ZANZIBAR ni
moja ya nchi ambazo zimejaaliwa kuwa na vipaji vya aina mbali mbali,vikiwemo
vya utunzi,ufinyanzi na hata katika maswala ya michezo,ambayo kwa kiasi fulani
ilitamba katika michezo ya aina tofauti.
Miongoni mwa
watu waliotamba visiwani humu katika mchezo wa soka na mpira wa mezani Abdullah
Juma Aley almaaruf Abdulwakati ambae aliweza kuitikisa Zanzibar nan chi
nyengine duniani michezo hiyo.
Kama utataja
majina ya watu waliowahi kutamba visiwani humu katika mchezo wa mpira wa meza
na soka bila ya kumtaja Abdulwakati itakuwa hukumaliza idadi yao.
Abdullah
Juma Aley ndio jina lake alilopewa na wazazi wake,lakini hata hivyo jina hilo
linafahamika kwa watu waliokuwa sio wengi kwani ukipita katika mitaa mingi ya
visiwani humu ikiwemo Kikwajuni na kumtaja jina la Abdullah hutompata mpaka
utaje Abdulwakati.
Jina hilo
ndio limekuwa maaarufu kuliko jina lake halisi kwa kipindi chote alichocheza
michezo hiyo Zanzibar,Tanzania,Afrika Mashariki na hata Arabuni .
Mwandishi wa
makala haya alimtafuta mwanamichezo huyo huko nyumbani kwake Michenzani na
kuzungumza nae kwa kina katika mambo mbali mbali yanayomuhusu yeye kimichezo.
Alisema
kwamba umaarufu wa jina la Abdulwakati hautokani na kitu chochote isipokuwa ni
mchezo wa soka ambao ulimpatia umaarufu mwaka 1980 na kuendelea.
Alisema
kwamba jina la Abdulwakati alilipata wakati alipokuwa mdogo akichezea timu ya
hero Boys ambapo alisema jina hilo alibatizwa na mwalimu wake wa soka Abubakar
Soni.
“Katika timu
yetu kulikujwa na wachezaji watatu na wote walikiuwa na majina ya Abdul ,hivyo
kutotufautisha sisi akaamua mimi kuniita Abdulwakati kwa vile nilikuwa nachezea nafasi ya
mshambuliaji wa kati,”alisema.
Mchezaji
huyo mkongwe ambae kwa kawaida ni mcheshi,alisema wachezaji wenzake walibatizwa
majina mengine kama vile Abdul Kikono na Abdul Kifupi.
Katika
maisha yake ya soka,alianza kung’ara mapema utotoni mpaka kupewa mikoba ya
unahodha kwenye timu ya shule visiwani Zanzibar.
Aliendelea
kucheza timu ya watoto kabla ya kujiunga na klabu ya Everton iliyokuwa na
maskani yake katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja mnamo mwaka 1970.
Kutokana na
uwezo wake mkubwa wa kusakata kabumbu Abdulwakati alichukuliwa na timu
iliyokuwa ikimilikiwa na kituo cha kulelea watoto cha Forodhan iliokuwa
ikijulikana kwa jina la Karume Boys na kutembea nayo katika mikoa mbali mbali
ya Tanzania.
Timu hiyo
ambayo ilikuwa chini ya uangalizi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehem Mzee
Abeid Aman Karume ambapo timu hiyo ilikuja kugawanyika mara baada ya kifo cha kiongozi
huyo mwaka 1972.
Akiwa katika
kikosi hicho cha Karume Boys alikutana na wachezaji wengi akiwemo Sihaba
Saadat,Omar Willium na wengine wengi.
Mnamo mwaka
1972 baada ya kusambaratika kwa Karume Boys,Abdulwakati alijiunga na kikosi cha
Small Simba baada ya kushawishiwa kufanya hivyo na kocha wa zamani wa kikosi
hicho ,Masoud Salim almaarud Maoud Kocha.
Kutokana na
ari,jitihada na moyo wake wa kusakata kabumbu wakati anapokuwa uwanjani,veteran
huyo alichaguliwa kujiunga na timu ya Taifa ya vijana ya Zanzibar mwaka huo huo
1972.
Akiwa na
Small Simba,Abdulwakati alikuwa kivutio kikubwa sawa na wachezaji wote wa timu
hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa baada ya kupanda daraja,ambapo ilianza kwa
moto mkubwa na kutikisa vigogo vya soka nchini.
Alisema timu
yao ilikuwa imesheheni vipaji na kuwa gumzo la mji na kuanza kujitwalia ubingwa
wa soka visiwani mwaka mwaka huo huo waliopanda ngazi 1983.
Chini ya
nyota mahiri akiwemo wakati,Small Simba iliweza kutamba vilivyo katika miaka
1985 hadi 1987.
“Kuanzia mwaka
1983 hapo moto wetu ulikuwa hauzimiki na mashabiki wetu wakapata wimbo wa ‘Moto
Small’ambapo kila tulipokuwa tunashuka dimbani au watu walipokuwa wakizungumzia
timu yetu waliimba Moto Small,alisema mwanandinga huyo.
Jambo ambalo
nyota huyo atabaki akilikumbuka maishani kwake ni tukio la mwaka 1987 kwa timu
ya Small Simba kupokonywa ubingwa na Miembeni ambao walikwenda mahakamani.
Anasema
anafahamu kwanini walishindwa kesi hiyo na kila mmoja alijua kutokana na hakimu
wa kesi hiyo alikuwa Miembeni damu,hivyo alisema haki haikutendeka.
Abdulwakati
alisema kwamba sababu za kwenda mahakamani wenzao na kupokonywa ubingwa
kumetokana na wenzao wa Miembeni kudai kwamba walimchezesha mchezaji Shaban
Mussa ambae hakuwa halali,licha ya chama cha soka Tanzania (FAT) kuthibitisha
mahakamani kuwa mchezaji huru.
Umahiri wake
katika soka uliwashawishi wahusika wa juu kumuita kwenye timu kubwa mwaka 1984
na kushiriki katika michuano ya Chalenji iliofanyika mjini Mombasa nchini
Kenya.
Milango ya
kheri ikamfungukia siku chache baada ya kurudi kutoka Mombasa,ambapo mashushu
wa Oman walikuwepo kusaka wachezaji wa kuwapeleka kwao.
Mwaka 1984
Abdulwakati alitua rasmin nchini Oman na kuanza kuwasuuza roho Waarabu kwa ufundi wake wa kumiliki mpira na
kupachika mabao.
Alisema
mechi yake ya kwanza ilikuwa kati ya Oman na Qatar katika michuano ya ubingwa
wa nchi za Ghuba akicheza kwa dakika 20 tu.
Aidha katika
mechi ya kihistoria iliyochezwa Riyadh Saudi Arabia ikiwa ni michuano ya Gulf
ushindi wa kwanza kwa Oman ulipatikana baada ya kurudi kambi nchini Brasil ambapo
Abdulwakati alifanikiwa kuipatia timu yake goli moja na timu yake kuibuka na
ushindi wa magoli 2-1.
Kutokana na
kipigo hicho Qatar ilimkatika rufaa Abdulwakati kwa madai kwamba ni
mgeni,lakini rufaa hiyo ilishindwa kwani nao pia walikuwa na wachezaji kutoka
Somalia wawili.
Hata hivyo
mchezaji huyo alikuwa halali kuchezea timu hiyo ya Oman kutokana na kufanyiwa
taratibu zote za uraia.
Baada ya
hapo akawa anapangwa mechi zote kwa dakika 90 na kuwashangaza matajiri wake kwa
kipaji alichokuwa nacho.
Anakumbuka
matokeo mazuri ni yale ya sare1-1 walipocheza na U.A.E ambao ni wapinzani
wakubwa wa Oman sawa na timu za Kenya na Uganda.
Anafahamisha
kwamba kila mwaka Oman ilikuwa ikishika mkia katika mashindano ya ‘Gulf Cup’
lakini katika mashindano hayo walishika nafasi ya nne kati ya nchi sita.
Pamoja na
mafanikio makubwa aliyoyapata katika nchi ya Oman,mchezaji huyo anakumbuka
kadhia iliyowakasirisha wachezaji baada ya kutwaa ubingwa wa Ghuba ambapo chama
cha soka na Wizara husika kushindwa kutimiza ahadi zao kwamba wangewapa zawadi
nono.
Akiwa na
timu hiyo,mwanasoka huyo veteran alifanikiwa kwenda katika nchi zote za ghuba
kushiriki michuano yao inayochezwa kwa zamu.
Katika
kumbukumbu yake alifahamisha kuwa wakati wakijiandaa na mashindano ya
Bahrainwalipiga kambi nchini Ufaransa na akabahatika kufundishwa na kocha Omar
Boras raia wa Uruguay mwaka 1988 hadi 1990, ambae alikuwa kocha wa nchi yake
katika mashindano ya kombe la dunia yaliofanyika Mexico mwaka 1986.
Baada ya
kumaliza waliyotumwa kwa Oman kuwa mabingwa wa Ghuba zilizjitokeza baadhi ya
timu kumtaka na hatimae alijiunga na klabu maarufu ya Fanja ilioko nchini Oman.
Wakati huo
alisema alikuwa ni Mtanzania wa kwanza kujiunga na Fanja mwaka 1985,kabla ya
kina Ahmed Amasha,Talib Hilal,Zahor Salim na Hilal Hemed.
Akiwa na
timu hiyo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Oman mara nyingi sambamba na kombe la
Sultan Qaboos kuanzia mwaka 1985 hadi 1992.
Aidha
alisema mwaka 1987 alirudi Zanzibar kwa ajili ya mapumziko na kwenda na timu ya
taifa nchini Ethiopia kwenye Chalenji ambapo walitoka sare na Kenya huku
Tanzania Bara wakiifunga magoli 2-0 na
kutoka sare na Ethiopia katika mechi ambayo mlinda mlango alikuwa Ali Bushiri
ambae aliokoa kwa penalti.
Hata hivyo
kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na makocha Gulam Abdallah na marehemu Mzee
Kheri kilitolewa na Zimbabwe katika hatua ya nusu fainali.
Anaelezea
kitendo cha muamuzi kuwabeba Wazimbabwe kilichangia kufungwa kwani walipokua
nyuma kwa mabao 2-1, Inocent Haule alisawazisha lakini likakataliwa.
Abdulwakati
ambae tangu akiwa kinda,alikuwa na lengo la kuchezea soka la kulipwa,anasema
aliwahi kushawishiwa na viongozi wa Simba wakati huo akiwa na timu ya Taifa
Stars lakini aligoma kwa vile hakuyaka kuihama Small Simba.
Kwa upande
wa mechi ambayo anaikumbuka akiwa na klabu ya Small Simba,siku moja walikwaaana
na Yanga katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
ambayo ilifanyika Mombasa Kenya.
Anasema
Small Simba wakiwa nyuma kwa magoli 2-0
hadi mapumziko, ndani ya chumba cha kubadilisha nguo alimuomba kocha
Abdulghani Msoma amtoe nahodha Fadhil Ramadhani.
Anasema
kufuatia mabadiliko hayo wakaweza kurudisha bao moja na ikiwa zimebakia dakika
10,mchezaji mwezake aliemtambulisha kwa jina la Kirara ambae kwa sasa ni
marehemu alimzidi maarifa Juma Mkambi
kasha akatulia na mpira akaja akamtoboa tena na kutoa pasi kwa Rashid Khamis
aliepachika bao la pili.
Kwa upande
wa mabeki ambao walikuwa wakimpa tabu wakati huo na timu zao kwenye mabano ni Hassan
Wembe(Malindi), Abdallah Rajab(KMKM) na Said Ibrahim Njunju(Miembeni).\
Mwanandinga
huyo alisema kwamba alikuwa akijisikia fahari sana akiona anacheza na kikosi
kizima cha Small Simba lakini zaidi akiwa na Yussu Kassim na marehemu Kassim
Kirara na mabeki Khamis Suleiman ‘Mpemba’ na Khalfan Ukasha.
Aidha
Abdulwakati hakuacha kusifia umahiri wa mlinda mlango wa zamani wa wapinzani
wao Black Fighters,Mwinjuma Makungu (marehemu) kwa ujasiri wake wa kuzuia
michomo akiruka kwa staili ya kipekee.
Anasema
kwamba kwa kiasi kikubwa soka limemsaidia kufika katika nchi mbali mbali kama
Algeria, Misri,Zambia,Ufaransa,Brazil na nchi zote za falme za kiarabu Malaysia
na Thailand.
Lakini mbali
na kuwika katika mpira wa miguu,Abdulwakati alikuwa mahiri katika mchezo wa
mpira wa meza (Table teniss) ambapo lifanikiwa kuchezea katika ya Taifa ya
Tanzania na timu ya Taifa ya Zanzibar na kuwa mchezaji nambari moja nchi nzima.
Abdulwakati
alihamisha kwamba mwaka 1974 aliiwakilisha Tanzania huko Alexandra Misri na
kutolewa katika hatua za awali,ambapo mwaka 1977 alishiriki katika mashindano
ya Tanzania Table Teniss kwa nafasi ya senior na bahati nzuri alichukua ubingwa
wa mchezo huo kwa Tanzania nzima.
Abdulwakati
aliweza kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Tanzania kwa miaka minne mfululizo
katika michuano ya Coastal Town Champion Ship ambayo ilikuwa ikichezwa katika
jiji la Dar es Salaam,Tanga na Mombasa katika kipindi cha Sikukuu za Pasaka.
Mwaka 1978
mwanamichezo huyo sambamba na wenzake walibeba bendera ya Tanzania kwenye
michuano ya Afrika (All African Games) nchini Algeria.
Katika
mashindano hayo alitolewa na Nigeria katika robo fainali na kusema kwa
kawaida Wamisri na Wanigeria katika
mchezo wa mpira wa meza.
Mwaka huo
huo wa 1978,Abdulwakati aliungana na wenzake kutoka katika Mikoa ya Tanzania
kushiriki katika mafunzo ya miezi sita kwa mchezo huo na kufundishwa na
aliekuwa bingwa wa dunia,Liyanko Liyang.
Aliwataja
wachezaji wenzake aliokuwa nao ni pamoja na Fatma Jidawi,Narman Jidawi,Shaaban
Umiki,na Mohammed Salum wote kutoka Zanzibar ambapo kutoka Tanzania Bara ni
Ahmed Diwani na Lucas Kiwango.
Alifafanua
kwamba kikosi cha mpira wa meza Zanzibar kilikuwa kizuri kutokana na mafunzo
waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa kocha wao Wu Li Yen ambae alikuwa Balozi mdogo
wa Jamuhuri ya Watu wa China.
Hivi sasa
Abdulwakati amekuwa akijumuika na wachezaji Veterani wengine hapa nchini kuunda
timu ya Wazee Sports Club inayofanya mazoezi yake kwenye viwanja vya kila siku
jioni.
Kuhusu
utofauti wa soka la zamani na sasa,Abdulwakati alisema soka la zamani lilikua
na tofauti kwani wachezaji wake walikuwa hawapati nafasi ya kucheza soka la
kulipwa katika nchi za Ulaya tofauti na sasa.
Aliongeza
kwamba wachezaji wa zamani walikuwa wakicheza kwa ari na nguvu zote tofauti na
ilivyo kwa wachezaji wa sasa kwani wamekuwa wanacheza kwa tamaa na fedha zaidi
na sio moyo wa kuzipenda timu zao.
Mchezaji
huyo mkongwe aliwashauri wachezaji hao kutopendelea kutumia vitu hivyo ambavyo
havitoweza kuwajengea viwango vyao katika uchezaji wa soka.
Huyo ndie
Abdulwakati aliezaliwa mwaka 1959 katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja na
kuanza elimu ya msingi katika shule ya Darajani mwaka 1967 na baadae kumalizia
masomo yake katika shule ya Vuga mwaka 1976.
Baadae
wazazi wake walimpeleka Mkoani Morogoro kwa ajili ya kurejea masomo yake ya
kidato cha tatu na cha nne katika Shule ya kilimo ya Ifakara.
Abdulwakati
ni baba mwenye familia ya watoto wawili Nawwal na Nageeb,hivi sasa ni muajiriwa
katika kampuni ya usafiri wa Anga Zanzibar (ZAT).