Friday, 4 September 2015

MOHAMMED AHMED:GWIJI WA MUZIKI WA TAARAB TANZANIA


“MAPENZI yangu pokea,kwa moyo wa ukunjufu
Wewe nnakulete,usiwe mbabaifu
Kama utayagomea,nitakujua dhaifu”.
Hio ni moja kati ya beti ya wimbo maarufu wa taarab asilia unaojulikana kwa jina la ‘Mapenzi yangu pokea’ulioghaniwa na mutrib mashuhuri na mkongwe ambae ameshastaafu,Maalim Mohammed Ahmed Mohammed.


Bila shaka jina hilo sio geni miongoni mwa wapenzi wa muziki wa taarab asilia wa Zanzibar na hata nje ya visiwa hivi vya marashi ya karafuu.
Licha ya kuwa Mohammed Ahmed ameimba miaka mingi iliyopita,lakini nyimbo zake bado ni dhahabu masikioni mwa wengi kila wanapozisikiliza zikipigwa katika vituo vya  redio au katika rekodi za cd.

Sifa za nguli huyu wa utunzi wa mashairi ya taarab na uimbaji,zilimshawishi mwandishi wa makala haya kumtafuta ili kufanya mahojiano naye,kwa dhamira ya kufahamu tarikh yake katika fani hiyo na siri ya mafanikio yake.

Akisimulia Maalim Mohammed Ahmed alisema fani hiyo hakurithi kutoka kwa mtu yoyote katika familia yake,bali yeye mwenyewe aliipenda pamoja nay eye mwenyewe kuvutwa na ushawishi kutoka kwa wenzake.

Alieleza kuwa mnamo mwaka 1961,ndipo alipojitumbukiza rasmin katika fani ya taarab kwa kujiunga na kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa chenye maskani yake katika mtaa wa Kokoni Malindi.

Huko alikutana na wasanii wengi akiwemo marehemu MaalimIddi Abdallah Farahan,Marehem Maalim Seif Salim,Maalim Abdallah Suleiman na wengine wengi.
Mara baada ya kujitosa kwenye klabu hiyo yenye historia ndefu katika bahari ya muziki wa taarab Afrika Mashariki,msanii huyo amesema alianza kwa kuimba wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Wanaodharau mapenzi yafaa tuwaapize’ wimbo ambao hapo awali uliimbwa na mwimbaji mwengine kundini humo.

Baadae alisema akaanza kuimba wimbo ‘Adam na Hawa’ uliotungwa na Marehem Saleh Ajmi ambao alisema hata hivyo wimbo huo haukupata umaarufu kwani uliimbwa mara moja.
Baada ya takriban miaka miwili nyimbo za kukopia na zilizotungwa na watunzi wengine,Maalim Mohammed Ahmed alisema mwaka 1963 alianza kutunga na wimbo wake wa kwanza ulikuwa ni ‘Mapenzi yangu pokea’ ambao mpaka sasa bado unapendwa.
Kuanzia hapo kasi yake ya utunzi ikapamba moto ambapo zipo nyimbo alizotunga na kuimba mwenyewe na nyengine zikaimbwa na wasanii wengine katika kundi lake hilo.

Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘Ua’  ulioimba na Almarhum Maalim Seif Salim ‘Kisebusebu’,Almarhum Bakari Abeid ‘Kibiriti na Petroli’ Maalim Seif Salim,pamoja na ‘Sasa sinae’ulioghaniwa na Almarhum Khamis Shehe.\

Mnamo mwaka 1964 wakati vikundi vyote vya Unguja vilipoungana na kuunda kikundi kimoja cha Mila na Utamaduni,Mutrib huyu alikuwa miongoni mwa wasanii waliojumuika kuanzisha kikundi hicho ingawa baadae aliondoka na kwenda masomoni.
Lakini baada ya kurudi kutoka masomoni,alieleza kuwa uongozi wa klabu ya Culture ulimuomba ajiunge nao na kumpa wadhifa wa Ukatibu,ingawa halikumzuia kuendelea na Nadi Ikhwan Safaa.
Wakati nikizungumza na gwiji huyu alinambia ametunga nyimbo nyingi sana,lakini nyengine amezisahau .
Hata hivyo,aliutaja mmoja wa wimbo alioutunga ambao aliupa jina la ‘Kunguru’ ambapo alinambia aliutunga na kuuimba yeye mwenyewe.
Baadhi ya maneno yaliokuwemo katika wimbo huo ni kama yafuatayo:
Kunguru ndege laghai,Anatabu kumnasa
Kama yeye hatokei,Mwenye hila na mikasa
Japo ukifanya rai,Weka mbele kumkosa.

Aidha Maalim Mohammed Ahmed alibainisha kuwa,hata klabu ya Culture yenye maskani yake mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar,aliitungua nyimbo kadhaa zikiwemo ‘Pesa’ ambao uliimbwa na msanii mkongwe Nihfadhi Abdullah, ‘Kukupenda sana ‘Rukia Ramadhan’  Sikujua kama mapenzi matamu nao ulighaniwa na bibie Mtumwa Mbarouk
Wimbo wa sikujua kama mapenzi matamu ulikuwa ukisema kama hivi:
“Ni hakika sikujua kwamba, Mapenzi matamu
Si dhihaka nakwambia,Yatanitia wazimu
Hivi sasa natambua,Kwamba yamenilazimu
Kila nikiliridhia,Inazidi yangu hamu.


Mbali na wimbo huo pia alitunga wimbo Pendo letu lishasibu  ambao uliimbwa na mkongwe mwengine na mwalimu katika jukwaa la sanaa za maigizo na tarab asilia Marehemu Bakari Abeid Ali.
Muziki wa taarab umeweza kumfikisha mkongwe huyo katika nchi mbali mbali duniani.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Kenya,Visiwa vya Comoro,Dubai na Abudhabi,Oman,Hispania,Ubelgiji,Ufaransa,Uholanzi,Italia,Denmark,Uswisi,Finland,Visiwa vya Reuniuon na nyenginezo.
Pia ametembela Mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara ambapo alikwenda kutumbuiza na klabu zake kwa vipindi tofauti.
Nilipomuliza anifafanulie tofauti anazoziona baina ya taarab asilia na ile inayoitwa ya kisasa,Maalim huyo kitaaluma,kwa sasa hakuna watunzi wa maana bali waliopo ni watu wanaotafuta maslahi pekee bila ya kuzingatia maadili na mambo muhimu katika utunzi wa nyimbo za taarab.

Alifahamisha kwamba wakati yeye anajiunga na taarab,ilikuwa lazima mtu alipie shilingi kumi na baadae kila mwezi shilingi tatu kinyume na miaka hii ambapo msanii anajiunga katika kikundi kwa matarajio ya kulipwa kabla hajaanza kutoa mchango wowote kukiinua kikundi anachojiunga nacho.

“Kuna tofauti kubwa kati yetu wasanii wa zamani na hawa wasanii wa sasa,sisi tulikujwa hatulipwi bali tukilipia ada ya klabu,mimi mwenyewe  wakati najiunga nililipa shilingi kumi na kila mwezi wanachama sote tulikuwa tunalipa,leo wasanii wanalipwa wao” alisema.

Kuhusu tofauti ya kimuziki,Maalim alisema hakuna kitu kinachoitwa modern taarab,bali hiyo ni aina ya ngoma iliyoingia mjini na kwa kuwa kiingiacho mjini si haramu  basi mambo yanakwenda tu kama yanavyoonekana.

“Taarab lazima ipigwe kwa kutumia ala za asili kama vile qanoon,oud,fidla na nyenginezo,lakini leo mtu unaweza kuwa na keyboard  yako ukapiga taarab,mimi sijawahi kuona kama wenzetu Tanga wanaita kumbwaya na Mombasa wanaita Chakacha basi  na hapa kwetu Unguja watafute jina lakini sio taarab,”alifafanua.

Nilitaka pia kujua ni wasanii gani wanaomvutia katika kazi zao,naye bila ya kigugumizi akawataja baadhi ya wasanii akiwemo Marehemu Rashid Sultan,Marehemu Bakari Abeid,Marehemu Seif Salim,Ali Soud na Marehemu Maulid Mohammed Machaprala.

Hata hivyo,kwa maneno yake,alieleza kuwa miongoni mwa wanawe hakuna anayeweza kusema kwa uhakika kama anafuata nyayo zake za usanii,ingawa alimtaja mmoja wa watoto wake aitwae Harusi kuwa anaonekana kujaribu kutaka kujiingiza katika tasnia hiyo..

Nilipomtaka atoe maoni juu ya dhana ya baadhi ya watu kuwa muziki ni uhuni,Maalim Mohammed alikuwa na fikra nyengine tofauti na kusema kuwa uhuni ni tabia ya mtu kwani wapo wahuni wanaojulikana sana katika jamii lakini kamwe hawafanyi kazi ya muziki wala usanii wa aina yoyote.

“Hizi ni dhana potofu muziki ni kazi kama kazi nyengine zinazoweza kumjengea mtu heshima na kutambulika kitaifa na kimataifa,pia muziki umetumika katika kusaidia mambo mbali mbali kwani una nguvu ya kuhamasisha.

Na zaidi mbona mimi sijawa muhuni,Umkulthum,Abdelhalim Hafidh na wengine wengin hawajakuwa wahuni,”alitoa mfano.

Juu ya siku hizi kutokuwepo kwa watunzi wengi wa masihairi ya taarab,msanii huyo alisema hiyo inasababishwa na muziki kugeuzwa biashara ,ambapo alisema watunzi wa sasa wanataka kulipwa na walipaji hakuna .

Akitoa mfano wa klabu za Malindi na Culture ambazo alisema zinashindwa kutoa nyimbo mpya kutokana na kushindwa kulipia.

Mbali na fani ya muziki,lakini msanii huyo aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali Serikalini baada ya awali kuwa mwalimu mkuu katika skuli tofauti ikiwemo Langoni, Wilaya ya Magharibi mwaka 1971,Ole(1972) Kisiwandui(1974) na baadae mwalimu mkuu skuli ya Sekondari Shangani mjini Unguja.

Aidha aliwahi kuwa Afisa wa Mambo ya Kale,Mkurugenzi Mipango Wizara ya mila na Utamaduni,Katibu Muhtasi Ikulu Zanzibar,Katibu Muhtasi wa Rais Ali Hassan Mwinyi Zanzibar,na Baadae Katibu Mkuu Afisi ya Rais.

Nafasi hiyo ya Katibu Mkuu alianzia kipindi cha Rais Marehemu Idrissa Abdulwakil na kuendelea mpaka wakati wa Rais Dr Salmin Amour Juma alipomaliza muda wake nae akafikia muda wa kustaafu.

Kupitia makala hii Maalim Mohammed Ahmed amewashauri wasanii wasikimbilie kuimba tu bali wajifunze kwanza apamoja na kutafuta ujuzi wa kupia ala mbali mbali za muziki wa taarab.

Alitoa mfano wa kikundi cha taarab asilia kinachoundwa na wanawake watupu cha Tausi ambacho kinawafundisha wasanii wake kuimba pamoja na upigaji wa ala.

Pia aliwaasa wasanii kuacha tabia ya kupikiana majungu na fitina katika vikundi ili kuepusha kuvunjika kwa vikundi hivyo.

Msanii huyo aliyebaki kuwa miongoni mwa mifano ya kuigwa alizaliwa mwaka 1940 katika mtaa wa Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja akiwa motto wa kwanza katika familia ya watoto watano wawili wakiume na watatu wakike.

Alianza kupata elimu ya msingi mwaka 1946 katika skuli ya ambayo wakati huo ikiitwa Mnazi Mmoja kuanzia darasa la kwanza hadi la pili ambapo skuli hiyo hivi sasa imekuwa kituo cha American Corner.

Baadae alihamia skuli ya Gulioni huko alisoma mpaka darasa la sita na kuhamia Kiembesamaki kwa masomo ya darasa la saba na la nane kabla ya kujiunga na ‘Junior Secondary School’ ambayo kwa sasa ni Benbella kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu.

Mnamo mwaka 1961 alijiunga na Chuo cha Ualimu na kuanza kusomesha mwaka 1962.

Ilipofika mwaka 1976 alijiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ngazi ya ‘Bachelor of Education’ na kumaliza mwaka 1979.
Mwaka 1983 alikwenda nchini Uholanzi kuendelea na masomo yay a digrii ya juu (Masters).

Gwiji huyo ameoa na amejaaliwa kupata watoto na pamoja na kustaafu taarab,amesema hupata wasaa wa kujikumbusha kuimba hususan katika shughuli maaalum ikiwemo harusi za familia yake

  

No comments:

Post a Comment