Mwezi
wa Ramadhaan imeteremshwa Qur-aan
Jichumie
fadhila za kusoma na kuhifadhi Qur-aan
QUR-AAN ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) yaliyoletwa kama ‘Wahyi’
(Ufunuo) kwa Mjumbe wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume wa mwisho
Muhammad (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyoandikwa katika
Misahafu, yanayorithiwa na vizazi kwa vizazi, yaliyonukuliwa kwa mapokezi
mengi, kusoma kwake ni ibaada, ni yenye miujiza hata kama ni sura ndogo kabisa,
na ni uongofu kamili wa watu wote.
Kama asemavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala): ((Alif Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muangaza, kwa idhini ya Mola wao mlezi, uwafikishe kwenye njia ya mwenye nguvu, Msifiwa)) [Ibraahiym: 1]
MAJINA YA QUR-AAN
Maulamaa na Wafasiri wa Qur-aan wametaja majina
mengi ya Qur-aan kutokana na dalili katika Qur-aan yenyewe na pia Hadiythi
Sharifu. Yafuatayo ni baadhi tu ya majina hayo:
KITABU
((Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake;
ni uongofu kwa wachamungu)) [Al-Baqarah: 2]
AL-FURQAAN (Upambanuzi)
((Ametukuka aliyeteremsha Furqani kwa mja
wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote)) [Al-Furqaan: 1]
ADH-DHIKR (Ukumbusho)
((Na haya
ni makumbusho yaliyobarikiwa, tuliyoyateremsha. Basi je! Mnayakataa?) [Al-Anbiyaa: 50]
AN-NUUR (Mwangaza)
((Enyi
watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola wenu mlezi. Na tumekuteremshieni
nuru iliyo wazi)) [An-Nisaa: 174]
MAWAIDHA
((Enyi
watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha
yaliyomo vifuani, na uongofu, na rehema kwa Waumini)) [Yuunus: 57]
ALLAAH
(SUBHAANAHU WA TA’ALA) AMEIHIFADHI QUR-AAN
Bila ya
shaka Qur-aan ni kitabu kitukufu kabisa anachokihitajia kila mtu kumpatia
uongofu kamili awe katika njia iliyonyooka na awe katika Twa’a ya Mola Wake
Mtukufu. Naye Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) ametuhakikishia kuhifadhiwa na kuthibitika kwake ili isiongezeke au
kupungua hata neno au herufi moja ikaja ikawa hii Qur-aan imechanganyika na
maneno ya mtu bali, ibakie kuwa ni maneno Yake Pekee Mola wa viumbe vyote.
Amesema
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
((Hakika
Sisi ndio tulioteremsha ukumbusho huu, na hakika sisi ndio tutaokaoulinda))
[Al-Hijr: 9]
((Kwa
hakika wanayoyakataa mawaidha haya yanapowajia (wataangamia), na haya bila ya
shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu))
((Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma
yake. Kimeteremshwa na mwenye hikima, msifiwa)) [Fusswilat: 41-42]
KUTEREMSHWA QUR-AAN KATIKA RAMADHAAN
Anasema
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo
Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na
upambanuzi)) [Al-Baqarah: 184]
QUR-AAN IMETEREMSHWA KWA MITEREMSHO YA AINA
MBILI KAMA IFUATAVYO:
MTEREMSHO
WA MARA MOJA
Imeteremshwa Qur-aan kamili kutoka
‘Lawhu-m-Mahfuudh’ (Ubao uliohifadhiwa) mpaka mbingu ya kwanza. Kama
inavyothibitishwa na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
((Hakika Sisi tumeiteremsha Qur-aan katika
Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu)) [Al-Qadar: 1]
((Hakika tumekiteremsha katika usiku
uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji)) [Ad-Dukhaan: 3]
MTEREMSHO WA KIDOGOKIDOGO
Imeteremshwa kwa muda wa miaka 23 tokea kupewa
utume Mtume Muhammad (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hadi kufa kwake, nayo imeteremshwa kidogo
kidogo kutokana na hali na matukio yaliyokuwa yakitokea.
Aayah za mwanzo kuteremshwa ni Aya tano katika
Surat Al-’Alaq
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
((Soma kwa jina la Mola wako mlezi
aliyeumba))
((Amemuumba binaadamu kwa tone la damu))
((Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda
wote!))
((Ambaye amefundisha kwa kalamu))
((Kamfundisha mtu aliyokuwa hayajui))
[Al-’Alaq: 1-5]
Kutokana na rai zilizo za nguvu kabisa na
zilizowafikiana zaidi, kwamba Aya ya mwisho kuteremshwa ni,
((Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa
Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilichochuma. Nao hawatadhulumiwa))
[Al-Baqarah: 281]
VIPI ILIKUWA IKITEREMSHWA
QUR-AAN?
Kuteremeshwa Qur-aan katika kifua cha Mtume
(Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) ilikuwa ni kutokana na ‘Wahyi’
(ufunuo) kama ilivyothibiti katika Qur-aan yenyewe.
((Na
namna hivi tumekufunulia Qur-aan kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa Miji
na walio pembezoni mwake)) [Ash-Shuura:
7]
((Sisi
tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur-aan hii. Na ijapokuwa kabla ya
haya ulikuwa miongoni mwa wasiojua)) [Yuusuf: 3]
((Soma
uliyofunuliwa katika Kitabu)) [Al-’Anqabuut: 45]
KWA NINI IMETEREMSHWA KIDOGO KIDOGO NA SIO UTEREMSHO MMOJA KAMILI?
Makafiri
waliteta kuhusu Qur-aan kama ilivyo kawaida yao na ukaidi wao wa kukanusha kwa
kila aina ya vitimbi na usemi, wakasema:
((Na wakasema waliokufuru: Kwa nini
hakuteremshiwa Qur-aan kwa jumla moja?))
[Al-Furqaan: 32]
Wakikusudia kwa nini haikuteremshwa Qur-aan
kama vitabu vya nyuma navyo ni Tawraah, Injiyl, Zabuur na kadhalika ambavyo
viliteremshwa kwa jumla moja?
Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) akawajibu kwa
kuwapa Hikma yake ya kuiteremsha kidogo kidogo kwa muda wa miaka ishirini na
tatu kutokana na matukio na hali ilivyokuwa ikitokea, kuwa ili Qur-aan ithibitike katika moyo wa
Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Aya ilivyomalizikia
kusema.
((Na
wakasema waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur-aan kwa jumla moja? Hayo ni
hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu)) [Al-Furqaan:
32]
Vile vile
amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
((Na
Qur-aan tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na
tumeiteremsha kidogo kidogo)) [Al-Israa: 106]
Anasema
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala),
((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa
watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi)) [Al-Baqarah: 184]
Kwa hivyo
basi ndugu Waislamu tujitahidi kufanya
ibada hii adhimu tusome na kuhifadhi Qur-aan kwa wingi kabisa kwani
thawabu na fadhila zake ni nyingi na adhimu mno kama tunavyozinukuu humu. Pia
tujitahidi uweze kuhitimisha (kumaliza kuisoma) japo mara moja Qur-aan nzima
kabla ya mwezi wa Ramadhaan kwisha.
Zifautazo
ni fadhila mbalimbali za kusoma na kuhifadhi Qur-aan:
Anasema
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
((Wale tuliowapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo
kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini)) [Al-Baqarah:121]
KUFANYA BIASHARA NA ALLAAH YENYE FAIDA TELE NA
ISIYOANGUKA
Na Anasema
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
((Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi
Mungu, na wakasimamisha Swalah, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika
Tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyododa (isiyoanguka))) ((Ili Yeye
Awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila zake.
Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani)) [Faatwir: 29-30]
MTU
BORA KABISA NI MWENYE KUJIFUNZA NA KUIFUNDISHA
Imetoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allahu
‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Mbora wenu ni yule mwenye kujifunza
Qur-aan kisha akaifundisha)) [Al-Bukhariy]
THAWABU MARA MBILI KWA MWENYE KUISOMA KWA
MASHAKA
(Mwenye ulimi mzito au tabu ya kufahamu kwa
haraka, lakini inambidi Muislamu ajitahidi kujifunza kuisoma sawa sawa)
Imetoka kwa ‘Aisha (Radhiya Allahu ‘anha) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema, ((Yule
aliyekuwa hodari wa kusoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika Waandishi wa Allaah watukufu wacha Mungu, na
yule ambaye anaisoma Qur-aan kwa mashaka na huku anajitahidi kwa kudodosa atapata ujira mara mbili)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
WATU WA QUR-AAN NI WATU BORA KWA ALLAAH
(SUBHAANAHU WA TA’ALA)
Imetoka kwa Anas (RadhiyaAllaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema ((Allaah Anao watu Wake wa karibu katika watu)). Wakamuuliza, ewe Mjumbe wa Allaah, nani hao? Akasema: (( Hhao ni watu
walioiandama Qur-aan na ni watu
waliokuwa bora kabisa wa Allaah))
[Ahmad, na Ibn Maajah]
TOFAUTI YA ANAYEISOMA NA ASIYEISOMA QUR-AAN
Kutoka kwa Abu Musa Al-Ash’ariy (Radhiya Allahu
‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Mfano wa Muumini ambaye anayesoma
Qur-aan ni kama tunda la Utrujjah harufu yake nzuri na ladha yake nzuri. Na mfano wa Muumini asiyesoma Qur-aan mfano
wake kama tende zisizokuwa na harufu lakini zina ladha tamu)) [Al-Bukhaariy na
Muslim]
THAWABU KWA KILA HERUFI MOJA
Imetoka kwa ‘Abdullahi Bin Mas’uud (Radhiya
Allahu ‘anhu kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,
((Atakayesoma herufi moja katika kitabu cha Allaah atapata hasanah (jema) moja,
na kila hasanah moja ni sawa na thawabu kumi, wala sisemi ‘Alif-Laam-Miym’ ni
herufi moja, bali Alif ni herufi moja na Laam ni herufi moja na Miym ni herufi
moja)) At-Tirimidhiy
KIOMBEZI SIKU YA QIYAAMAH
Imetoka
kwa Abu Umaamah (Radhiya Allahu ‘anhu)
kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Someni Qur-aan kwani itakuja siku
ya Qiyaamah ikimuombea mwenye kuisoma))
Muslim
QUR-AAN HUMNYANYUA MTU NA HUMDHALILISHA
MWINGINE
Imetoka
kwa ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) ambaye amesema, Mtume wenu amesema ((Allaah Atawanyanyua baadhi ya watu kwa
kitabu hiki (Qur-aan) na Atawadhalilisha wengine kwa kitabu hiki)) [Muslim]
QUR-AAN HUMPANDISHA MTU DARAJA YA PEPO
Imetoka
kwa ‘Abdullah bin ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema
((Huambiwa rafiki wa Qur-aan (Aliyeiandama Qur-aan) soma na panda (juu katika
daraja za Pepo) na uisome kwa ‘Tartiyl’
(utaratibu na utungo) kama ulivyokuwa ukiisoma (kwa Tartiyl) ulipokuwa duniani,
kwani makazi yako ni pale utakapofika katika aya ya mwisho utakayoisoma))
[Sahiyh Al-Jaami’i]
MWENYE KUHIFADHI QUR-AAN HUTANGULIA KABURINI (KWA
AJILI YA MWANGA ANAOJAALIWA NAO)
Imetoka kwa Jaabir (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba alikuwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) akiwakusanya watu wawili waliokufa katika vita vya Uhud
katika nguo moja kisha anauliza, ((Nani katika hao mwenye Qur-aan zaidi? Anapojulishwa
mmoja kati ya hao, humtanguliza kaburini))
[Al-Bukhaariy]
KUTEREMKA MALAIKA KWA UTULIVU NA RAHMA KWA
WANAOSOMA QUR-AAN
Imetoka
kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu)
kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema
((Hawakusanyiki pamoja watu katika miongoni mwa nyumba za Allaah wakisoma
kitabu cha Allaah, na wanafundishana baina yao, ila huwateremkia utulivu na
hufunikwa na rahma na Malaika huwazunguka na Allaah Anawataja mbele ya aliokuwa
nao)) [Muslim]
KUHIFADHI NA KUJIFUNZA MAANA YAKE NI BORA
KULIKO MAPAMBO YA DUNIA
Imetoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhiya Allahu ‘anhu) ambaye amesema, Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) alitujia wakati tulikuwa
katika Suffah akauliza, kuna yeyote miongoni mwenu anayetaka kwenda soko la But-haan-Al-’Aqiyq na akapata humo
ngamia wawili (wa thamani kabisa wa kike) bila ya kutenda dhambi au kukata
undugu? Tukajibu kwamba sote tunapenda kufanya na kupata hivyo. Kisha akasema,
basi aende mmoja wenu msikitini akajifunze au asome aya mbili katika kitabu cha
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) basi akifanya hivyo ni bora kuliko ngamia (wa
thamani kabisa wa kike). Na aya tatu ni
bora kuliko ngamia watatu, na aya nne ni bora kuliko ngamia wanne, na mfano wa
hivyo hivyo wa aya kwa ngamia )) [Muslim]
MWENYE KUHIFADHI QUR-AAN HUVALISHWA TAJI
SIKU YA QIYAAMAH
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu
‘anhu) ambaye amesema, Mtume (Swalla
Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
amesema, ((Qur-aan itakuja siku ya Qiyaamah na itasema, Ewe Mola, Mpambe
(Mwenye kuhifadhi Qur-aan) kisha atavalishwa taji, kisha (Qu’raan) itasema Ewe
Mola, muongezee, kisha huyo mtu atavishwa nguo ya heshima, kisha itasema
(Qur-aan) Ewe Mola Ridhika naye, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ataridhika naye.
Kisha ataambiwa, soma na panda, atapokea thawabu zaidi za mema kwa kila aya
(atakayosoma) )) At-Tirmidhy na Al-Haakim na kaisahihisha Albaniy
Allaahumma Tujaalie Tuwe Wenye Kuandama
Qur-aan Ili Utulipe Fadhila hizi Ya Rabb.
No comments:
Post a Comment