huyo.
Hivi sasa Rukia Ramadhani ni muimbaji huru ambae anaimbia vikundi tofauti anapopata mualiko kikiwemo kikundi cha Zanzibar One Modern Taarab na vikundi vyengine.
Pia msanii huyo ni mwalimu wa sauti(kuimba) katika Chuo cha Muziki wa nchi za Jahazi(DCMA) ambapo aliwataka wasanii kujifunza zaidi  mara wanapoingia katika fani hiyo.
“Nawashauri wasanii kujifunza zaidi kusoma muziki ili waweze kujifahamu na kuelewa nini wanachokifanya jukwaani kwani wasanii wengi hawataki kujifunza.
Rukia Ramadhani Ali ni mtoto pekee wa bwana Ramadhani Ali na Bi Zuhura ambapo mbali na fani ya usanii lakini pia ni muajiriwa wa serikali katika Wizara ya Katiba na Sheria.


No comments:

Post a Comment