Tuesday, 8 July 2014

MAKALA - HALED- MSOMI,MJASIRIAMALI ALIEJITUMBUKIZA KATIKA FANI YA SANAA YA FILAM



Na Aboud Mahmoud                                  
“Sanaa si uhuni sanaa ni kazi kama zilivyo kazi nyengine tena kwa nchi zilizoendelea kama Marekani wasanii ni kama tunu ya taifa thamani wanayopewa utaona hata kama wakija katika nchi zetu wana ushawishi mkubwa sana na watu,kwa hiyo heshima huanzia nyumbani,”.

Hayo sio maneno yangu bali ni maneno ya msanii chipukizi wa filamu ambae anaonekana kuwa na bidii na kuhakikisha kwamba anafika mbali kupitia sanaa ya uigizaji wa filamu nae sio mwengine bali ni Haled Tolbert,
Haled ni miongoni mwa wasanii chipukizi nchini Tanzania ambae ameonekana kuvuta hisia za mashabiki wengi wanaoangalia filamu mbali mbali zinazotoka nchini humu almaaruf kwa jina la ‘Bongo Movies’.
Kijana huyo ambae mbali na ya kuwa msanii wa filamu lakini pia mjasiriamali ambae ambae anafanya kazi za maswala ya teknolojia ya Computer (IT) pamoja na kuandika stori ambazo zinahusu jamii na hatimae nyengine kufanyiwa filamu.
Haled alibahatika kukutana na mwandishi wa makala hii na kumuelezea mambo mbali mbali katika fani yake ya filamu jinsi alipoanzia,alipofikia na matumaini yake ya hapo baadae.
Kijana huyo ambae ni mwembamba,mrefu,amezaliwa mwaka 1985  jijini Dar es Salaam katika hospitali ya Muhimbili akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto wane.
Elimu yake alianzia mnamo mwaka 1993 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba,ambapo mwaka 2000 hadi 2003 alipata elimu ya sekondari katika shule ya sekondari ya Azania.
Mwaka 2004alijiunga na masomo ya kidato cha tano na sita huko nchini Uganda katika shule ya St Charles Lwanga-Kasasa ambapo mara baada ya kumaliza alijiunga na masomo ya elimu ya juu (University) kufanya shahada ya kwanza ya utalii ‘Degree of Tourism’ ambapo aliweza kusimamisha masomo yake kutokana na sababu ambazo alisema hazikuwezi kuepukika.
Baada kutokea kwa sababu hizo zilizomfanya aachane na masomo,alikuja visiwani Zanzibar na kupata kazi katika hoteli ya Fairmont Hotel akiwa ni wakala Front Office.
Mwaka 2009 hoteli hiyo iliingua moto kubahatika kupata kazi katika hoteli nyengine ‘Kasha Boutique’ ambayo alisema ilikuwa ikimiliwa na mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar aliemtaja kwa jina la Shinuna Karume akiwa kama Meneja wa Mapokezi katika hoteli hiyo.
Msanii huyo alifanya kazi katika hoteli hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na baaade alirudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiunga na mafunzo ya Computer katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(U D).
Akiwa chuoni hapo alipata nafasi ya kusoma maswala ya Information Technology &Computing pia alijiunga na masomo kwa njia ya mtandao(Online) katika chuo cha Cisco Academy cha nchini Marekani kujifunza Sisco Networking.
Akiwa bado mwanafunzi,Haled alipata nafasi ya kuajirfiwa katika kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom akiwa wakala wa Customer Care ambapo alidumu na kampuni hiyo kwa muda wa miezi saba na baadae alipata kazi katika makampuni ya Quality Group ltd akiwa kama IT technician.
Baadae alirudi chuoni ambapo alijiunga na chuo kikuu huria(Open University of Tanzania) kuchukua Degree ya Human Resources management .
Katika maswala sanaa,Haled alisema kwamba sanaa kwake ni ubunifu ,hivyo baada ya kujifunza na kuona maisha mbali mbali yay a nchi za Afrika Mashariki na kuona masiha ya watu mbali mbali alijikuta anatumbukia katika fani ya sanaa ya uigizaji wa filamu.
Lakini pia alisema kwamba wapo wasanii ambao walionekana kumvutia katika maswala hayo ya uigizaji ndipo na yeye akajikuta anatumbukia katika fani hiyo,ambapo alimtaja msanii Bishanga ndie aliemvutia.
“Sanaa kwangu ni ubunifu baada ya kuona maisha ya watu wa Afrika Mashariki na kwengineko ndiko kulikonifanya niingie katika fani hiyo,lakini pia wasanii mbali mbali akiwemo Bishanga ndio walionivutia nikajikuta najiunga na sanaa hiyo,”alisema.
Aidha Haled alimtaja Isike Samuel  ndie aliemuibua na kumwambia kwamba anaweza kuigiza ambapo alisema kwamba Isike kwa sasa ndie meneja wake na anamuaminia katika kufanya kazi zote za uigizaji.
Kuhusu familia yake kushirikiana nae katika maswala ya Uingizaji,Haled alisema kwamba familia yake akiwemo mama yake na bibi yake ndio wanampa mashirikiano makubwa sana katika maswala ya sanaa ya filamu.
“Kusema kweli familia yangu akiwemo  mama yangu na bibi yangu wamekuwa wakinipa mashirikiano ya kutosha na kunihamasisha sana nifanye vitu vyenye ubunifu,”alifahamisha.
Filamu yake ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Misuko’ ambapo katika filamu hiyo Haled aliigiza kama mwalimu wa shule ambapo filamu hiyo ilishirikisha wasanii mahiri akiwemo Haji Adam,Rose Ndauka na wengine wengi.
Mbali na filamu hiyo,Haled amesema kwamba zipo filamu nyengine ameigiza ikiwemo ‘Tulizana’ ambayo imetoka mwanzoni mwa wiki hii pamoja na ‘Nesi feki’inayotarajiwa kutoka hivi karibuni ambapo alisema filamu hizo zote zimewashirikisha wasanii wengi maarufu na kufanya kazi yake kwa kujiamini.
Kuhusu matatizo,Haled alisema kwamba matatizo ambayo anakumbana nayo katika kazi yake ya uigizajini kukosa mashirikiano ya kutosha kutoka kwa wasanii wenye majina makubwa hususana wakati wanapotaka kurekodi filamu.
“Matatizo niliyoyaona mpaka saivi ni kukosa mashirikiano kwa wasanii wenye majina makubwa na zaidi wakati tukitaka kurekodi filamu ndo inazidi tatizo hilo,lakini matatizo mengi kwangu nayaona ni ya kawaida ambayo naweza kuyakabili mwenyewe,”alisema.
Katika maswala ya faida,msanii huyo alieleza kwamba faida yake kubwa ni kupata exposure kwa wasanii ambao tayari ameshafanya nao kazi,pamoja na kupata fans wengi sana.
Kuhusu mategemeo yake ya baadae msanii huyo alisema kwamba ni kuifanya sanaa ya uigizaji kuwa ni ajira yake rasmin,poa anategemea kukua kitaifa na kimataifa duniani kote.
“Mategemeo yangu mengine kuhakikisha kwamba vijana wanadumisha na kuiwelesha zaidi jamii kuhusiana na mambo mbali mbali yanayofanyika katika kupitia filamu,”.
Alifahamisha kwamba katika fani yake ya uigizaji huwa anapenda kusoma kupitia wasanii mbali mbali wa ndani nan je ya nchi jinsi wanavyoigiza ili na yeye awe msanii mzuri zaidi.
Haled alitoa ushauri kwa wasanii wenzake wachana kuongeza juhudi zaidi kwani sanaa ni ubunifu hivyo aliwaeleza kwamba siku hizi ukiwa mjuzi utakuwa mtendaji kila mtu atapenda kazi zao.
Aidha msanii huyu aliwashauri wasanii wakubwa kutumia ukubwa wao katika kuboresha mapungufu yote yaliopo katika tasnia hii kwa kuongea na vyombo husika .
Alisema kufanya hivyo kutaweza kuwasaidia wasanii wasanii wadogo na hata katika maisha ya tasnia hiyo kwa ujumla.
“Naishauri Serikali iwe sikivu katika kilio cha wasanii kwani wasanii wamekuwa wanachangia sana katika pato la taifa pia wasanii wamesaidia sana kupatikana  ajira kwa vijana pamoja sanaa hiyo kuelimisha jamii na kupata nchi yenye raia mwema,”alifafanua.
Haled mbali ya kuwa muigizaji lakini pia ni mwandishi wa story  mbali mbali zinazotengenezewa filamu ambapo alieleza kwamba ameshaandika hadithi nyingi sana na kuuza kwa wasanii mbali mbali.
Alisema miongoni mwa hadithi hizo  alizoandika ni ‘Msamaha wa Rais’ ambayo alisema ni hadithi ya kusisimua na tayari ameipeleka katika Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi(ZIFF) kwa ajili ya mashindano mwaka huu.

Mbali na sanaa ya uigizaji,lakini Haled pia ni mjasiriamali ambae ni mtaalamu wa mambo ya Information Technology (IT) ambae anafanya kazi zote za Computer.

No comments:

Post a Comment