Tuesday, 30 June 2015

AL-MARHUM SHEIKH BAKATHIR: NGUZO IMARA ILIYOITANGAZA VYEMA ZANZIBAR KATIKA MWASWALA YA DINI YA KIISLAM


ZANZIBAR ni moja ya nchi maarufu zilizobarikiwa kuwa na wanazuoni wengi ambao waliweweza kuitangaza vyema nchi hii kutokana na kutoa elimu ya dini ya Kiislamu kwa vijana nwa ndani na nje ya nchi hii.

Kama utataka kutaja majina yao pamoja na sifa walizokuwa nazo katikamkutekeleza na kuutangaza Uisalmu,basi huwezi kuwamaliza kutokana na wingi wao ambao ndio ulioifanya Zanzibar kuwa mashuhuri katika maswala ya dini ya Kiislamu.

Miongoni mwa wanazuoni hao ni pamoja na Marehemu Sheikh Abdallah Abubakar Abdalla Muhammad Bakathir,ambae nae ni mmoja wa wanazuoni maarufu visiwani Zanzibar ambae ameshafika mbele ya haki lakini bado mafunzo yake aliyokuwa akiyatoa yanaendelea kufanyiwa kazi.
“Rabananfaa nabimaa lamtana,Rabi alli nalladhian fahuna,Rabi fakih na wafakih ahlana,Wakaraba tilanafai didinaa,Maahli kutri untha wazaka,Rabi wafiq na wawafiq hulima,Trtadhika huwalwafiila lkarama.

Hii ni dunia maarufu katika kipindi hichi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo mara baada ya kumaliza kwa darsa ya tafsiri ya Quraan kipindi hicho kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC) husomwa dua hiyo.

Dua hiyo ambayo ni maarufu sana kwa waumini wa dini ya Kiislam katika masikio yao,ambapo kama huwezi kujua kwamba dua hiyo ilirekodiwa na marehemu Maalim Abdalla Abubakar Bakathir.

Maalim Bakathir ni mmoja wa wanazuoni maarufu ambao ametoa elimu ya dini ya Kiislamu ikiwemo kitabu cha Quraan kwa vijana wengi ambao hivi sasa wameweza kushika nafasi yake kuwa walimu maarufu.

Mwandishi wa makala hii alibahatika kukutana na mmoja wa wanafunzo wake ambae kwa sasa ni Mwalimu mkuu wa Madrasat Noor ambayo ilianzishwa na yeye marehemu,Maalim Abdulrahman Sheikh Al-habshi na kumuelezea historia ya marehemu Maalim Bakathir.

Marehemu Maalim Abdalla Bakathir alizaliwa mwaka 1941 hapa hapa Zanzibar akiwa ni mtoto pekee wa mwanachuo maarufu Marehemu Sheikh Abubakar Abdalla Bakathir ambapo pia babu wa marehemu alikuwa mwanachuoni.

Baada ya kutimiza miaka miwili baba wa marehemu Maalim Bakathir alifariki duni na kulelewa na aliekuwa mwanafunzi wa baba yake marehemu Sheikh Muhammad Bin Omar Al-Khatib maarufu ‘Bwana wa Shangani’ pamoja na mkewe Bi Khadija Bint Abdalla ambae alikuwa shangazi wa Maalim Bakathir.

Kuhusu maisha yake ya elimu ya dini marehemu Maalim Bakathir alianza akiwa na umri mdogo ambapo elimu hiyo aliipata kutoka kwa wlaimu wake wakiwemo akina marehemu Maalim Himid Hajj Abdalla,Maalim Abdalla Muadhin na Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka).

Baadae marehemu Maalim Bakathir alipata nafasi ya kwenda kuongeza elimu ya dini ya Kiislamu huko Lamu Mombasa Kenya ambapo pia alibahatika kupata elimu kutoka kwa wanazuoni maarufu akiwemo Sayyid Bahasany,Shariff Al-Aididi na Sayyid Ally Badawi.

Baada ya kupata elimu kwa wanazuoni mbali mbali wa ndani nan je ya Zanzibar kuanzia miaka ya 1960,marehemu Maalim Bakathir alianza kusomesha Quraan Madrassat Sunni Cuth ambapo kwa sasa unajulikana kwa jina la Masjin Hanaffy uliopo Mkunazini ambapo aliajiriwa kusomesha watoto wenye asili ya kihindi.

Mnamo Machi 1 mwaka 1967 Marehemu alianzisha Madrassat Noor hapo hapo Masjid Hanafy na kuanza kusomesha watoto wa makabila mbali mbali yalioko visiwani Zanzibar.

Mbali na kuwa mwalimu wa Madrassa,Marehemu pia aliweza kufungua Darsa baina ya Sala ya Magharib na Isha huko Masjid Jibril mnamo miaka ya 1991 na 1992.

Marehemu aliendelea na darsa hiyo pamoja na madrassa hiyo hadi mwaka 1988 alipostaafu na kuwaachia wanafunzi wake wakiwemo marehemu Mohammed Majid,Ustadh Khalid Mohammed Mrisho na Maalim Abdulrahman Sheikh Al-habshi nay eye alibakia kuwa mlezi.

“Mimi na wenzangu ndio tuliokuwa wanafunzi wake ambapo alituachia darsa pamoja na chuo kwa ajili ya kuendeleza na kwa uwezo wa Allah (S.W) bado tunaendeleza elimu hiyo aliyotupa kuwapa na wengine ,”alisema Maalim Abdulrahman.
Pia marehemu Maalim Bakathir aliwahi kuwa mwalimu wa Quraan kwa wanafunzi wenye asili ya Kibohora.


Aidha mbali ya kuwa mwalimu wa Madrassa,lakini pia marehemu aliwahi kuwa mwalimu wa skuli mnamo mwaka 1970 ambapo alisomesha katika skuli ya Hamamni akiwa mwalimu wa dini.

Marehemu Maalim Bakathir aliweza kusimamia mambo mengi ya kheri ikiwemo kusimamia maswala ya sadaka,kujenga miskiti na vyuo vya quraan,aliwahi kuwa Mjumbe wa kamati nyingi za kidini ikiwemo kamati ya Zaka pamoja na kuwa Mjumbe wa bodi ya Wakfu na mali ya amana.

Ilipofika Juni 4 mwaka 2000 Maalim Bakathir alifariki dunia huko nchini India ambapo alikwenda kwa ajili ya matibabu na kuzikwa katika makaburi ambayo wamezikwa wazee wake hapo Ukutani mjini Unguja.

Marehemu Maalim Abdalla Bakathir atakumbukwa kwa mambo mengi ya kheri aliyoyafanya katika visiwa vya Zanzibar ikiwemo kusomesha na kutoa wanafunzi mbali mbali waliotawanyika ndani nan je ya Zanzibar.

Pia alikuwa msimamizi wa Masjid Jibril baada ya kuondoka Maalim wake Maalim Himid kwa kuhamia jijini Dar es Salaam.

Marehemu Bakathir ni mtu mmoja ambae anaendelea na ataendelea kukumbukwa kutokana na mambo mengi ya kheri ikiwemo utenzi wa Miraj ambao ulirekodiwa na kusomwa kila mwaka ifikapo siku hiyo na ZBC Radio.

Aidha katika fani nyengine aliwahi kuwa mtunzi wa mashairi ya kidini ambayo alikuwa akisoma yeye mwenyewe na pia alikuwa mtunzi wa mashairi ya kisiasa lakini hayo alikuwa hasomi mwenyewe.

Marehemu Maalim Bakathir aliwahi kuoa na kupata mtoto mmoja wa kiume ambapo mtoto huyo alifariki akiwa na umri wa miaka 18 mwaka 1991 hivyo marehemu mpaka anakufa hakua na mtoto .

Hii ni faraja kwa Wazanzibari kupata mambo mengi ya dini ambayo yameweza kusaidia kudumisha na kuendeleza uislamu katika vuisiwa hivi.

Kutokana na baadhi ya mamabo aliyoyafanya katika kulingania dini ya kiislamu na kuitangaza Zanzibar kwa kutoa vijana wengi ambao bado wanaendeleza mambo ya kheri aliyoyaacha,Inshaallah Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amuondoshee kiza cha kaburi Aamin


Wabilahi Taufiq. 

No comments:

Post a Comment