Thursday, 11 June 2015

ABDULWAKATI: NYOTA ISIYOSAHAULIKA KATIKA FANI YA SOKA NA TENISS


ZANZIBAR ni moja ya nchi ambazo zimejaaliwa kuwa na vipaji vya aina mbali mbali,vikiwemo vya utunzi,ufinyanzi na hata katika maswala ya michezo,ambayo kwa kiasi fulani ilitamba katika michezo ya aina tofauti.

Miongoni mwa watu waliotamba visiwani humu katika mchezo wa soka na mpira wa mezani Abdullah Juma Aley almaaruf Abdulwakati ambae aliweza kuitikisa Zanzibar nan chi nyengine duniani michezo hiyo.

Kama utataja majina ya watu waliowahi kutamba visiwani humu katika mchezo wa mpira wa meza na soka bila ya kumtaja Abdulwakati itakuwa hukumaliza idadi yao.

Abdullah Juma Aley ndio jina lake alilopewa na wazazi wake,lakini hata hivyo jina hilo linafahamika kwa watu waliokuwa sio wengi kwani ukipita katika mitaa mingi ya visiwani humu ikiwemo Kikwajuni na kumtaja jina la Abdullah hutompata mpaka utaje Abdulwakati.

Jina hilo ndio limekuwa maaarufu kuliko jina lake halisi kwa kipindi chote alichocheza michezo hiyo Zanzibar,Tanzania,Afrika Mashariki na hata Arabuni .
Mwandishi wa makala haya alimtafuta mwanamichezo huyo huko nyumbani kwake Michenzani na kuzungumza nae kwa kina katika mambo mbali mbali yanayomuhusu yeye kimichezo.

Alisema kwamba umaarufu wa jina la Abdulwakati hautokani na kitu chochote isipokuwa ni mchezo wa soka ambao ulimpatia umaarufu mwaka 1980 na kuendelea.
Alisema kwamba jina la Abdulwakati alilipata wakati alipokuwa mdogo akichezea timu ya hero Boys ambapo alisema jina hilo alibatizwa na mwalimu wake wa soka Abubakar Soni.

“Katika timu yetu kulikujwa na wachezaji watatu na wote walikiuwa na majina ya Abdul ,hivyo kutotufautisha sisi akaamua mimi kuniita Abdulwakati  kwa vile nilikuwa nachezea nafasi ya mshambuliaji wa kati,”alisema.

Mchezaji huyo mkongwe ambae kwa kawaida ni mcheshi,alisema wachezaji wenzake walibatizwa majina mengine kama vile Abdul Kikono na Abdul Kifupi.

Katika maisha yake ya soka,alianza kung’ara mapema utotoni mpaka kupewa mikoba ya unahodha kwenye timu ya shule visiwani Zanzibar.

Aliendelea kucheza timu ya watoto kabla ya kujiunga na klabu ya Everton iliyokuwa na maskani yake katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja  mnamo mwaka 1970.

Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata kabumbu Abdulwakati alichukuliwa na timu iliyokuwa ikimilikiwa na kituo cha kulelea watoto cha Forodhan iliokuwa ikijulikana kwa jina la Karume Boys na kutembea nayo katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Timu hiyo ambayo ilikuwa chini ya uangalizi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehem Mzee Abeid Aman Karume ambapo timu hiyo ilikuja kugawanyika mara baada ya kifo cha kiongozi huyo mwaka 1972.

Akiwa katika kikosi hicho cha Karume Boys alikutana na wachezaji wengi akiwemo Sihaba Saadat,Omar Willium na wengine wengi.

Mnamo mwaka 1972 baada ya kusambaratika kwa Karume Boys,Abdulwakati alijiunga na kikosi cha Small Simba baada ya kushawishiwa kufanya hivyo na kocha wa zamani wa kikosi hicho ,Masoud Salim almaarud Maoud Kocha.


Kutokana na ari,jitihada na moyo wake wa kusakata kabumbu wakati anapokuwa uwanjani,veteran huyo alichaguliwa kujiunga na timu ya Taifa ya vijana ya Zanzibar mwaka huo huo 1972.

Akiwa na Small Simba,Abdulwakati alikuwa kivutio kikubwa sawa na wachezaji wote wa timu hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa baada ya kupanda daraja,ambapo ilianza kwa moto mkubwa na kutikisa vigogo vya soka nchini.

Alisema timu yao ilikuwa imesheheni vipaji na kuwa gumzo la mji na kuanza kujitwalia ubingwa wa soka visiwani mwaka mwaka huo huo waliopanda ngazi 1983.
Chini ya nyota mahiri akiwemo wakati,Small Simba iliweza kutamba vilivyo katika miaka 1985 hadi 1987.

“Kuanzia mwaka 1983 hapo moto wetu ulikuwa hauzimiki na mashabiki wetu wakapata wimbo wa ‘Moto Small’ambapo kila tulipokuwa tunashuka dimbani au watu walipokuwa wakizungumzia timu yetu waliimba Moto Small,alisema mwanandinga huyo.

Jambo ambalo nyota huyo atabaki akilikumbuka maishani kwake ni tukio la mwaka 1987 kwa timu ya Small Simba kupokonywa ubingwa na Miembeni ambao walikwenda mahakamani.

Anasema anafahamu kwanini walishindwa kesi hiyo na kila mmoja alijua kutokana na hakimu wa kesi hiyo alikuwa Miembeni damu,hivyo alisema haki haikutendeka.

Abdulwakati alisema kwamba sababu za kwenda mahakamani wenzao na kupokonywa ubingwa kumetokana na wenzao wa Miembeni kudai kwamba walimchezesha mchezaji Shaban Mussa ambae hakuwa halali,licha ya chama cha soka Tanzania (FAT) kuthibitisha mahakamani kuwa mchezaji huru.

Umahiri wake katika soka uliwashawishi wahusika wa juu kumuita kwenye timu kubwa mwaka 1984 na kushiriki katika michuano ya Chalenji iliofanyika mjini Mombasa nchini Kenya.

Milango ya kheri ikamfungukia siku chache baada ya kurudi kutoka Mombasa,ambapo mashushu wa Oman walikuwepo kusaka wachezaji wa kuwapeleka kwao.

Mwaka 1984 Abdulwakati alitua rasmin nchini Oman na kuanza kuwasuuza roho Waarabu  kwa ufundi wake wa kumiliki mpira na kupachika mabao.

Alisema mechi yake ya kwanza ilikuwa kati ya Oman na Qatar katika michuano ya ubingwa wa nchi za Ghuba akicheza kwa dakika 20 tu.

Aidha katika mechi ya kihistoria iliyochezwa Riyadh Saudi Arabia ikiwa ni michuano ya Gulf ushindi wa kwanza kwa Oman ulipatikana baada ya kurudi kambi nchini Brasil ambapo Abdulwakati alifanikiwa kuipatia timu yake goli moja na timu yake kuibuka na ushindi wa magoli 2-1.

Kutokana na kipigo hicho Qatar ilimkatika rufaa Abdulwakati kwa madai kwamba ni mgeni,lakini rufaa hiyo ilishindwa kwani nao pia walikuwa na wachezaji kutoka Somalia wawili.

Hata hivyo mchezaji huyo alikuwa halali kuchezea timu hiyo ya Oman kutokana na kufanyiwa taratibu zote za uraia.

Baada ya hapo akawa anapangwa mechi zote kwa dakika 90 na kuwashangaza matajiri wake kwa kipaji alichokuwa nacho.

Anakumbuka matokeo mazuri ni yale ya sare1-1 walipocheza na U.A.E ambao ni wapinzani wakubwa wa Oman sawa na timu za Kenya na Uganda.

Anafahamisha kwamba kila mwaka Oman ilikuwa ikishika mkia katika mashindano ya ‘Gulf Cup’ lakini katika mashindano hayo walishika nafasi ya nne kati ya nchi sita.

Pamoja na mafanikio makubwa aliyoyapata katika nchi ya Oman,mchezaji huyo anakumbuka kadhia iliyowakasirisha wachezaji baada ya kutwaa ubingwa wa Ghuba ambapo chama cha soka na Wizara husika kushindwa kutimiza ahadi zao kwamba wangewapa zawadi nono.

Akiwa na timu hiyo,mwanasoka huyo veteran alifanikiwa kwenda katika nchi zote za ghuba kushiriki michuano yao inayochezwa kwa zamu.

Katika kumbukumbu yake alifahamisha kuwa wakati wakijiandaa na mashindano ya Bahrainwalipiga kambi nchini Ufaransa na akabahatika kufundishwa na kocha Omar Boras raia wa Uruguay mwaka 1988 hadi 1990, ambae alikuwa kocha wa nchi yake katika mashindano ya kombe la dunia yaliofanyika Mexico mwaka 1986.

Baada ya kumaliza waliyotumwa kwa Oman kuwa mabingwa wa Ghuba zilizjitokeza baadhi ya timu kumtaka na hatimae alijiunga na klabu maarufu ya Fanja ilioko nchini Oman.

Wakati huo alisema alikuwa ni Mtanzania wa kwanza kujiunga na Fanja mwaka 1985,kabla ya kina Ahmed Amasha,Talib Hilal,Zahor Salim na Hilal Hemed.
Akiwa na timu hiyo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Oman mara nyingi sambamba na kombe la Sultan Qaboos kuanzia mwaka 1985 hadi 1992.

Aidha alisema mwaka 1987 alirudi Zanzibar kwa ajili ya mapumziko na kwenda na timu ya taifa nchini Ethiopia kwenye Chalenji ambapo walitoka sare na Kenya huku Tanzania Bara wakiifunga magoli 2-0  na kutoka sare na Ethiopia katika mechi ambayo mlinda mlango alikuwa Ali Bushiri ambae aliokoa kwa penalti.

Hata hivyo kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na makocha Gulam Abdallah na marehemu Mzee Kheri kilitolewa na Zimbabwe katika hatua ya nusu fainali.

Anaelezea kitendo cha muamuzi kuwabeba Wazimbabwe kilichangia kufungwa kwani walipokua nyuma kwa mabao 2-1, Inocent Haule alisawazisha lakini likakataliwa.

Abdulwakati ambae tangu akiwa kinda,alikuwa na lengo la kuchezea soka la kulipwa,anasema aliwahi kushawishiwa na viongozi wa Simba wakati huo akiwa na timu ya Taifa Stars lakini aligoma kwa vile hakuyaka kuihama Small Simba.

Kwa upande wa mechi ambayo anaikumbuka akiwa na klabu ya Small Simba,siku moja walikwaaana na Yanga katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambayo ilifanyika Mombasa Kenya.

Anasema Small Simba wakiwa nyuma kwa magoli 2-0  hadi mapumziko, ndani ya chumba cha kubadilisha nguo alimuomba kocha Abdulghani Msoma amtoe nahodha Fadhil Ramadhani.

Anasema kufuatia mabadiliko hayo wakaweza kurudisha bao moja na ikiwa zimebakia dakika 10,mchezaji mwezake aliemtambulisha kwa jina la Kirara ambae kwa sasa ni marehemu  alimzidi maarifa Juma Mkambi kasha akatulia na mpira akaja akamtoboa tena na kutoa pasi kwa Rashid Khamis aliepachika bao la pili.

Kwa upande wa mabeki ambao walikuwa wakimpa tabu wakati huo na timu zao kwenye mabano ni Hassan Wembe(Malindi), Abdallah Rajab(KMKM) na Said Ibrahim Njunju(Miembeni).\

Mwanandinga huyo alisema kwamba alikuwa akijisikia fahari sana akiona anacheza na kikosi kizima cha Small Simba lakini zaidi akiwa na Yussu Kassim na marehemu Kassim Kirara na mabeki Khamis Suleiman ‘Mpemba’ na Khalfan Ukasha.

Aidha Abdulwakati hakuacha kusifia umahiri wa mlinda mlango wa zamani wa wapinzani wao Black Fighters,Mwinjuma Makungu (marehemu) kwa ujasiri wake wa kuzuia michomo akiruka kwa staili ya kipekee.

Anasema kwamba kwa kiasi kikubwa soka limemsaidia kufika katika nchi mbali mbali kama Algeria, Misri,Zambia,Ufaransa,Brazil na nchi zote za falme za kiarabu Malaysia na Thailand.

Lakini mbali na kuwika katika mpira wa miguu,Abdulwakati alikuwa mahiri katika mchezo wa mpira wa meza (Table teniss) ambapo lifanikiwa kuchezea katika ya Taifa ya Tanzania na timu ya Taifa ya Zanzibar na kuwa mchezaji nambari moja nchi nzima.

Abdulwakati alihamisha kwamba mwaka 1974 aliiwakilisha Tanzania huko Alexandra Misri na kutolewa katika hatua za awali,ambapo mwaka 1977 alishiriki katika mashindano ya Tanzania Table Teniss kwa nafasi ya senior na bahati nzuri alichukua ubingwa wa mchezo huo kwa Tanzania nzima.

Abdulwakati aliweza kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Tanzania kwa miaka minne mfululizo katika michuano ya Coastal Town Champion Ship ambayo ilikuwa ikichezwa katika jiji la Dar es Salaam,Tanga na Mombasa katika kipindi cha Sikukuu za Pasaka.

Mwaka 1978 mwanamichezo huyo sambamba na wenzake walibeba bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Afrika (All African Games) nchini Algeria.

Katika mashindano hayo alitolewa na Nigeria katika robo fainali na kusema kwa kawaida  Wamisri na Wanigeria katika mchezo wa mpira wa meza.

Mwaka huo huo wa 1978,Abdulwakati aliungana na wenzake kutoka katika Mikoa ya Tanzania kushiriki katika mafunzo ya miezi sita kwa mchezo huo na kufundishwa na aliekuwa bingwa wa dunia,Liyanko Liyang.

Aliwataja wachezaji wenzake aliokuwa nao ni pamoja na Fatma Jidawi,Narman Jidawi,Shaaban Umiki,na Mohammed Salum wote kutoka Zanzibar ambapo kutoka Tanzania Bara ni Ahmed Diwani na Lucas Kiwango.

Alifafanua kwamba kikosi cha mpira wa meza Zanzibar kilikuwa kizuri kutokana na mafunzo waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa kocha wao Wu Li Yen ambae alikuwa Balozi mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China.

Hivi sasa Abdulwakati amekuwa akijumuika na wachezaji Veterani wengine hapa nchini kuunda timu ya Wazee Sports Club inayofanya mazoezi yake kwenye viwanja vya kila siku jioni.

Kuhusu utofauti wa soka la zamani na sasa,Abdulwakati alisema soka la zamani lilikua na tofauti kwani wachezaji wake walikuwa hawapati nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika nchi za Ulaya tofauti na sasa.

Aliongeza kwamba wachezaji wa zamani walikuwa wakicheza kwa ari na nguvu zote tofauti na ilivyo kwa wachezaji wa sasa kwani wamekuwa wanacheza kwa tamaa na fedha zaidi na sio moyo wa kuzipenda timu zao.

Mchezaji huyo mkongwe aliwashauri wachezaji hao kutopendelea kutumia vitu hivyo ambavyo havitoweza kuwajengea viwango vyao katika uchezaji wa soka.

Huyo ndie Abdulwakati aliezaliwa mwaka 1959 katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja na kuanza elimu ya msingi katika shule ya Darajani mwaka 1967 na baadae kumalizia masomo yake katika shule ya Vuga mwaka 1976.

Baadae wazazi wake walimpeleka Mkoani Morogoro kwa ajili ya kurejea masomo yake ya kidato cha tatu na cha nne katika Shule ya kilimo ya Ifakara.

Abdulwakati ni baba mwenye familia ya watoto wawili Nawwal na Nageeb,hivi sasa ni muajiriwa katika kampuni ya usafiri wa Anga Zanzibar (ZAT).





No comments:

Post a Comment