Maalim Idriss ameacha misingi bora ya maisha ya dini ya kiislamu
ZANZIBAR ni moja ya nchi maarufu
ambayo iliyotoa walimu, masheikh na wanazuoni wengi ambao wameweza kuitangaza
nchi pamoja na kuwasomesha vijana wengi wa ndani na nje ya Zanzibar.
Kama utataja
majina ya masheikh hao ambao wamekuwa vinara wa kusomesha elimu hiyo ya dini,
basi huwezi kumaliza bila ya kumtaja Al-marhum Maalim Idriss.
Kufahamika
kwake huko hakutokani jambo lolote isipokuwa kazi yake ya ualimu ambapo
alifanikiwa kutoa taaluma ya dini ya kiislamu kwa vijana wengi. Miongoni mwao
hivi sasa ni masheikh wakubwa wa kutegemewa katika jamii yetu.
Kutokana
na kuwa ni mwanazuoni maarufu visiwani humu, Makala hii imefanikiwa kutafuta
historia yake alipoanzia katika maswala ya kidini, mpaka Mwenyezi Mungu
alipomuhitaji kiumbe wake.
Katika
kipindi kama hiki cha mwezi mtukufu wa
Ramadhan, marehemu alikuwa akisomoa hitma na utangulizi kabla ya kuanza kwa
darsa katika msikiti Gofu.
Jina
lake kamili ni Mohammed Idriss Mohammed Saleh Comorian, alizaliwa Septemba 17
mwaka 1934 akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto nane, wakiwem wanne
wanaume na wanne wanawake.
Kama
ilivyo kawaida ya watoto wengi wa dini ya kiislamu kuanza kusoma ilmu ya dini
wakiwa wadogo, nae marehemu Maalim Idriss alikuwa miongoni mwa vijana hao.
Wazazi
wa marehemu Maalim Idriss walimpeleka kujifunza ilmu ya Quraan katika chuo cha Maalim Syd Mohammed Alawi
Jamalily kilichopo katika mtaa wa Mchangani.
Mbali
na kusoma katika chuo hicho, lakini wazee wa marehemu hawakuwa nyuma katika
kumpa elimu zaidi ya dini, ambapo baada ya hapo pia walimpeleka kujifunza zaidi
elimu ya dini kwa masheikh mbali mbali.
Miongoni
mwa masheikh waliomsomesha Marehemu Maalim Idriss ni pamoja na marehemu Sheikh
Kamus katika msikiti wa Mbuyuni, Sud Alawi maarufu ‘Sharifu mrefu’, Sheikh
Abdallah Muadhini, Maalim Himid na masheikh mbali mbali ambao wote hao
wameshafika mbele ya haki.
Baada
ya hapo marehemu maalim Idriss alipelekwa skuli kwa ajili ya kujifunza elimu ya
dunia, elimu hiyo aliipata katika skuli mbali mbali ikiwemo Shimoni, Kengeja
Pemba na alimaliza elimu yake katika skuli ya Govt Boys Secondary School kwa
sasa inajulika kwa jina Ben bella.
Mnamo
mwaka 1950, Marehemu Maalim Idriss alijiunga na
masomo ya ualimu katika chuo cha
na mara baada ya kumaliza masomo hayo alianza kusomesha .
Marehemu
alisomesha katika skuli mbali mbali za mjini na mashamba ikiwemo skuli ya Dole,
ambapo baada ya miaka mingi ya kusomesha skuli maalim alistaafu kazi hiyo.
Mara
baada ya kustaafu kusomesha, Marehemu alikuwa akijishughulisha na kazi ya
kusomesha watoto wadogo elimu ya Quraan hapo katika mtaa wa Shangani katika
msikiti wa Mambo Msiige.
Aidha
kutokana na kazi hiyo ya kutoa elimu ya kitabu kitukufu kwa vijana wadogo,mwaka
1985 pia alikuwa Imamu wa msikiti huo huo wa Mambo msiige.
Lakini
kutokana na kuwa na kazi ya kusomesha vijana pamoja na Imamu, lakini marehemu
Maalim Idriss aliweza kuanzisha Jumuiya isiyokuwa ya Kiserikali (NGO) iliyokuwa
ikijulikana kwa jina la Islamic Madrass Relief Organisatio (IMRO).
Jumuiya
hiyo ambayo ilijikita zaidi katika kuvisaidia vyuo vya Quraan pamoja na
kuwasaidia watoto mayatima kazi ambayo alifanikiwa kuifanya katika uhai wake na
inaendelezwa mpaka hivi sasa.
Kutokana
na kuona umuhimu wa kuuendeleza uislamu, marehemu alifungua Maktaba
inayojulikana kwa jina la Islamic Museum hapo nyumbani kwake Shangani.
Kuanzishwa
kwa maktaba hiyo kuliweza kuwasaidia watu wengi wakiwemo wageni na wenyeji
waliokuwa wakifika katika maktaba hiyo kufaidika na kazi nzuri aliyoianzisha.
Katika maktaba hiyo ambayo iliweza kuweka
historia ya mambo mbali mbali ikiwemo ikiwemo historia ya Maulamaa mbali mbali
wa Afrika Mashariki, Comoro, Oman na Yemen.
Lakini
pia Marehemu alikuwa kiongozi wa Uradi wa Bausudani alishika nafasi hiyo hadi
kufariki kwake, ambapo uradi huu alikabidhiwa kuusoma katika Masjid jibril kila
siku ya Jumanne na Alhamis.
Marehemu
Maalim Idriss aliweza kushika nyadhifa mbali mbali katika maswala ya kidini na
hata katika vikundi mbali mbali na hata katika vikundi vya vijana wa Kiislamu.
Miongoni
mwa nyadhifa hizo ni pamoja na Mwenyekiti wa Mwinyi Baraka Foundation, Mlezi
katika chuo cha Madrasatul Munawar, mwanzilishi na Mwenyekiti wa bodi ya
wadhamini ya ZOP inayoendesha kambi 40 za matibabu Unguja na Pemba.
Aidha
makala hii ilibahatika kuzungumza na mmoja wa wanafunzi wake aliowasomesha na
kumlea katika maadili mema,Mohammed Omar Al sheikh (Juda).
Juda
alisema anamkumbuka marehem maalim Idriss kutokana na mambo mengi mema
aliyomfanyia ikiwemo kumlea katika maadili mema yenye misingi ya kidini .
Pia
alisema mbali na elimu hiyo, pia alimpeleka kwa marehemu maalim Kamus kupata
mambo mengi ya kidini.
“Namshukuru
sana na namkumbuka mrehemu maalim Idriss kwani amelea katika misingi mizuri ya
kidini na ambayo ndio yalioweza kunisaidia kufikia hapa nilipo”.
“Pia
marehemu ndie alienishika mkono mpaka msikiti wa Mbuyuni kwa marehemu Maalim
Kamus kupata elimu ya kidini ambayo ndio inanisaidia mpaka leo, namuomba
Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake,” aliongezea.
Lakini
mbali na Juda,pia nilipata nafasi ya kuzungumza na mwanafunzi wake Ally
Hamdan,nae alimsifia mwalimu wake kutokana na kumpa elimu iliyo bora ambayo
anaitumia.
“Kwa
marehemu maalim Idriss nimeweza kupata mambo mengi sana ikiwemo kujifunza elimu
ya quraan ambayo naitumia mpaka hivi sasa na mambo mbali mbali yanayohusu dini
ya kiislamu,” alifafanua.
Marehemu
Maalim Idriss atakumbukwa kwa mambo mengi sana ya kheri aliyoyafanya na bado yanaendelezwa mpaka hivi
sasa, ikiwemo kuhudhuria katika hadhara mbali mbali za kidini.
Pia
kushiriki katika hauli za wanazuoni,kwani alikuwa hodari wa kutoa historia za
maulamaa na kazi zao walizokuwa wakizifanya katika uhai wao.
Marehemu
Maalim Idriss alikuwa akipenda watu, hodari katika kuwaelimisha vijana
kujishughulisha na maswala ya kidini na hakuwa na ubaguzi kwa watu wa rika
tofauti
Maalim
Mohamed Idriss Mohamed Saleh amefariki akiwa na umri wa miaka 78 na maziko yake
yalifanyika nyumbani kwa ndugu yake Profesa Saleh huko Kilimani na kuhudhuriwa
na watu wengi sana wakiwemo masheikh, walimu na waumini wa dini ya kiislamu.
Mwenyezi
Mungu amlaze mahali pema peponi ameen.
No comments:
Post a Comment