“INALILAHI
wa Ina Ilayhi Rajiuun yaani hakika sisi ni waja wa Mwenyezi Mungu na sisi kwake
tutarejea,”hiyo ni kauli ambayo kila muumini wa dini ya Kiislamu anaifahamu kwa
kuwa ina maana ya kukumbuka kila kilichoumwa na Allah (SW) basi hakina budi
kurejea kwake kwa maana ya kufa.
Kwa kila
muislamu akiisikia kauli hii huwa anafahamu kwamba ameletwa duniani kwa ajili
ya kumuabudu Allah (SW) basi iko siku atarudi kwake.
Naweza
kuinasibisha kauli hii kwa Al marhum Sheikh Mohammed Majid ambae ni mmoja wa
maulamaa wa dini ya kiislamu waliokuwepo hapa Zanzibar katika kuitangaza dini
ya Mwenyezi Mungu(Uislamu).
Marehemu
Sheikh Mohammed Majid ni miongoni mwa wanazuoni maarufu wenye maarifa makubwa
ya dini ya kiislamu waliotangulia mbele ya haki ambao walikuwepo Zanzibar
katika kuitangaza dini ya Mwenyezi mungu.
Sheikh Majid
atakumbukwa maisha kutokana na uwezo wake na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi
Mungu katika kulingania dini ya Kiislamu na kuisambaza kupitia njia tofauti ili
iwafikie wale waliokusudiwa.
Marehemu
Mohammed Majid alizaliwa Juni 5 mwaka 1956 katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa
Kaskazini Unguja,ambapo elimu yake ya awali alianza kuipata kisiwani Pemba
kijiji cha Mchakaeni.
Marehemu
Sheikh Mohammed Majid alikuwa akiishi kisiwani humo kutokana na baba yake
kuhamia kwa shughuli za uvuvi akitokea kijijini kwao Matemwe.
Mwaka 1965
marehemu alihamia kisiwani Zanzibar na kuanza elimu yake ya Maahad Islamia
ambayo kwa sasa inajulikana kama Chuo cha Kiislamu Mazizini ambapo kwa wakati
huo ilikuwa ni elimu ya sekondari.
Mara baada
ya kumaliza elimu ya sekondari Sheikh huyo alikwenda nchini Sudan mwaka 1984
katika chuo kikuu cha kimataifa cha Afrika kuchukua elimu ya dini ya kiislamu
pamoja na lugha ya kiarabu .
Baadae
alikwenda nchini Saudi Arabia kuchukuwa shahada ya kwanza ya dini ya Kiislamu
na Kiarabu.
Mwaka
1992,Marehemu alirudi Sudan kuchukua shahada ya Uzamili yaani ‘Masters Degree’
ya lugha ya Kiarabu na dini ya Kiislamu na mara baada ya kumaliza elimu hiyo
alirudini nyumbani Zanzikbar.
Marehemu
Sheikh Mohammed Majid hakuwa nyuma katika maswala ya kutafuta elimu ya dini nay
a dunia kutokana na kwamba alikuwa akijua umuhimu wa elimu.
Alikaa
Zanzibar kwa muda mfupi na baadae alirudi nchini Sudan kuchukuwa elimu ya
udaktari wa Falsafa “PHD” ya dini ya Kiislamu pamoja na lugha ya Kiarabu.
Elimu
alizozipata nchi mbali mbali na aliyoipata hapa nchini kupitia walimu
waliomsomesha dini aliweza kuongeza dini kipaji chake na kuwa na hamu kubwa ya
kuitangaza dini ya kiislamu.
Marehemu Dr
Mohammed Majid baada ya kumaliza elimu hiyo na kurudi nyumbani alisomesha lugha
ya Kiarabu katika kituo cha Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ambacho kwa
sasa ni Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).
Pia marehemu
Dk Mohammed Majid ni miongoni mwa
waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Kiislamu Chukwani na pia aliwahi kuwa
msaidizi Mwalimu Mkuu Madrassat Noor mpaka mwaka 2000 baada ya kufariki
marehemu Maalim Bakathir.
Marehemu
Sheikh Mohammed Majid alitawazwa rasmin kuwa mwalimu mkuu wa Madrassa hiyo
iliyopo katika mtaa wa Ukutani mjini Unguja.
Mnamo mwaka
2002 sawa na mwaka 1423,Marehemu Sheikh Mohammed Majid alifariki dunia na
kuzikwa kijijini kwao Matemwe Mnazimmoja Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dk Mohammed
Majid atakumbukwa maisha na waislamu wote wa hapa visiwani Unguja na Pemba kwa
ujumla kwa kuwa na changamoto kubwa ya kuanzisha kipindi cha Jiongezee Maarifa kinachorushwa
na Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC).
Kipindi
hicho kimeweza kuvutia vijana wengi kutaka kuifahamu na kusoma zaidi mwenendo
wa dini yao ya kiislamu pamoja na kitabu kitukufu cha Quraan.
Baadhi ya
masheikh waliokuwepo hapa Zanzibar wanamzungumzia kwamba marehemu huyo
atakumbukwa sana katika kipindi chake hicho cha Jiongezee Maarifa ambacho
hupendwa na waislamu wengi kwa kuwafanya vijana wengi kuwa na hamu ya kuijua
dini yao.
“Marehemu
Sheikh Mohammed tunamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoyafanya wakati alipokuwa
yuhai kwa kuanzisha kipindi cha Jiongezee maarufa ambacho kimewaongoa vijana
wengi wa Kiislamu na kufanya kipindi
hicho kikauwa mpaka kufikia kisiwani Pemba.
Katika
kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,Marehemu Sheikh Mohammed Majid
alikuwa akisomesha somo la Fiqhi na Quraan katika msikiti wa Jongeani na
msikiti wa Mchangani yote ya mjini Unguja.
Marehemu
ameweza kujijengea jina lake kwa kuweza kuitangaza dini ya Kiislamu kupitia
Nyanja mbali mbali kwa vijana na watu wazima ili kuzidi kukuwa kwa jamii ya
Kiislamu kwa kufuata maadili mema ya dini yao.
Aidha
Marehemu atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri mbali ya kulingania dini ya Kiislamu,lakini
pia mapenzi yake kwa watu wote wa rika tofauti,ucheshi na pia hakuwa mtu mwenye
majivuno.
Marehemu
aliacha wake watatu na watoto 11,wanawake 10 na mwanamme mmoja.
Kwa niaba ya
makala haya na mafundisho yake mema ya
hapa duniani kwa ajili ya Akhera, Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amlaze
mahali pema peponi Aamin.
No comments:
Post a Comment