“ NAFARIJIKA
mno kuona kazi zangu za kisanii katika fani ya muziki wa taarab na nimepata
heshima kubwa,hivyo najivunia kutimiza miaka 51 jukwaani pamoja na kupata
nafasi kubwa ya kutoa elimu ya muziki,”.
Maneno hayo
yametoka kinywani mwa msanii maarufu na gwiji wa kutunga na kuimba nyimbo za
taarab asilia visiwani hapa,Mohammed Ilyas Amirdin.
Bila shaka
jina hilo sio geni miongoni mwa mashabiki wa taarab katika ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati na hata barani Ulaya na katika Nchi kadhaa za Kiarabu.
Umashuhuri
wa mkongwe huyo ambae hivi sasa ametimiza miaka 51 tangu ajitumbukize katika
usanii huo,unatokana na ujuzi kipaji alichonacho pamoja na sauti nzito yenye
mvuto wa kipekee na inayoweza kumtoa nyoka pangoni pamoja na kuwavutia walioko
mbali.
Akizungumza
na mwandishi wa makala hii,Ilyas alisema chimbuko la umahiri wake lilianzia
katika fani ya kusoma kitabu cha Quraan kwa njia ya Tajweed pamoja na pamoja na
kughani kasida akiwa kijana mdogo.
Alieleza
kwamba wakati akiwa darasa la sita katika shule ya Darajani mwaka 1962
alijiunga rasmin katika tasnia ya muziki kwa kujumuika na kikundi cha watoto
wadogo kilichoanzishwa na marehemu Maalim Iddi Abdallah Farahan pamoja na
mkewe.
Alisema
katika kikundi hicho walikuwemo wasanii wengi akiwemo Mukrim Hamdan,Ahmed
Tahir,Saleh Hassan Sheikh,pamoja na watoto wa marehemu Iddi Farahan
Suleiman na Bashir.
Kwa mujibu
wa maelezo yake kwa mara ya kwanza kupanda jukwaani na kuimba ilikuwa mwaka
1965 katika ukumbi wa Sayyid Khalifa ambao kwa sasa ni jengo la Shirika la
Utangazaji Zanzibar ZBC Televisheni ambapo aliimba wimbo aliotunga mwenyewe
uliojulikana kwa jina la ‘Ua la kijani’.
Ingawa siku
hiyo ilikuwa ndo mwanzo kutolewa ukumbini,sauti yake na namna alivyolimudu
jukwaa iliwavutia wasanii maarufu wakati huo marehemu Iddi Farahi na marehemu
Maalim Seif Salim.
“Kutokana na
kile nilichokionyesha siku ile ya mwanzo,walimu wangu walinishauri nijiunge na
Nadi Ikhwan Safaa na bila ajizi nilikuwa na hiyo ikawa hatua yangu ya kwanza
kuelekea katika mafanikio niliyonayo sasa,”alisema.
Msanii huyo
alisema akiwa ndani ya kundi hilo alibahatika kukutana na wasanii wengi mahiri
akiwemo marehemu Maulid Machaprala,Mohammed Seif Khatib,Mohammed Ahmed,Abdallah
Issa,Salum Kassim Nihifadhi Abdallah na wengine wengi.
Awali
alipojiunga na kundi hilo,Ilyas alisema kwamba wasanii wake walikuwa wkaiimba
nyimbo zenye kuelezea maudhui ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Mnamo mwaka
1968 Ilyas alitunga wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Umeumbuka ‘ukiwa wa kwanza
tangu ajiunge na kundi hilo ambalo hivi sasa linatimiza miaka 111 tangu
kuzaliwa kwake.
“Nilipojiunga
na Nadi Ikhwan Safaa tulikuwa tunaimba nyimbo za Mapinduzi,lakini mwaka 1968
tulianza kutunga nyimbo za kawaida na mimi nilitunga nyimbo ilojulikana kwa
jina la Umeumbika,”alifafanua.
Baadae
alifahamisha kwamba msanii Jawad Ibrahim ambae kwa sasa anaishi nchini Muscat
Oman,alimtungia wimbo uliokua ukijulikana kwa jina la ‘Tone la mvua’ ambao pia
ulimpatia umaarufu zaidi kutokana na maudhui yake.
Aidha Ilyas
ambae amevishwa joho la kuitwa Profesa alieleza kwamba aliweza kumtungia
wimbo mwalimu wake marehemu Seif Salim
uliokuwa ukijulikana kwa jina la ‘Cheka uondoe shaka’.
Baadae
msanii huyo gwiji aliweza kuhama visiwani Zanzibar na kuhamia jijini Dar es
Salaama kwa kujiunga na kundi la Al-Wattan ingawa hapo hakuwahi kutunga nyimbo
bali alikuwa akighani wimbo wake wa Umeumbika ambao alitokana nao visiwani
Zanzibar.
Umahiri
wake,na uwezo wa kuimiliki sauti yake anapokuwa jukwaani haukuonekana na
wapenzi wa taarab Zanzibar pekee,bali pia ulivuka bahari na kufika ng’ambo ya
visiwa vya Marashi ya karafuu vya Unguja na Pemba.
Hilo
lilithibitishwa na kuchukuliwa kwake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
wakati huo Mustafa Songambele,ili aende akanzishe kikundi cha taarab mkoani
humo.
Alipofika
Mkoani humo aliweza kuanzisha kundi lililokuwa likijulikana kwa jina la
‘Shinyanga Musical Club kundi ambalo aliweza kudumu nalo kwa muda wa miaka
minne.
Ilyas
alidhihirisha uwezo wake pale alipolitungia wimbo kundi hilo ambao wimbo huo
aliupa jina la ‘Ninaishi na waridi’ ambao alisema uliwavutia wengi na
kumuongezea mashabiki.
Kwa kuwa
umuhimu wa kujifunza zaidi upo pahali popote,hatimae Ilyas alirejea jijini Dar
es Salaam na kujiunga na Brass Band ya Jeshi la Polisiili kujiendeleza katika
fani hiyo ambapo hapo pia alikaa kwa muda wa miaka minne.
Baada ya
hapo Profesa Ilyas alirejea visiwani Zanzibar kujumuika na wenzake wa Nadi
Ikhwan Safaa (Malindi) na hapo ndipo alipoweza kutunga nyimbo nyingi sana
pamoja na kutia muziki.
Profesa
alisema kwamba akiwa hapo,aliweza kutunga nyimbo zaidi ya 40 ambazo ziliimbwa
na waimbaji mahiri na mashuhuri hapa visiwani kama vile Rukia
Ramadhan,Mwanahawa Ali,Marehemu Machaprala na wengine wengi.
Alizitaja
baadhi ya nyimbo alizotunga yeye mwenyewe pamoja na kutia muziki ni pamoja na
Usiku wa fadhila,Njoo kwa mtu mkweli,Mwana wa mwenzio,Siri ya moyoni,Ameniteka
na nyengine nyingi.
Katika
mikakati ya kujiimarisha zaidi kimuziki,mwaka 1990 msanii huyo aliunda kikundi chake mwenyewe
cha Twinkling Star(Nyota zameremeta) pamoja wenzake kadhaa akiwemo Seif Salim, Ally Bassalama, Juma
Chanichi,Abdulaziz Yussuf ambao hao wote
wameshatangulia mbele ya haki.
Baadhi ya
vibao vilivyotamba na kupendwa na wengi ni pamoja na Bahati haina kwao,Moyoni
sina nafasi,Nisafirishe kwa huba na kadhalika.
Baadhi ya
maneno yaliokuwemo katika wimbo wa Moyoni sina nafasi ni kama ifuatavyo.
Moyoni sina
nafasi,Kuweka nongwa na chuki
Wala silipi
kisasi ,Kufanya hivyo sitaki
Kugombana
nina hisi,Nnapotoka siogopi
Kipaji,umahiri,moyo
wa kujituma na kutunga nyimbo nyingi bora
ni mambo yaliomuinua sana mkongwe huyo na kutokana na sifa hizo aliwahi
kutumiwa barua ya pongezi kutoka kwa Malikia Elizabeth wa Uingereza.
“Nashukuru
sana katika nyimbo nilizotunga kwenye kikundi cha Nyota zameremeta
zilizniwezesha kupata barua nyingi sana za pongezi pamoja na ile iliyotoka kwa
Malkia wa Uingereza kutambua kmipaji changu hii ni faraja kubwa
kwangu,”alisema.
Lakini
pamoja na mafanikio hakuna jambo linalokosa changamoto,ingawa katika hili Ilyas
alisema matatizo aliyokuwa akiyapata hayakumpa tabu kwa vile aliweza kuyakabili
na kuyachukulia kama ni sehemu ya kazi.
Nilipomuliza
ni faida gani alizozipata katika harakati za usanii,mwanamuziki huyo alisema ni
pamoja na umaarufu ndani nan je ya Zanzibar,kuheshimiwa na watu wa rika tofauti
sambamba na kutembea nchi mbali mbali duniani.
Alizitaja
nchi ambazo alizowahi kufika kwa kazi ya usanii ni pamoja na Oman,Dubae,Visiwa
vya Comoro,Uingereza,Ujarumani,Ufaransa,Italia Finland, Kenya na nyengine
nyingi.
Mtu akiwa
msanii au unashiriki katika fani yoyote hukosi wasanii wanaokuvutia au
kuwashabikia.
Kwa upande
wa Prefesa Ilyas aliwataja wasanii wanaomgusa ni pamoja na Rukia
Ramadhani,Sabah Muchacho na marehemu Seif Salim.
Aidha
hakuweza kuficha mapenzi yake kwa wasanii wanaoimba nyimbo za kiarabu akina
Mohammed Abdulwahab,Ummu Kulthum,na Abdelhalim Hafidh ambao wote ni marehemu
pia alisema anavutiwa na waimbaji wa kizungu kama Julio Iglasius na Elvis Presley.
Akizungumzia
dhana iliyo mawazo mwa wengi,kuwa muziki ni uhuni,Profesa Ilyas alipinga vikali
na kusema kwamba na kusema kwamba uhuni ni tabia ya mtu mwenyewe kwa vile kwa
vile wapo wahuni ambao hawana uhusiano na mambo ya muziki.
“Hili la
kuwa muziki ni uhuni nalipinga hadi mwisho wa dunia,hizi ni tabia ambazo mtu
huamua kujitumbukiza hata kama sio mwanamuziki tunawaona wengi wa aina
hiyo,”alifahamisha.
Kuhusu aina
mpya ya taarab iliyoingia nchini na pengine duniani sasa,alidai hakuna kitu
kama hicho ‘modern taarab’ bali huo ni muziki unaoengezwa vionjo kwa kutumia
ala za kisasa baada ya zile za asili.
Mbali na
kujihusisha na usanii hapa nchini,Profesa Ilyas aliwahi kuajiriwa katika Idhaa
ya Kiswahili ya Ujerumani(DW) akiwa msomaji wa mashairi na tenzi na kuandaa
makala za utamaduni.
Ilyas
alielezwa kutopendezwa na mtindo wa vikundi vya taarab ambavyo wasanii wake
hawataki kujituma kwa kutunga nyimbo zao lakini wanategema nyimbo za wengine na
hata kuzinunua na kuziita zao .
“Huu sio
mtindo mzuri,usanii ni kutumia akili kwa kutunga vitu vipya mtu anapochukua kazi
za mwengine kuita yako bado unampa umaarufu aliyeitengeneza,nawaomba wasanii
waache tabia kama hiyo kama wanataka kuendelea,”alisema.
Aidha alitoa
wito kwa Serikali kupitia Ofisi za Hakimiliki(COSOZA) kuzidisha mikakati katika
kusimamia na kulinda haki za wasanii ili zisiwanufaishe watu wajanja wanaokula
migongoni mwao.
Alielezea
miongoni mwa mambo yanayochangia tasnia ya taarab isikue ni ushirikiano mdogo
kati ya wasanii na Serikali .
Hata hivyo
Profesa Ilyas alimpongeza aliekuwa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo,Ali
Juma Shamuhuna,kutokana na msaada wake mkubwa aliompa hadi kufika kupata barua
ya Malkia.
Gwiji huyo
alizaliwa Zanzibar katika mtaa wa Vikokotoni mwezi Machi tarehe 23 mwaka 1952
akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto watano wanaume wawili na wanawake
watatu.
Alianza
masomo mwaka 1958 katika shule ya Darajani kuanzia darasa la kwanza hadi la
nane .
Pamoja na
kundi lake na Nyota zameremeta,pia anasaidia kuwafundisha wasanii wa kikundi
cha wanawake cha Tausi Women Taarab kinachoongozwa na Mkurugenzi wake Maryam
Hamdan na pia hupiga muziki na wasanii kadhaa katika hoteli ya Serena Inn.
No comments:
Post a Comment