Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amehimiza umuhimu wa wanamichezo kuendelea kudumisha nidhamu michezoni ili
kulijengea sifa
Bora Taifa katika sekta hiyo kwa kuwa na wanamichezo walishiba
maadili na heshima iliyotukuka.
Balozi Seif Ali iddi alitoa himizo hilo wakati
alipokuwa akizungumza na wachezaji pamoja na Viongozi wa Timu ya Soka ya Taifa
ya Jang’ombe { Wakombozi wa Ng’ambno } katika hafla ya kukabidhiwa Kikombe cha
ubingwa baada ya Timu hiyo kupanda Daraja la kwanza Kanda mwaka huu.
Alisema nidhamu na heshima ndio kitu pekee
kilichosababisha wachezaji wa enzi zilizopita hapa Zanzibar kuwika na hatimae
kuiletea sifa Zanzibar katika ulimwengu wa kabumbu.
Balozi Seif alieleza kwamba Vijana wa sasa wana
nafasi pana ya kuendelea kujifunza mbinu mbali mbali za michezo na hatimae kuwa
mastaa ambazo hupatikana kupitia kwenye vipindi vya Televisheni pamoja na
mitandao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza
wachezji pamoja na Viongozi wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe kutokana na
kazi kubwa waliyoifanya na hatimae kuchukuwa ubingwa kwa kuingia daraja la
Kwanza Kanda.
Balozi Seif alisema juhudi za wachezaji hao kwa
upande mwengine zimeanza hatua mpya ya kujijengea uwezo wa kupata ajira kupitia
mchezo wa soka ambao unaonekana kupendwa sana Duniani.
“ Wapo wachezaji maarufu wanaochezea timu
zinazotajika Duniani katika ulimwengu wa kabumbu ambapo wengine wanatokea hata
mataifa ya Afrika yanayolingana kiwango cha soka na Tanzania “ Alisema Balozi
Seif.
Katika kuunga mkono wanamichezo hao wa Timu ya Soka
ya Taifa ya Jang’ombe Balozi Seif ameahidi kuisaidia Timu hiyo Seti mbili za
Jezi pamoja na Mipira Minne na akawataka wajiwekee malengo zaidi ya kufanikiwa
katika fani yao hiyo kwa siku zijazo.
“ Wale Jamaa wakikuoneni mnavyolisakata soka sawa
sawa kikweli watafikia hatua ya kukununueni tuu na kwa upande mwengine Zanzibar
tutakuwa na haki ya kujigamba kwamba tumetoa wachezaji wanaouwezo wa kuchezea
timu za Kimataifa “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala ya ujenzi wa Jengo la kudumu la
Timu hiyo ya Taifa ya Jang’ombne Balozi Seif aliwashauri Viongozi na wachezaji
hao kuanza ujenzi wa msingi na yeye atakuwa tayari kusaidia matofali kwa hatua
ya kunyanyua.
Alisema uwezo wa kujenga jengo lao uko mikononi
mwao ambapo viongozi wao jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kwamba wanasaidia
nguvu na maarifa ili kuona malengo waliyojipangia yanakwenda hatua baada ya
hatua.
Mapema Rais wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe
Salim Ridhiwani alisema Uongozi wa Klabu hiyo umeamuwa kuimarisha Timu hiyo ili
kurejesha heshima na hadhi ya klabu hiyo iliyopotea katika miaka ya hivi
karibuni.
Ridhiwani alisema Wanachama wa klabu hiyo
wanajivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya klabu hiyo hasa kutokana
na wachezaji wa timu hiyo kuiwezesha timu yao kuyakabili mashindano makubwa ya
Kombe la Mapinduzi na kutoa upinzani mkubwa kwa timu zenye uzoefu wa mashindano
ya soka Kimataifa.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mohammed Said
Dimwa alisema Uongozi wa Jimbo hilo umeifufua tena Timu hiyo ndani ya Kipindi cha
miaka Miwili iliyopita baada ya kufifia kutokana na changamoto kadhaa
zilizokuwa zikiikabili timu hiyo katika miaka ya nyuma.
Dimwa aliahidi kwamba yeye pamoja na viongozi
wenzake watasimama imara katika kuhakikisha Timu hiyo inarejea katika hadhi
yake iliyopewa na wapenzi wa timu hiyo ya kuitwa wakombozi wa Ng’ambo.
Timu ya Taifa ya Jang’ombe { Wakombozi wa Ng’ambo }
ilipanda Daraja na kushiriki mashindano ya Daraja la Kwanza Kanda mwaka huu
baada ya kuifunga Timu ya Soka ya Maungani Goli 1-0 katika mchezo wa Mwisho wa
mashindano ya Ligi Daraka la Pili.
No comments:
Post a Comment