Friday, 12 June 2015
WATANZANIA WATIKWA KUENDELEZA UTAMADUNI WAO
Na Aboud
Mahmoud,Zanzibar
IPO haja kwa
wananchi wa Tanzania kuendeleza na kudumisha utamaduni wao ili kuweza
kujitangaza kitaifa na kimataifa pamoja na kuvuta watalii wengi ili kuja kuona
tamaduni zao.
Hayo
yamesemwa na Balozi wa Uswiss ambae amemaliza muda wake Olivier Chave, katika
sherehe za kutimiza miaka 14 ya Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi Zanzibar
(DCMA) pamoja na kumuaga yeye mwenyewe
ambae ni mfadhili mkuu wa chuo hicho.
Alisema
kwamba utamaduni wa nchi ndio kitu muhimu ambacho watu wengi kutoka nchi mbali
mbali hupenda kukijua na kuvutia watalii wengi ambao huongeza mapata ya nchi.
Alisema
kwamba zipo nchi nyingi duniani zimekuwa zikipata wageni wengi kupitia kukuza
utamaduni wao pamoja na kuutangaza ndani na nje ya nchi kutokana na kushirikiana
baina ya wananchi na Serikali.
“Nawaomba
wafanyabiasha, na wadau wa sekta mbali mbali kuunga mkono utamaduni wa Zanzibar
kwani tukiiwachia Serikali na wasanii peke yake nchi hii haitoweza kujitangaza
na kupata mafanikio ya aina mbali mbali,”alisema.
Aidha balozi
Chave aliikisifia chuo cha DCMA kwa kuwa mstari wa mbele kuwarithisha vijana wa
Kitanzania katika utamaduni wa mambo mbali mbali ikiwemo ngoma za asili.
Hivyo
aliwashauri walimu na uongozi wa bodi hiyo kutochoka katika kuwarithisha vijana
hao na sanaa ambayo inahitaji kuendelezwa katika kuitangaza Tanzania na
Zanzibar kwa ujumla kitaifa na kimataifa.
Katika
sherehe hizo mabzo zilifanyika katika chuo hicho kulifuatiwa na burudani mbali mbali ikiwemo taarab, na ngoma za
asili.
BALOZI SEIF: DUMISHENI NIDHAMU KWENYE MICHEZO
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amehimiza umuhimu wa wanamichezo kuendelea kudumisha nidhamu michezoni ili
kulijengea sifa
Bora Taifa katika sekta hiyo kwa kuwa na wanamichezo walishiba
maadili na heshima iliyotukuka.
Balozi Seif Ali iddi alitoa himizo hilo wakati
alipokuwa akizungumza na wachezaji pamoja na Viongozi wa Timu ya Soka ya Taifa
ya Jang’ombe { Wakombozi wa Ng’ambno } katika hafla ya kukabidhiwa Kikombe cha
ubingwa baada ya Timu hiyo kupanda Daraja la kwanza Kanda mwaka huu.
Alisema nidhamu na heshima ndio kitu pekee
kilichosababisha wachezaji wa enzi zilizopita hapa Zanzibar kuwika na hatimae
kuiletea sifa Zanzibar katika ulimwengu wa kabumbu.
Balozi Seif alieleza kwamba Vijana wa sasa wana
nafasi pana ya kuendelea kujifunza mbinu mbali mbali za michezo na hatimae kuwa
mastaa ambazo hupatikana kupitia kwenye vipindi vya Televisheni pamoja na
mitandao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza
wachezji pamoja na Viongozi wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe kutokana na
kazi kubwa waliyoifanya na hatimae kuchukuwa ubingwa kwa kuingia daraja la
Kwanza Kanda.
Balozi Seif alisema juhudi za wachezaji hao kwa
upande mwengine zimeanza hatua mpya ya kujijengea uwezo wa kupata ajira kupitia
mchezo wa soka ambao unaonekana kupendwa sana Duniani.
“ Wapo wachezaji maarufu wanaochezea timu
zinazotajika Duniani katika ulimwengu wa kabumbu ambapo wengine wanatokea hata
mataifa ya Afrika yanayolingana kiwango cha soka na Tanzania “ Alisema Balozi
Seif.
Katika kuunga mkono wanamichezo hao wa Timu ya Soka
ya Taifa ya Jang’ombe Balozi Seif ameahidi kuisaidia Timu hiyo Seti mbili za
Jezi pamoja na Mipira Minne na akawataka wajiwekee malengo zaidi ya kufanikiwa
katika fani yao hiyo kwa siku zijazo.
“ Wale Jamaa wakikuoneni mnavyolisakata soka sawa
sawa kikweli watafikia hatua ya kukununueni tuu na kwa upande mwengine Zanzibar
tutakuwa na haki ya kujigamba kwamba tumetoa wachezaji wanaouwezo wa kuchezea
timu za Kimataifa “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala ya ujenzi wa Jengo la kudumu la
Timu hiyo ya Taifa ya Jang’ombne Balozi Seif aliwashauri Viongozi na wachezaji
hao kuanza ujenzi wa msingi na yeye atakuwa tayari kusaidia matofali kwa hatua
ya kunyanyua.
Alisema uwezo wa kujenga jengo lao uko mikononi
mwao ambapo viongozi wao jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kwamba wanasaidia
nguvu na maarifa ili kuona malengo waliyojipangia yanakwenda hatua baada ya
hatua.
Mapema Rais wa Timu ya Soka ya Taifa ya Jang’ombe
Salim Ridhiwani alisema Uongozi wa Klabu hiyo umeamuwa kuimarisha Timu hiyo ili
kurejesha heshima na hadhi ya klabu hiyo iliyopotea katika miaka ya hivi
karibuni.
Ridhiwani alisema Wanachama wa klabu hiyo
wanajivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya klabu hiyo hasa kutokana
na wachezaji wa timu hiyo kuiwezesha timu yao kuyakabili mashindano makubwa ya
Kombe la Mapinduzi na kutoa upinzani mkubwa kwa timu zenye uzoefu wa mashindano
ya soka Kimataifa.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mohammed Said
Dimwa alisema Uongozi wa Jimbo hilo umeifufua tena Timu hiyo ndani ya Kipindi cha
miaka Miwili iliyopita baada ya kufifia kutokana na changamoto kadhaa
zilizokuwa zikiikabili timu hiyo katika miaka ya nyuma.
Dimwa aliahidi kwamba yeye pamoja na viongozi
wenzake watasimama imara katika kuhakikisha Timu hiyo inarejea katika hadhi
yake iliyopewa na wapenzi wa timu hiyo ya kuitwa wakombozi wa Ng’ambo.
Timu ya Taifa ya Jang’ombe { Wakombozi wa Ng’ambo }
ilipanda Daraja na kushiriki mashindano ya Daraja la Kwanza Kanda mwaka huu
baada ya kuifunga Timu ya Soka ya Maungani Goli 1-0 katika mchezo wa Mwisho wa
mashindano ya Ligi Daraka la Pili.
RUKIA RAMADHANI: MSANII ASIEPENDA KUITWA MALKIA WA MIPASHO
“NIKUMBATIE mwenye wivu atazame,Nikumbatie roho yake imuume
Nikumbatie mwenye wivu
alalame,Nikumbatie akujue wangu mume
Njiani nikipita arudi kinyume nyume,Kata kiu yeye Fanta mi
sina habari nae
Ajijue cheo chake mina yeye hatufanani,Atuone ashituke anijue
mimi nani
Cheza na mimi mpenzi cheza name kwa helenzi,Mambo mazuri
laazizi ndo hayataki haraka”
Ni moja ya beti katika nyimbo maarufu za muziki wa taarab
visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wa wimbo unaojulikana kwa jina la
‘Nikumbatie’ ambao uliimwa katika kundi maarufu la East African Melody.
Maneno hayo ni miongoni mwa wimbo mzima ulioghaniwa na
mwanadada mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni sie mwengine bali ni bibie Rukia
Ramadhani Ali.
Rukia ni msanii mahiri katika anga la muziki wa taarab ndani
nan je ya Tanzania ambae kila kona ya dunia anajulikana kutokana na kipaji
chake alichojaaliwa na muumba wake.
Msanii huyo ambae hapendelei kuitwa malkia wa mipasho kutokana na kutopendelea kuimbwa nyimbo za
kupashana na kuelekeza zaidi nguvu zake katika nyimb o za mahaba na
kubembeleza.
Nilipomuuliza anajiskiaje kuitwa jina hilo la malkia wa
mipasho,hakuonesha bashasha wala haiba yake ya kawaida ya kutabasamu na akajibu
‘sitaki kuitwa malkia wa mipasho kwa sababu siimbi wala sifikirii kuimba
mipasho’.
Jibu hilo lilinifanya nishangae kidogo kwa vile nyimbo za
mipasho ndio zaidi hivi sasa zinazowapa umaarufu mkubwa waimbaji wake kiasi cha kumuuliza nini sababu
ya msimamo wake huo.
“Mimi ni msanii ninaependa zaidi taarab asilia ambayo lugha
ya mashairi yake ni ya kiungwana,haina maneno makali tofauti na taarab ya
kisasa,wanaimba tu lakini haina maadili ya Kizanzibari au taarab kwa
ujumla,”alisema bila ya kutaka kuingia ndani zaidi.
Nilipotaka kujua alipoanzia hadi alipofikia,Rukia hakukataa
tulikwenda hatua kwa hatua hadi mwisho wa mazungumzo yetu,alipoanzia alipofikia
na matarajio yake ya baadae.
Msanii huyo alisema alijitosa rasmin katika fani ya muziki
mwaka 1974 katikam kikundi cha Tawi la Afro Shirazi Party la Mwembeshauri chini
ya mwalimu wake Marehemu Khamis Shehe.
Alisema wakati huo walikusanywa watoto wengi wa mtaani hapo
kwa ajili ya kufundishwa masuala ya uimbaji na baada ya mafunzo ya muda walipelekwa
majaji wenye uelewa mpana wa muziki huo na uimbaji kwa kuwachuja vijana hao.
Rukia alikuwa miongoni mwa vijanan waliopenya katika mchujo
wa majaji hao na hapo ukawa mwanzo wa mafanikio
yake kwa vile kupita huko kulimfanya apelekwe katika klabu maarufu ya
tab visiwani humu ya Culture Musical Club yenye maskani yake katika mtaa wa
Vuga mjini Unguja.
Alianza mazoezi katika klabu hiyo na hatimae kuanza kuimba
akiwa bado mwanafunzi wa shule na hivyo kuweza kubeba majukumu yake yote ya
usanii na masomo shuleni.
Alisema alianza rasmin kuanza kupanda jukwaani akiwa na kundi
lake la Culture na nyimbo yake ya kwanza ilijulikana kwa jina la ‘Kukupenda
sana ndilo kosa langu sitofanya tena naapa kwa Mungu,Nilioyaona yanatosha
kwangu’.
Kutoka kwake huko kuliwashtua wazazi wake ambao waliona
kwamba anajikita zaidi katika maswala ya nuimbaji,badala ya kuzingatia masomo
yake hivyo ilimsababishia kuhamishwa
Zanzibar na kupelekwa Dar es Salaama
kuendelea na masomo.
Msanii huyo mahiri alieleza kwamba alikaa jijini humo kwa muda wa miaka minne na kuendelea na masomo katika shule ya msingi ya Temeke kabla ya kurejea Unguja kuendelea na masomo yake katika shule ya Rahaleo,Kidutani ndogo na kubwa ambapo alimalizia kidato cha nne.
Msanii huyo mahiri alieleza kwamba alikaa jijini humo kwa muda wa miaka minne na kuendelea na masomo katika shule ya msingi ya Temeke kabla ya kurejea Unguja kuendelea na masomo yake katika shule ya Rahaleo,Kidutani ndogo na kubwa ambapo alimalizia kidato cha nne.
Kurejea kwake Unguja kulimfanya arudie tena kwenye muziki wa
taarab na kwa bahati mbaya au nzuri hakurejea tena katika kundi lake la awali
bali alihamia kwenye kundi mama la Nadi Ikhwan Safaa.
Alisema akiwa ndani ya kundi hilo,lenye maskani yake katika
mtaa wa Kokoni mjini Unguja alikweza kuimba nyimbo kadhaa ambazo ziliweza
kumjengea jina na kumpa umaarufu zaidi.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Nnazama, Nadra na
Sadfa,Hidaya, Baada ya dhiki faraja,Niapishe na nyiengine nyingi ambazo zote
hizo zinaendelea kupendwa hadi hivi sasa.
Rukia alisema kuanzishwa kwa kundi jipya la taarab la Bwawani
ambalo lilikuwa linamilikiwa na hoteli ya Bwawani kulimfanya ahame katika kundi
lake hilo na kuhamia katika kundi la Malindi chini ya msanii mahiri Marehemu
Mwalimu Abdallah .
Alisema kikundi hicho cha Bwawani hakikudumu muda mrefu sana
kwa vile kilivunjika,lakini kabla ya kuvunjika msanii huyo alifanikiwa
kukiimbia kikundi hicho nyimbo kadhaa zikiwemo Nidhibiti,na Nadekea change.
Baadhi ya maneno yaliokuwemo katika nyimbo ya Nidhibiti ni
kama hivi
Nidhibiti unitunze,Nitunze nihifadhike
Nihifadhi wanyamaze,Nipoe nitononoke
Raha zako nieneze,Milele milele nifarijike
Miti shamba wamalize,Halafu waweweseke.
Rukia ambae ni miongoni mwa wasanii waanzilishi wa kundi la
‘The East African Melody’ ambalo llilianzishwa nchini Dubae mwaka 1992,akiwa na
wasanii kadhaa.
Akiwa nchini humo nyimbo za mwanzo alizoimba ni pamoja na
Karibu habibi,Nimesharidhika na Nasubiri miujiza na baadae kundi hilo lilihama
nchini Dubae na kuhamia visiwani Zanzibar.
Katikati ya mwaka 2000 msanii huyo alipumzika kuimba kwa muda
wa mwaka mmoja hadi mwaka 2001 aliporejea tena kwenye ulingo wa taarab na kundi
lake hilo la East African Melody.
Mara baada ya kurejea tena msanii huyo alionekana kuendelea
kuvutia zaidi kutokana na kuimba nyimbo
zake kadhaa ambazo zilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi wa muziki wa
taarab .
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na Njoo Habibi,Nani kama
wewe,Wastara hasumbuki,Kufa na tai shingoni,Nataka ridhaa yako,pamoja na nyimbo
ya Nikumbatie.
Mbali na kuimba Rukia anamudu saana sanaa ya uigizaji ambapo
aliwahi kuigiza mchezo wa ‘Mkombozi wa Mwafrika’ambapo alisema kwamba uimbaji
uliweza kumletea matatizo kutoka kwa watu mbali mbali ikiwemo kumtishia kumpiga
na hata wengine kutaka kumuwekea sumu kwenye chakula.
Pamoja na kutishiwa huko na vitisho hivyo msanii huyo
alikabiliana na changamoto hizo ambazo hazikumkatisha tama na kuendelea na
shughuli yake hiyo aliyokiri kuipenda ndani ya damu yake.
Rukia hakufafanua kwa nini alitishiwa,lakini alisema hayo ni
mambo ya zamani na kwa sasa ayameshapita.
“Kwa kweli nilipokuwa najiunga na mambo ya sanaa nilipata
tabu saana kwani nilitishiwa kupigwa na hata kuambiwa nitatiliwa sumu kwenye
chakula lakini hayo yalikua mambo ya zamani sasa hivi hayapo,”alisisitiza.
Kuhusu maswala ya faida katika fani ya sanaa,Rukia alisema
muziki wa taarab umeweza kumsaidia kupata faida nyingi ikiwemo
umaarufu,kuheshimiwa na watu wa rika mbali mbali pamoja na kusafiri.
Alizitaja nchi alizotembelea kupitia muziki wa taarab ni
pamoja na Mikoa mbali mbali ya Tanza
nia,Kenya,Msumbiji,Comoro,Nigeria,Misri,Dubae,Oman,Abu Dhabi,Jamhuri ya
Dominica,Ufaransa,Uswiss,Ubelgiji,Italia,Uholanzi,Slovenia,Ujerumani,Japan,Marekani
na Uingereza.
Rukia alisema mpaka sasa kwa yeye ni taarab asilia ambayo ndio
mwalimu wake katika fani hiyo lakini pia hiyo haimzuii kuimba taarab ya kisasa.
“Taarab asilia ndio taarab hizi nyengine tunaimba tu kufuata
wakati,mimi siwezi kuidharau kwa kuwa ndiko nilipoanzia,”alifahamisha.
Akizungumzia juu ya tabia ya wasanii kuhama hama vikundi mara
kwa mara ,alisematabia hiyo sio nzuri ,lakini ijulikane kwamba msanii hawezi
kuhama bila ya sababu maalum.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba kuhama kwake hakutokani
na maslahi,bali kutokana na matatizo mbali mbali yaliokuwa yakijitokeza.
Msanii huyo hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa
wasanii mbali mbali ambao walimuwezesha kudumu katika fani hiyo akiwemo
marehemu Asha Simai,marehemu Khamis Shehe na Mohammed ilyas.
Kwa vile hakuna msanii
yoyote ambae hana msanii anaemvutia ,kwa upande wake Rukia alisema anavutiwa na
uimbaji wa wasanii wengi akiwemo marehemu Asha Simai,Marehemu Abdulaziz Yussuf
na Profesa mohammed Ilyas.
“Marehemu Bi Asha Simai alikuwa akinivutia mno katika fani
yake ya uimbaji hasa nyimbo ya iwapi ile ahadi, inanisuuza roho yangu Namuomba
Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake,”alisema msanii huyo.
Hivi sasa Rukia Ramadhani ni muimbaji huru ambae anaimbia
vikundi tofauti anapopata mualiko kikiwemo kikundi cha Zanzibar One Modern
Taarab na vikundi vyengine.
Pia msanii huyo ni mwalimu wa sauti(kuimba) katika Chuo cha
Muziki wa nchi za Jahazi(DCMA) ambapo aliwataka wasanii kujifunza zaidi mara wanapoingia katika fani hiyo.
“Nawashauri wasanii kujifunza zaidi kusoma muziki ili waweze
kujifahamu na kuelewa nini wanachokifanya jukwaani kwani wasanii wengi hawataki
kujifunza.
Rukia Ramadhani Ali ni mtoto pekee wa bwana Ramadhani Ali na
Bi Zuhura ambapo mbali na fani ya usanii lakini pia ni muajiriwa wa serikali
katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Thursday, 11 June 2015
WANAHABARI WATAKIWA KUTUMIA KALAMU ZAO ILI KUDUMISHA AMANI
WAANDISHI wa
habari nchini wametakiwa kuacha kuandika habari ambazo zitakazosababisha
kusababaisha vurugu na kuondosha amani iliyopo nchini Tanzania hasa katika kipindi cha uchaguzi.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar
(ZAMEWO) Maryam Hamdani, wakati alipokua akifungua mafunzo ya siku mbili kwa
wanahabari juu ya haki za binadamu na sharia za waandishi,huko katika ukumbi wa
Kituo cha Huduma za Sheria.
Mwenyekiti
huyo alisema kwamba nchi kadhaa duniani zimekuwa zikitokea kwa fujo kutokana na
wanahabari kuandika habari ambazo zinahamasisha kwa wananchi kufanya vitendo
ambavyo husababisha kuvunjiika kwa amani.
Alisema
kwamba si vyema kuonekana nchi kama Tanzania ambayo ni nchi yenye amani
kuharibika kutokana na maneno makali yanayozungumzwa na wanasiasa na wanahabari kuyafikisha kwa jamii.
“Nakuombeni
wanahabari wenzangu tuzitumie kalamu zetu kwa kuandika habari ambazo zitasaidia
kudumisha amani iliyopo nchini kwetu na sio kuandika habari ambazo
zitasababisha kuvunjika kwa amani,”alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha
aliseleza kuwa chuki za wanasiasa na maneno ya hasira yanayotoka katika midomo
ya viongozi hao wa kisiasa yakiandiikwa katika na kutangazwa katika vyombo vya
habari yanaweza kusababisha hali ya hatari katika nchi.
“Katika
kipindi kama hichi cha uchaguzi hutokea mambo mbali mbali na kauli za kutisha
na za hasira kutoka kwa wanasiasa,hivyo nakuombeni kuacha tabia ya kuandiika
maneno hayo ili Tanzania isije ikawa kama Burundi au nchi nyengine,”alifahamisha.
Hivyo
aliwataka wanahabari hao kusaidia kuwaelimisha wananchi kuleta na kuiendeleza
amani iliyopo hapa nchini pamoja kuielimisha Serikali kulinda amani iliyopo.
Mafunzo hayo
ya siku mbili kwa waandishi wa habari yameandaliwa na Kituo cha Huduma za
Sheria Zanzibar (ZLSC) kwa kushirikiana na Chama cha Waa ndishi wa Habari za
Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA).
ABDULWAKATI: NYOTA ISIYOSAHAULIKA KATIKA FANI YA SOKA NA TENISS
ZANZIBAR ni
moja ya nchi ambazo zimejaaliwa kuwa na vipaji vya aina mbali mbali,vikiwemo
vya utunzi,ufinyanzi na hata katika maswala ya michezo,ambayo kwa kiasi fulani
ilitamba katika michezo ya aina tofauti.
Miongoni mwa
watu waliotamba visiwani humu katika mchezo wa soka na mpira wa mezani Abdullah
Juma Aley almaaruf Abdulwakati ambae aliweza kuitikisa Zanzibar nan chi
nyengine duniani michezo hiyo.
Kama utataja
majina ya watu waliowahi kutamba visiwani humu katika mchezo wa mpira wa meza
na soka bila ya kumtaja Abdulwakati itakuwa hukumaliza idadi yao.
Abdullah
Juma Aley ndio jina lake alilopewa na wazazi wake,lakini hata hivyo jina hilo
linafahamika kwa watu waliokuwa sio wengi kwani ukipita katika mitaa mingi ya
visiwani humu ikiwemo Kikwajuni na kumtaja jina la Abdullah hutompata mpaka
utaje Abdulwakati.
Jina hilo
ndio limekuwa maaarufu kuliko jina lake halisi kwa kipindi chote alichocheza
michezo hiyo Zanzibar,Tanzania,Afrika Mashariki na hata Arabuni .
Mwandishi wa
makala haya alimtafuta mwanamichezo huyo huko nyumbani kwake Michenzani na
kuzungumza nae kwa kina katika mambo mbali mbali yanayomuhusu yeye kimichezo.
Alisema
kwamba umaarufu wa jina la Abdulwakati hautokani na kitu chochote isipokuwa ni
mchezo wa soka ambao ulimpatia umaarufu mwaka 1980 na kuendelea.
Alisema
kwamba jina la Abdulwakati alilipata wakati alipokuwa mdogo akichezea timu ya
hero Boys ambapo alisema jina hilo alibatizwa na mwalimu wake wa soka Abubakar
Soni.
“Katika timu
yetu kulikujwa na wachezaji watatu na wote walikiuwa na majina ya Abdul ,hivyo
kutotufautisha sisi akaamua mimi kuniita Abdulwakati kwa vile nilikuwa nachezea nafasi ya
mshambuliaji wa kati,”alisema.
Mchezaji
huyo mkongwe ambae kwa kawaida ni mcheshi,alisema wachezaji wenzake walibatizwa
majina mengine kama vile Abdul Kikono na Abdul Kifupi.
Katika
maisha yake ya soka,alianza kung’ara mapema utotoni mpaka kupewa mikoba ya
unahodha kwenye timu ya shule visiwani Zanzibar.
Aliendelea
kucheza timu ya watoto kabla ya kujiunga na klabu ya Everton iliyokuwa na
maskani yake katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja mnamo mwaka 1970.
Kutokana na
uwezo wake mkubwa wa kusakata kabumbu Abdulwakati alichukuliwa na timu
iliyokuwa ikimilikiwa na kituo cha kulelea watoto cha Forodhan iliokuwa
ikijulikana kwa jina la Karume Boys na kutembea nayo katika mikoa mbali mbali
ya Tanzania.
Timu hiyo
ambayo ilikuwa chini ya uangalizi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehem Mzee
Abeid Aman Karume ambapo timu hiyo ilikuja kugawanyika mara baada ya kifo cha kiongozi
huyo mwaka 1972.
Akiwa katika
kikosi hicho cha Karume Boys alikutana na wachezaji wengi akiwemo Sihaba
Saadat,Omar Willium na wengine wengi.
Mnamo mwaka
1972 baada ya kusambaratika kwa Karume Boys,Abdulwakati alijiunga na kikosi cha
Small Simba baada ya kushawishiwa kufanya hivyo na kocha wa zamani wa kikosi
hicho ,Masoud Salim almaarud Maoud Kocha.
Kutokana na
ari,jitihada na moyo wake wa kusakata kabumbu wakati anapokuwa uwanjani,veteran
huyo alichaguliwa kujiunga na timu ya Taifa ya vijana ya Zanzibar mwaka huo huo
1972.
Akiwa na
Small Simba,Abdulwakati alikuwa kivutio kikubwa sawa na wachezaji wote wa timu
hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa baada ya kupanda daraja,ambapo ilianza kwa
moto mkubwa na kutikisa vigogo vya soka nchini.
Alisema timu
yao ilikuwa imesheheni vipaji na kuwa gumzo la mji na kuanza kujitwalia ubingwa
wa soka visiwani mwaka mwaka huo huo waliopanda ngazi 1983.
Chini ya
nyota mahiri akiwemo wakati,Small Simba iliweza kutamba vilivyo katika miaka
1985 hadi 1987.
“Kuanzia mwaka
1983 hapo moto wetu ulikuwa hauzimiki na mashabiki wetu wakapata wimbo wa ‘Moto
Small’ambapo kila tulipokuwa tunashuka dimbani au watu walipokuwa wakizungumzia
timu yetu waliimba Moto Small,alisema mwanandinga huyo.
Jambo ambalo
nyota huyo atabaki akilikumbuka maishani kwake ni tukio la mwaka 1987 kwa timu
ya Small Simba kupokonywa ubingwa na Miembeni ambao walikwenda mahakamani.
Anasema
anafahamu kwanini walishindwa kesi hiyo na kila mmoja alijua kutokana na hakimu
wa kesi hiyo alikuwa Miembeni damu,hivyo alisema haki haikutendeka.
Abdulwakati
alisema kwamba sababu za kwenda mahakamani wenzao na kupokonywa ubingwa
kumetokana na wenzao wa Miembeni kudai kwamba walimchezesha mchezaji Shaban
Mussa ambae hakuwa halali,licha ya chama cha soka Tanzania (FAT) kuthibitisha
mahakamani kuwa mchezaji huru.
Umahiri wake
katika soka uliwashawishi wahusika wa juu kumuita kwenye timu kubwa mwaka 1984
na kushiriki katika michuano ya Chalenji iliofanyika mjini Mombasa nchini
Kenya.
Milango ya
kheri ikamfungukia siku chache baada ya kurudi kutoka Mombasa,ambapo mashushu
wa Oman walikuwepo kusaka wachezaji wa kuwapeleka kwao.
Mwaka 1984
Abdulwakati alitua rasmin nchini Oman na kuanza kuwasuuza roho Waarabu kwa ufundi wake wa kumiliki mpira na
kupachika mabao.
Alisema
mechi yake ya kwanza ilikuwa kati ya Oman na Qatar katika michuano ya ubingwa
wa nchi za Ghuba akicheza kwa dakika 20 tu.
Aidha katika
mechi ya kihistoria iliyochezwa Riyadh Saudi Arabia ikiwa ni michuano ya Gulf
ushindi wa kwanza kwa Oman ulipatikana baada ya kurudi kambi nchini Brasil ambapo
Abdulwakati alifanikiwa kuipatia timu yake goli moja na timu yake kuibuka na
ushindi wa magoli 2-1.
Kutokana na
kipigo hicho Qatar ilimkatika rufaa Abdulwakati kwa madai kwamba ni
mgeni,lakini rufaa hiyo ilishindwa kwani nao pia walikuwa na wachezaji kutoka
Somalia wawili.
Hata hivyo
mchezaji huyo alikuwa halali kuchezea timu hiyo ya Oman kutokana na kufanyiwa
taratibu zote za uraia.
Baada ya
hapo akawa anapangwa mechi zote kwa dakika 90 na kuwashangaza matajiri wake kwa
kipaji alichokuwa nacho.
Anakumbuka
matokeo mazuri ni yale ya sare1-1 walipocheza na U.A.E ambao ni wapinzani
wakubwa wa Oman sawa na timu za Kenya na Uganda.
Anafahamisha
kwamba kila mwaka Oman ilikuwa ikishika mkia katika mashindano ya ‘Gulf Cup’
lakini katika mashindano hayo walishika nafasi ya nne kati ya nchi sita.
Pamoja na
mafanikio makubwa aliyoyapata katika nchi ya Oman,mchezaji huyo anakumbuka
kadhia iliyowakasirisha wachezaji baada ya kutwaa ubingwa wa Ghuba ambapo chama
cha soka na Wizara husika kushindwa kutimiza ahadi zao kwamba wangewapa zawadi
nono.
Akiwa na
timu hiyo,mwanasoka huyo veteran alifanikiwa kwenda katika nchi zote za ghuba
kushiriki michuano yao inayochezwa kwa zamu.
Katika
kumbukumbu yake alifahamisha kuwa wakati wakijiandaa na mashindano ya
Bahrainwalipiga kambi nchini Ufaransa na akabahatika kufundishwa na kocha Omar
Boras raia wa Uruguay mwaka 1988 hadi 1990, ambae alikuwa kocha wa nchi yake
katika mashindano ya kombe la dunia yaliofanyika Mexico mwaka 1986.
Baada ya
kumaliza waliyotumwa kwa Oman kuwa mabingwa wa Ghuba zilizjitokeza baadhi ya
timu kumtaka na hatimae alijiunga na klabu maarufu ya Fanja ilioko nchini Oman.
Wakati huo
alisema alikuwa ni Mtanzania wa kwanza kujiunga na Fanja mwaka 1985,kabla ya
kina Ahmed Amasha,Talib Hilal,Zahor Salim na Hilal Hemed.
Akiwa na
timu hiyo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Oman mara nyingi sambamba na kombe la
Sultan Qaboos kuanzia mwaka 1985 hadi 1992.
Aidha
alisema mwaka 1987 alirudi Zanzibar kwa ajili ya mapumziko na kwenda na timu ya
taifa nchini Ethiopia kwenye Chalenji ambapo walitoka sare na Kenya huku
Tanzania Bara wakiifunga magoli 2-0 na
kutoka sare na Ethiopia katika mechi ambayo mlinda mlango alikuwa Ali Bushiri
ambae aliokoa kwa penalti.
Hata hivyo
kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na makocha Gulam Abdallah na marehemu Mzee
Kheri kilitolewa na Zimbabwe katika hatua ya nusu fainali.
Anaelezea
kitendo cha muamuzi kuwabeba Wazimbabwe kilichangia kufungwa kwani walipokua
nyuma kwa mabao 2-1, Inocent Haule alisawazisha lakini likakataliwa.
Abdulwakati
ambae tangu akiwa kinda,alikuwa na lengo la kuchezea soka la kulipwa,anasema
aliwahi kushawishiwa na viongozi wa Simba wakati huo akiwa na timu ya Taifa
Stars lakini aligoma kwa vile hakuyaka kuihama Small Simba.
Kwa upande
wa mechi ambayo anaikumbuka akiwa na klabu ya Small Simba,siku moja walikwaaana
na Yanga katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
ambayo ilifanyika Mombasa Kenya.
Anasema
Small Simba wakiwa nyuma kwa magoli 2-0
hadi mapumziko, ndani ya chumba cha kubadilisha nguo alimuomba kocha
Abdulghani Msoma amtoe nahodha Fadhil Ramadhani.
Anasema
kufuatia mabadiliko hayo wakaweza kurudisha bao moja na ikiwa zimebakia dakika
10,mchezaji mwezake aliemtambulisha kwa jina la Kirara ambae kwa sasa ni
marehemu alimzidi maarifa Juma Mkambi
kasha akatulia na mpira akaja akamtoboa tena na kutoa pasi kwa Rashid Khamis
aliepachika bao la pili.
Kwa upande
wa mabeki ambao walikuwa wakimpa tabu wakati huo na timu zao kwenye mabano ni Hassan
Wembe(Malindi), Abdallah Rajab(KMKM) na Said Ibrahim Njunju(Miembeni).\
Mwanandinga
huyo alisema kwamba alikuwa akijisikia fahari sana akiona anacheza na kikosi
kizima cha Small Simba lakini zaidi akiwa na Yussu Kassim na marehemu Kassim
Kirara na mabeki Khamis Suleiman ‘Mpemba’ na Khalfan Ukasha.
Aidha
Abdulwakati hakuacha kusifia umahiri wa mlinda mlango wa zamani wa wapinzani
wao Black Fighters,Mwinjuma Makungu (marehemu) kwa ujasiri wake wa kuzuia
michomo akiruka kwa staili ya kipekee.
Anasema
kwamba kwa kiasi kikubwa soka limemsaidia kufika katika nchi mbali mbali kama
Algeria, Misri,Zambia,Ufaransa,Brazil na nchi zote za falme za kiarabu Malaysia
na Thailand.
Lakini mbali
na kuwika katika mpira wa miguu,Abdulwakati alikuwa mahiri katika mchezo wa
mpira wa meza (Table teniss) ambapo lifanikiwa kuchezea katika ya Taifa ya
Tanzania na timu ya Taifa ya Zanzibar na kuwa mchezaji nambari moja nchi nzima.
Abdulwakati
alihamisha kwamba mwaka 1974 aliiwakilisha Tanzania huko Alexandra Misri na
kutolewa katika hatua za awali,ambapo mwaka 1977 alishiriki katika mashindano
ya Tanzania Table Teniss kwa nafasi ya senior na bahati nzuri alichukua ubingwa
wa mchezo huo kwa Tanzania nzima.
Abdulwakati
aliweza kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Tanzania kwa miaka minne mfululizo
katika michuano ya Coastal Town Champion Ship ambayo ilikuwa ikichezwa katika
jiji la Dar es Salaam,Tanga na Mombasa katika kipindi cha Sikukuu za Pasaka.
Mwaka 1978
mwanamichezo huyo sambamba na wenzake walibeba bendera ya Tanzania kwenye
michuano ya Afrika (All African Games) nchini Algeria.
Katika
mashindano hayo alitolewa na Nigeria katika robo fainali na kusema kwa
kawaida Wamisri na Wanigeria katika
mchezo wa mpira wa meza.
Mwaka huo
huo wa 1978,Abdulwakati aliungana na wenzake kutoka katika Mikoa ya Tanzania
kushiriki katika mafunzo ya miezi sita kwa mchezo huo na kufundishwa na
aliekuwa bingwa wa dunia,Liyanko Liyang.
Aliwataja
wachezaji wenzake aliokuwa nao ni pamoja na Fatma Jidawi,Narman Jidawi,Shaaban
Umiki,na Mohammed Salum wote kutoka Zanzibar ambapo kutoka Tanzania Bara ni
Ahmed Diwani na Lucas Kiwango.
Alifafanua
kwamba kikosi cha mpira wa meza Zanzibar kilikuwa kizuri kutokana na mafunzo
waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa kocha wao Wu Li Yen ambae alikuwa Balozi mdogo
wa Jamuhuri ya Watu wa China.
Hivi sasa
Abdulwakati amekuwa akijumuika na wachezaji Veterani wengine hapa nchini kuunda
timu ya Wazee Sports Club inayofanya mazoezi yake kwenye viwanja vya kila siku
jioni.
Kuhusu
utofauti wa soka la zamani na sasa,Abdulwakati alisema soka la zamani lilikua
na tofauti kwani wachezaji wake walikuwa hawapati nafasi ya kucheza soka la
kulipwa katika nchi za Ulaya tofauti na sasa.
Aliongeza
kwamba wachezaji wa zamani walikuwa wakicheza kwa ari na nguvu zote tofauti na
ilivyo kwa wachezaji wa sasa kwani wamekuwa wanacheza kwa tamaa na fedha zaidi
na sio moyo wa kuzipenda timu zao.
Mchezaji
huyo mkongwe aliwashauri wachezaji hao kutopendelea kutumia vitu hivyo ambavyo
havitoweza kuwajengea viwango vyao katika uchezaji wa soka.
Huyo ndie
Abdulwakati aliezaliwa mwaka 1959 katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja na
kuanza elimu ya msingi katika shule ya Darajani mwaka 1967 na baadae kumalizia
masomo yake katika shule ya Vuga mwaka 1976.
Baadae
wazazi wake walimpeleka Mkoani Morogoro kwa ajili ya kurejea masomo yake ya
kidato cha tatu na cha nne katika Shule ya kilimo ya Ifakara.
Abdulwakati
ni baba mwenye familia ya watoto wawili Nawwal na Nageeb,hivi sasa ni muajiriwa
katika kampuni ya usafiri wa Anga Zanzibar (ZAT).
Wednesday, 10 June 2015
TAUSI WOMEN TAARAB: KUNDI LINALOPIGA MUZIKI WA TAARAB KWA KUTUMIA ALA ZA ASILI
TAUSI ni
mmoja wa ndege maarufu ambae ni mrembo alieumbika kutokana na umbo lake zuri la
kupendeza,uzuri huo pia huonekana kwa manyoya yake ambayo pia ni kivutio kwa
wengi wakiwemo watoto wadogo.
Nyimbo mbali
mbali ziliwahi kuimbwa ambazo zinaonyesha kumsifia ndege huyo na kuonekana
kuvuta mapenzi kwa watu wengi,lakini pia uzuzri wa ndege huyo kumefanya hata
kupatikana kwa jina la la mtu kwa uzuri wake.
Lengo langu
sio kumsifia wala kumzungumzia ndege huyo ,bali ni kuzuzngumzia mustakabali
mzima wa kundi la taarab la akina mama ambalo limeweza kujizolea umaarufu
mkubwa sana ndani nan je ya visiwa vya Zanzibar.
Mara baada
ya kuona kazi zinazofanywa na akina mama hao mwanzo mwa mwezi huu katika
tamasha la Sauti za Busara hamu na shauku kubwa ilinipata ya kutaka kujua
kiundani azma na lengo la kuanzishwa kwa kundi hilo.
Niliweza
kufika katika Makao Makuu ya Klabu hiyo yalipo katika maeneo ya Kisiwandui
mkabala na Msikiti Mabati mjini Unguja na kukutana na Mkurugenzi wa kundi hilo Bi
Maryam Hamdani.
Bi Maryam
alinielezea tangu kuanzishwa kwake,walipofikia na matumaini ya baadae ya kundi
hilo .
Tausi ni
kikundi pekee nchini Tanzania kinachopiga muziki wa taarab asilia ambacho
kinafanya shughuli zake zote kupitia akina mama wanaoongozwa na Mkurugenzi huyo
anaepiga ala ya Qanoon.
Sio jambo la
rahisi kuona akina mama hao wanaweza kufanya kazi hasa ya kupiga ala asilia
ambazo ni ngumu kutokana na ala hizo kutumika bila ya umeme na ndio jambo
lililonifanya niamini kwamba wanawake wakiamua wanaweza.
“Tangu utoto
wangu Tausi na Ziwarde nilikuwa nawapenda sana nikaamua nikaamua kukiita
kikundi hichi jina la ndege huyu na pia nilitaka kubadilisha majina ya vikundi
vya taarab na sio kila siku hayo kwa hayo,”alisema Bi Maryam.
Tausi
ilizaliwa rasmin Julai mwaka 2009 kikiwa na vijana wa kike 22 ambapo alianza
nao kwa kuwafundisha kupiga ala mbali mbali akiwa yeye na walimu wenzake
Marehemu Iddi Abdallah Farahan,Mohammed Ilyas,Ramadhan Muhidin na Ali Ibrahim.
Walianza kwa
kuwafundisha kutumia ala mbali mbali ikiwemo Qanoon,Udi,Fidla,Violin,Tablah,Key
board, Bongos na aina mbali mbali za ala ambazo zinatumika katika muziki wa
taarab asilia.
“Hamu yangu
ya kupenda muziki wa taarab na mimi mwenyewe nikiwa msanii na pia nafahamu
kutumia ala ya Qanoon ndio niaamua kuanzisha kikundi hichi ambapo nilianza na
akina mama 22,”alisema.
Mara baada
ya kuonekana kwamba upo umuhimu kutokana na kuanzishwa kwa kikundi hicho watu
mbali mbali wenye hamu ya kuwa wasanii ambao wanahitaji kujifundisha kutumia
ala walianza kujiunga na Tausi.
Mkurugenzi
huyo anafahamisha kwamba sharia ya kikundi hicho kuwa hakuna msanii yoyote
aliekuwemo ndani ya Tausi lazima ajue kupiga ala na sio kubakia kwenye kuimba
tu.
“Wapo
wasanii ambao walijiunga na Tausi wakiwa hawajuai chochote zaidi ya kuimba
tu,lakini nashukuru kutokana na jitihada ya Tausi na sharia yetu watu wote
wajue kupiga ala basi sasa hivi takriban wasanii wetu wote wanajua kutumia
ala,”alifahamisha.
Hakuna jambo
lizilokuwa na matatizo wala faida,lakini kwa upande wa matatizo yanayokikabili
kikundi hicho ni ukosefu wa vifaa ikiwemo kukatika kwa nyuzi ambazo zinatumika kwenye ala na
matatizo mengine amabayo alisemani ya kawaida tu.
Lakini kwa
upande wa faida,Tausi imeweza kupata faida mbali mbali ikiwemo kujua kupiga
ala,kujiajiri wenyewe kujua zaidi kutumia ala za asili,kupiga taarab katika
sehemu mbali mbali na kuweza kusafiri.
Mkurugenzi
huyo alizitaja sehemu ambazo wamebahatika kufanya maonyesho ni katika matamasha
ya busara kwa miaka mitatu,sherehe za mkutano wa EU sherehe za chakula cha
usiku kwa wadau wa elimu pamoja na uzinduzi wa mkutano mkuu wa AU uliofanyika
mjini Nairobi na kuhudhuriwa na alikekuwa Makamo wa Rais wan chi hiyo Raila
Odinga.
Lakini pia
Mkurugenzi huyo alisema kujwa faida nyengine kwa kundi hilo ni kuhudhuria
katika matamasha ya kimataifa yaliofanyika nchini Lebanoon na Misri.
“Hii ni
faida kwetu na faraja iliyoje kupata kufanya maonyesho katika sehemu mbali
mbali tena kubwa ambazi imeweza kutusaidia kukitangaza kikundi chetu pamoja na
nchi yetu kwa ujumla,”alieleza.
Aidha kundi
hilo pia limeweza kupiga nyimbo mbali mbali pamoja na Bashraf zao wenyewe
ambazo zimetungwa katika kundi hilo ambapo miongoni mwa watunzi hao akiwa yeye
mwenyewe Mariam Hamdani.
Tausi
linatamba na nyimbo zake mbali mbali zikiwemo Usione vyaelea,Walodhani mzaha,Nibembeleze,Si
rahisi na dhana ambapo kwa upande wa bashraf zinajuliakana kwa jina la Tausi na
Alya.
“Kundi letu
limeweza kutunga nyimbo pamoja na bashraf
ambapo tunapokwenda katika maonyesho huwa tunapiga nyimbo zetu
wenyewe,”aliongezea Mkurugenzi huyo.
Aidha kwa
upande wa matarajio ya kikundi hicho Maryam alisema ni matarajio yao
kuwasomesha wasanii wa kundi hilo ndani nan je ya Zanzibar ili waweze kuwa
wasanii watakaoitangaza vyema Zanzibar.
“Matarajio
yetu Tausi ni kuwapa mafunzo yalio bora wasanii wetu ambayo watayapata ndani
nan je ya Zanzibar ili wawe wasanii bora ambao wataitangaza Zanzibar kupitia
fani hii ya muziki wa Taarab asilia,”alisema.
Mbali na
hayo lakini pia malengo mengine ya Tausi ni kupata wasanii bora wa kike ambao
ambao wataweza kutunga mashairi ambayo yatasaidia kuwainua wanawake na pia
kutafuta klabu maalum .
Alifahamisha
kwamba lengo la kutafuta klabu ni kutaka kuendelea kwa kikundi hicho ambapo
alifahamisha kwamba vikundi vingi sana
vya taarab vinakufa kutokana na kukosekana kwa klabu .
Maryam
Hamdani ambae pia ni Makamo wa Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) amewashauri wasanii kuendeleza muziki wa
taarab asilia ili waweze kuitangaza nchi yao kupitia fani hiyo.
Pia
aliwashauri wanawake kutumia fani hiyo kuwa ni ajira na sio kuifanya fani hiyo
kuonekana kuwa ni fani ya kihuni jambo ambalo alisema kuwa sio kweli bali ni
dhana potofu kwa watu wasiopenda fani hiyo.
Kutokana na
sababu mafanikio hayo,Mkurugenzi wa Tausi ambae pia ni mwanzilishi wa kundi
hilo ana kila sifa ya kupewa kutokana na ujasiri wake alionao katika kusaidia
kutetea haki za wanawake wenzake katika Nyanja ya muziki wa taarab.
Hii ni
faraja kubwa kwa nchi yetu kutokana na mama huyo kuona umuhimu kundi hilo na
hakuna budi kwa taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi kukisaidia kikundi
hicho ili kiweze kukuwa na kuwapatia ajira akina mama hao.
Tausi ambalo
ni kundi maarufu likiwa chini ya mlezi wake aliekuwa Waziri wa Fedha za zamani
wa Jamuhuri ya Muungano wam Tanzania Zakia Meghji linaendelea kufanya maonyesho
yake katika sehemu mbali mbali za mjini na mashamba.
Subscribe to:
Posts (Atom)











