Na Haroub Hussein
Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel leo imetoa msaada wa
vyakula kwa ajili ya mwezi wa Ramadhani kwa makundi maalumu ya wazee hapa
visiwani Zanzibar.
Msaada
huo unajumuisha sukari, unga wa ngano pamoja na mchele umetolewa katika hafla
fupi ya makabidhiano iliyofanyika leo.
Kampuni
ya Zantel upande wa Zanzibar imeainisha wazee zaidi ya 120 wenye uhitaji wa
vyakula kwenye mwezi huu wa Ramadhani walio chini ya jumuiya ya wazee hapa
Zanzibar.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano hayo kwa wazee, Mkurugenzi wa Biashara wa
Zantel-Zanzibar, bwana Mohammed Mussa, amesema ni kawaida kwa kampuni ya Zantel
kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii katika kipindi hiki cha Ramadhani.
'Tuna
furaha sana leo kuweza kusaidia jamii hii ya wazee ambao mara nyingi wamekuwa
wanasahaulika, kwani tunaamini wazee ni sehemu muhimu sana ya jamii ndio maana
Zantel leo tumeamua kutoa msaada huu ambao unatutofautisha sana na makampuni
mengine katika vipaumbele vyetu' alisema Mussa.
Mussa
aliongeza kuwa kama kampuni ya simu inayoongoza Zanzibar, Zantel mara zote
imekuwa mfano katika shughuli zake za kijamii na vipaumbele vyake kiujumla.
Akizungumza
wakati wa shughuli hiyo, mgeni rasmi ndugu Msham Abdallah, ambaye ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar, alisema anaipongeza Zantel
kwa kushirikiana na serikali kuyasaidia makundi ya wazee.
‘Serikali
imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali katika kulisaidia kundi hili la wazee,
kwahiyo ni furaha kwetu leo kuona Zantel imekuwa ya kwanza kusaidia kundi hili
leo’ alisema bwana Abdallah.
Akitoa
neno la shukrani kwa kampuni ya Zantel, naibu mwenyekiti wa jumuiya ya wazee
Zanzibar, Bwana Mwadini Kutenga, alisema anawashukuru Zantel kwa msaada huo,
akisema umekuja kwa wakati mufaka hasa ukizingatia kuwa wanakaribia kuadhimisha
sikukuu ya Idi.
'Kwa
misaada hii, Zantel inawafanya wazee nao wajiskie sehemu ya jamii, kwani mara
nyingi wamekuwa wakisahaulika sana na kwa hakika hatutawasau kwa ukarimu wao
huu' alisema bwana Kutenga.
Kampuni
ya Zantel imekuwa msitari wa mbele katika kusaidia makundi mbalimbali ya
kijamii kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani, na msaada huu ni maalumu kwa kundi
la wazee ambalo mara nyingi linasahaulika katika jamii.
Jumuiya
ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na lengo la
kuwaunganisha na kuwasaidia wazee Zanzibar na sasa ina wanachama zaidi ya 1000.
No comments:
Post a Comment