“NIKIWA hai
nataka kushuhudia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,ambao ambao unafuata misingi yote
ya demokrasia zaidi kwa vyombo vya habari,”.
Hiyo ni
miongoni mwa kauli alizowahi kuzitoa katika uhai wake Marehemu Profesa Haroub
Othman kwenye moja ya semina ya uzinduzi wa kitabu hapa visiwani Zanzibar.
Tarehe kama
ya leo mwaka 2009,Tanzania iliingiwa na simanzi kubwa baada ya kuondokewa na
mpiganaji na mtetezi wa haki za wanyonge Marehemu Professa Haroub Miraji
Othman.
Ilikuwa ni
vigumu kuamini lakini ni kweli wakati ulifika,Mwenyezi Mungu (SW) alimwita nae
akaitika kutokana na wito ambao mwanadaamu yoyote hana budi kuuitika.
Siku
iliyofuata ya Juni 29 mwaka 2009
Watanzania walio wengi na hasa wasomi wa nchi hii waliungana na familia
ya marehemu katika mazishi yake yaliofanyika nyumbani kwao Baraste na kuzikwa
katika makaburi yaliopo katika kijiji cha Chuwini.
Kuondoka
katika dunia hii kwa kipenzi cha wengi ilikua ni vigumu kuaminika kutokana na
kuwepo kwake karibu na wanajamii pamoja na kazi yake ya kutetea haki na maslahi
ya wanyonge.
Ni ukweli
usiofichika kwamba marehemu Profesa Haroub ni nguzo kuu iliyo katika ghafla
katika ujenzi wa demokrasia,haki,amani na utengamano Zanzibar,Tanzania,Afrika
na dunia kwa ujumla.
Marehemu
Profesa Haroub atakumbukwa daima kutokana na michango yake mingi ikiwemo
kuhubiri haja ya kuwepo kwa mabadiliko na kuwa mwanaharakati mahiri wa sharia
na haki za binaadamu na utawala bora.
Pia
atakumbukwa kwa mengi mazuri hasa katika mchango wake kwa jamii akiwa ni
mpiganaji wa haki za binaadamu pamoja na alikuwa anapenda kusema ukweli.
Nanukuu ile
kauli ambayo nakumbuka aliitoa katika siku ya kumkumbuka aliyekuwa Mkurugenzi
wa Idara ya Umoja wa Walemavu marehemu Maalim Khalfan Hemed Khalfan.
Marehemu
Profesa Haroub alisema ‘Kama utakuwa humkumbuki mwenzako ambae ameshafika mbele
ya haki,basin a wewe uhakikishe kwamba hutokumbukwa,”.
Kutokana na
kauli hiyo ambayo imenivutia sana na kujaza hamasa ya kuandika makala hii,na
kwa umuhimu aliokuwa nao marehemu katika nchi yetu hatuna budi sote Watanzania
tumkumbuke.
Kwa mujibu
wa kitabu maaraufu cha ‘Haroub Othman Farewell to the Chairman ‘kilichotungwa
takriban miaka sita iliyopita mara baada ya kifo chake kutokea.
Wanasiasa,viongozi,wanasheria,
wanahabari pamoja na wanafunzi wake waliweza kutoa maoni yao kutokana na
umuhimu aliokuwa nao kwa nchi yake Marehemu.
Hii
inaonesha wazi kuwa ni pengo kubwa sana ambalo ni gumu kuzibika kwa kipindi kifupi
kutokana na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu na kuwa na umuhimu katika
jamii nzima na sio kifamilia pekee.
Kitabu hicho
kimemnukuu Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda
alivyomueleza Profesa Haroub kuwa mtaalamu aliyebobea katika mitaala ya
maendeleo nani mwanaharakati wa haki za
binaadamu ambae anafahamika ndani nan je ya nchi.
Waziri mkuu huyo ambae alisema marehemu
alikuwa mwalimu wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970 pia
alimuelezea kuwa ni mtu ambae ndani na nje ya chuo hakuwa mchoyo wa kutoa elimu
yake na wala ushauri wa kitaalamu.
Kutokana na
kauli ya Waziri Mkuu wetu wa Tanzania kuwa marehemu alitumia vyema sana vipaji
alivyokuwa navyo na karama alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu bila ya majivuno,woga wa
wivu.
Nae
mwanahabari wa siku nyingi Salim Said Salim alimuelezea marehemu Profesa Haroub kuwa ni mwanaharakati asiye na shaka
na aliyetukuka nan i mtu wa kupigiwa mfano.
Pia
alimuelezea kwamba aliweza kumfunza mambo mengi sana pamoja na kumuonesha njia
ambayo anaamini kuwa ni sahihi katika maisha yake ya kila siku.
Umuhimu wa
marehemu Profesa Haroub haukuonekana kwa mwanahabari Salim Said Salim,bali kwa
wanahabari wengi sana miongoni mwao ni mwanahabari Haura Shamte .
Haura
alimuelezea marehemu kuwa ni alama ya fikra pevu,mahiri na yenye busara pamoja
na wadhifa aliokuwa nao na heshima kubwa katika jamii ya Watanzania.
Haura
alimsifia marehemu kuwa pamoja na usomi aliokuwa nao,lakini hakujitenga na watu
wa kawaida na alishiriki katika shughuli mbali mbali alizoarifiwa.
“Marehemu
aliamini kwamba watu wote ni sawa
hakujikweza wala hakutakabari,binafsi Profesa alikuwa chanzo changu cha
habari kila nilipotingwa na jambo hasa
katika masuala ya kisiasa,”alisema Haura.
Kwa upande
wa kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) hawakuwa nyuma kutoa sifa njema
za Marehemu Profesa kutokana na umuhimu wake katika kituo hicho akiwa akiwa
mmoja wa waanzilishi wa kituo hicho.
Aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho Iss-haq Ismail Shariff,alieleza kwamba ukweli
usiofichika kuwa marehemu aliitaka Zanzibar wanaondokana na shida za kutafuta
haki zao za msingi katika wakati mgumu walihitaji.
“Profesa
Haroub atakumbukwa kwa dhamira yake njema ya kutaka kuwa Wazanzibari wana uwelewa katika masuala yote ya sheria,haki za
binaadamu na maendeleo,”alisema Mkurugenzi huyo.
Mbali na
wasomi lakini kwa upande wa familia yake,haukuwa nyuma kutoa maoni au wasifu
mzuri wa marehemu ndugu yao ambapo ndugu yake Othman Miraji Othman alimuelezea
kwa kina kaka yake.
Kitabu kimefafanua
kuwa Miraj alisema,Marehemu Profesa Haroub alikuwa nguzo ya familia ya ukoo wao
na haikutetereka hadi mwisho wa maisha yake.
Alisema
jambo lolote litakalomfikia ndugu yake au rafiki yake likiwa la furaha au
msiba,marehemu ingawa alikuwa anaishi Dar es Salaam,lakini alikuwa nahudhuria
katika shughuli hiyo.
Aidha ndugu
huyo alimuelezea kaka yake kuwa alikuwa akiipenda sana Zanzibar na ndio sehemu
aliyokuwa akiipendelea sana kuvutia
pumzi yake ya mwisho kuliko sehemu nyengine.
Mmoja wa
watu waliotoa ujumbe kwa njia ya mashairi ni Jenerali Ulimwengu ambae alisema
katika mashairi yake .
Haroub kenda
harudi,Ndiyo yetu sote sudi
Kifo kwetu
sote budi,Ahadi ikiwadia
Ela tuko
kulia,Mataka kujishikia
Haroub alo
azizi,katimiza yake kazi
Bila kufanya
ajizi,Sote tumemridhia.
Hizi ni
baadhi ya beti za utenzi uliotungwa na Jenerali Ulimwengu kwa ajili ya marehemu
Brofesa Haroub Othman .
Hakuna jambo
lisilokuwa muhimu kwa wananchi wa Tanzania kukumbuka mchango wa marehemu
Profesa Haroub katika taaluma yake ikiwemo kufundisha taaluma ya maendeleo na
mambo ya sheria kwa muda wa miaka 41.
Pia alitoa
elimu katika maeneo makubwa ya ufundishaji ikiwemo haki za binaadamu,Ujenzi wa
Demokrasia na utawala bora,historian a falsafa ya siasa na siasa za kusini mwa
Afrika na Mashariki ya kati.
Ni vigumu
kueleza mambo mengi kuhusu mchango wake kama mwanataaluma katika wasifu huu
ambapo eneo moja kubwa la utafiti na ushauri,aliweza kuchapisha vitabu vingi na
makala nyingi katika vitabu na majarida ya kitaifa na kimataifa.
Ni machache
niliyoyaeleza kuhusu marehemu Profesa Haroub Miraj Othman ambae kwa anaemjua na
asiemjua ataamini kwamba Profesa alikuwa kiungo mahiri katika jamii ya
Kitanzania.
Hivyo basi
hakuna budi kwa wasomi na wasiowasomi kufuata nyayo za marehemu kutokana na kuwa
mhamasishaji na mpiganaji wa haki za binaadamu hasa wanyonge.
Marehemu
Profesa Haroub alizaliwa Novemba 30 mwaka 1942 katika mtaa wa Baraste Kipande
na kuanza masomo yake katika skuli ambayo ikijulikana kwa jina la French
Comorian School ilioko katika mtaa wa Kajificheni mnamo mwaka 1949.
Mwaka 1958
marehemu alichaguliwa kujiunga na chuo cha UwalimuBeit el Rass ambapo baadae
ambapo baadae alijiunga na elimu ya juu Urusi katika chuo kikuu cha Moscow
ambapo huko alipata shahada hya uzamili wa sheria (LLM) mwaka 1967.
Mwaka 1969
alipata shahada ya Diploma ya sheria katika chuo kikuu cha Hague,Uholanzi na
mwaka 1980 alipata shahada ya uzamivu (PHD) chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Marehemu
aliajiriwa katika chuo kikuu cha Afrika Mashariki mwaka 1969 ambapo mwaka 1970
aliajiriwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam hadi pale Mwenyezi Mungu
alipochukua roho yake .
Alianza kazi
katika kitivo cha sheria kwa muda mfupi na baadae alihamia katika taasisi ya
taluma na maendeleo.
Marehemu
aliweza kushika nyadhifa mbali mbaliikiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi mwaka
1981-1982 na baadae alikuwa Mkurugenzi kamili kwa vipindi viwiwli mfululizo
1982-1988.
Pia marehemu
aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UDASA pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi.
Marehemu
alikuwa ni mchapa kazi,alikuwa ni mtu aliejitolea katika maisha yake na kutetea
wanyonge ndani na nje ya nchi.
Marehemu
Profesa Haroub kabla ya kifo kumkuta Juni 27 mwaka 2009 alishiriki katika
uzinduzi wa kitabu cha ‘Race Revolution and the
Struggle’ kinachozungumzia maisha ya kisiasa ya Makamo wa Kwaza wa Rais
Maalim Seif Shariff Hamad.
Kitabu hicho
pia kinazungumzia maisha ya mwanasiasa mkongwe na Waziri wa Elimu wa zamani Ali
Sultan Issa ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Baytul-Yamin uliopo
Funguni mjini Unguja.
Aidha
marehemu usiku wa Juni 27 hiyo hiyo alishiriki uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa
la Filamu kwa Nchi za Jahazi(ZIFF) ambapo mwandishi wa makala hii alibahatika
kumuona siku hiyo marehemu akisalimiana na Waziri Kiongozi mstaafu wa
Zanzibar,Shamsi Vuai Nahodha ambae alikuwa mgeni rasmin siku hiyo.
Profesa
Haroub ambae ameacha mke ambae nae ni Profesa Saida Saleh Yahya na mtoto wao
Mmoja Tahir Haroub Othman.
Alifariki
dunia asubuhi ya Juni 28 mwaka 2009 kama leo na kuzikwa Juni 29 katika makaburi
yaliopo kijijini kwao Chuwini.
Mwenyezi
Mungu amsameh makosa yake na amlaze mahali pema peponi Aamin.
Makala hii
imepatikana kupitia kitabu maarufu cha ‘Haroub Othman Farewell to the Chairman’
kwa msaada wa kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar