Wednesday, 17 July 2019

DAR ES SALAAM:JIJI LENYE HISTORIA KUBWA

DAR ES SALAAM ni  jiji lenye harakati kubwa, watu wengiwanaozunguka huku na kule takriban saa 24 ingawa wingi wao umekua ukitafautiana baina ya eneo na eneo.
Upo pia utamaduni wa aina yake kulikochangiwa na mchanganyiko mkubwa wa makabila tofauti yaishio hapo, upo pia msongamano mkubwa wa magari takriban katika barabara zote za jiji hilo.





Ni jiji pia lenye harakati kubwa za kibiashara za aina mbali mbali kama  vile vyakula, vinywaji, na mahitaaji mengine mbali mbali ya lazima na hata yale ya anasa.
Aidha ni jiji lenye idadi kubwa ya wakaazi  kuliko sehemu yoyote ya Tanzania na pia zipo harakati nyingi zaidi za Kiserikali kuliko Mkoa mwengine wa Tanzania ingawa hivi sasa harakati hizo zimeanza kuhamia katika mji mkuu wa katika Mkoa wa Dodoma.
Ni jiji la Dar es Salaam lenye wastani wa karibu kilomita za mraba zinazozidi kidogo 85, ambapo zamani ulikua ukifahamika kama ni mji wa kinanani kutokana na majina yake, ilikua ni rahisi sana kutambua wenyeji wa mji ule ambao uko kando kando ya bahari ya hindi.
Majina ya akina Shomvi,Rehani,Janja,Mwinyikambi,Mwinjuma,Kishiwa na Ubaya lakini kwa uchache tu yalikua yanakukaribisha Bandari Salama au ukipenda Mzizima ikimaanisha ukarimu, upole na pia ukarimu wa watu hulka zao kwa enzi hizo.
Majina ya vijiji nayo pia yalikua sawa na wanajamii wenyewe wa hapo kwa mfano Gezaulole,Mbwamaji,Magogoni,Kigamboni,Bunju,Vianzi,Mjimwema,na Mussa Hassan maarufu kwa sasa Msasani.
Kibugumo na Kariakoo ni miongoni mwa majina majina haya yalikua yakimtambulisha mgeni kuwa yupo kwa watu gani kwenye mji huo ambao asili kubwa ya wakaazi wake  ni kabila la kizaramo kwa wakati huo.
Hivi sasa Dar es Salaam ikiwa na mchanganyiko wa kila aina ya watu ni vigumu sana kuweza kuwatambua wenyeji wa sehemu hiyo wako wapi na ni akina nani, lakini unaweza kuchukua siku mbili au wiki kuweza kusikia majina kama hayo ya asili niliyoyaainisha kwa kuyataja awali.



Kata utakutana na kijana aliezaliwa baada ya uhuru wa Disemba 9 mwaka 1961 na baadae Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ukamuuliza unajua nini kuhusu Mzizima na Bandarisalama?.
Jibu utakalolipata hapa hapa ni kuwa pengine ataweza kukuelezea kuwa Mzizima ni moja ya skuli ya Sekondari iliyopo jijini hapo katika mtaa wa Upanga ambayo ni maarufu sana.
Wenyeji wa mkoa huo wanaifahamu Dar es Salaam kwa majina makubwa mawili kwanza wengine watakueleza Bandarisalama au kwa jina la Mzizima.
Dar es Salaam ukipenda Mzizima ni miongoni mwa miji ya zamani katika mwambao wa bandari ya hindi ambao ustawi wake ulianza kupamba moto katika miaka ya 1857.
Historia yake inakwenda mbali zaidi kiasi cha miaka 1000 pale jamii ya kabila ya Barawa wakiwa na kabila ya wazaramo walipoanza shughuli za kilimo katika mji huo ambao leo hata nafasi ya kupanda mgomba unaitafuta.
Dar es Salaam au Mzizima ni mji ambao uliendelezwa kutoka mwaka 1866 wakati Sultan Sayyid bin Majid bin Sultan wa Zanzibar ambae pia eneo la mwambao wa pwani alikua akitawala kutoka maili 200 kutoka usawa wa bahari,Sultan huyo ndie alietoa jina la Dar es Salaam “Heaven of Peace”.
Geza ulole ni neon lenye asili ya Kizaramo ambalo lina  maana ya ‘Jaribu uone’ ambapo kwwa vijana wa sasa sio wengi sana ambao wanafahamu maana ya neon hilo .
Wengi wao wanaweza kukwambia ule wimbo wa Gezaulole, mama geza ulole mama ee, biashara ya njugu na korosho haikufai kaka wee twendezetu Kibugumo na Mwanalidadu tukaanzishe makao mapya.
Dar es Salaam ni kama miji mengine ya pwani,haikuwa salama na biashara ya utumwa vijijini kama Kimbiji na Mjimwema vilikaliwa sana na waarabu kutoka Oman  ambao wakati huo walikua wakijishughulisha na biashara ua utumwa na nyenginezo.
Wenyeji wa Mkoa huo ni Wazaramo na Wandengereko ambapo baada ya shughuli za kilimo na uvuvi na kazi nyenginezo walikua wakipenda sana kukaa barazani,ambapo baraza zao zilikua zikijengwa kwa udongo na nyumba zake zikijengwa kwa makuti.
Watu wake walikua wakiishi kijamaa mkaazi wa Msasani au Kariakoo na Magogoni pengine hata Mjimwema waliweza kutambuana majina na nyumba wanazoishi wenzao.
Ngoma za asili zilikua zikipigwa katika mitaa mbali mbali ya mji huo ambapo sasa ni maeneo machache yaliobaki ukakuta watu wakicheza ngoma katika shughuli zao.
Kwa hakika Dar es Salaama ilikua ikifika Ijumaa akina mama walikua na heka heka kubwa kwa upande wa shughuli,hapo akina baba wakibakia nyumbani na watoto, wanawake wanampeleka mwari mkoleni kwenda kupatiwa mafunzo maalum kabla ya kwenda kwa mumewe.
Shughuli kama hizo zilikua zikianza siku ya Ijumaa zikiendelea hadi siku ya Jumamosi ambayo ni siku ya mbiga na siku ya Jumapili mwari anatoka na kuekwa uwanjani akiwa njiani kuelekea kwa mumewe.
Hapo tena mdundiko, gombesugu,mkinda na segere ikianza kutumbuiza kuanzia siku ya Ijumaa jioni.
Hivi sasa ni nadra sana kusikia gombesugu ikipigwa na badala yake utasikia majina mengine ya kisasa ambayo ni tofauti sana na ngoma za asili.
Hivi sasa ngoma ya segere inapigwa kwa kutumia  kinanda na piano ambavyo ni tofauti na ilivyokua ikipigwa hapo awali, siku ya mkole hivi sasa inaitwa Kitchen Party ambapo tofauti na mila na dwwsturi zilizotumiwa na wazee wa huko.
Tukirudi nyuma Dar es Salaam ilikua  imo katika mipango mizuri iliokua imepangwa na Sultan Majid ambapo mipango yake hiyo ilikuja kuharibiwa na Wajerumani.
Wajerumani hao waliingia hapo na utamaduni wao na mambo yao jambo ambalo liliwachukiza sana wazalendo ama wenyeji wa mji huo ambapo kwa kushirikiana na Abushiri ambaye alikua mwarabu walianzisha mapambano dhidi ya Wajerumani.
Hata hivyo kutokana na upungufu wao walizidiwa nguvu na Abushiri pamoja  na wafuasi wake walinyongwa na Wajerumani.
Ikulu ya Magogoni ni moja ya majengo ya kihistoria ambalo liliachwa na wakoloni,ukumbi wa Karimjee ni jengo la Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na makanisa yaliopo pembezoni mwa ukingo wa bahari ni majengo machache kwa mfikaji wa jijini Dar es Salaam atayaona mwanzo.
Hivi sasa shughuli za bandari hiyo zimetanuka na kufanywa za kisasa zaidi kuliko ilivyokua awali kwani vifaa vya kazi vinavyotumika sasa wakati huo ilikua ni ndoto kuonekana.
Kwa ujumla Bandari Salama imekua ni tegemeo kubwa la juhudi za kiuchumi hapa Tanzania kutokana na harakati za kibiashara na pia usafiri wa abiria ndani nan je ya Tanzania.
Kutokana na kukua kwa Dar es  Salaam yenyewe na kuwepo mchanganyiko mkubwa wa wenyeji na wageni na pia harakati zaidi za kijamii hata utamaduni wa wenyeji nao umeanza kubadilika kwa kiasi fulani kwani wao kama  sehemu ya jamii mara nyengine  wanalazimika kufuata mchanganyiko huo uliopo tofauti na ilivokua miaka kadhaa iliyopita.






No comments:

Post a Comment