Thursday, 16 July 2015

ZANTEL YATOA MSAADA WA VYAKULA KWA JUMUIYA YA WAZEE ZANZIBAR



Na Haroub Hussein


 Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel leo imetoa msaada wa vyakula kwa ajili ya mwezi wa Ramadhani kwa makundi maalumu ya wazee hapa visiwani Zanzibar.

Msaada huo unajumuisha sukari, unga wa ngano pamoja na mchele umetolewa katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika leo.

Kampuni ya Zantel upande wa Zanzibar imeainisha wazee zaidi ya 120 wenye uhitaji wa vyakula kwenye mwezi huu wa Ramadhani walio chini ya jumuiya ya wazee hapa Zanzibar.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa wazee, Mkurugenzi wa Biashara wa Zantel-Zanzibar, bwana Mohammed Mussa, amesema ni kawaida kwa kampuni ya Zantel kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii katika kipindi hiki cha Ramadhani.


'Tuna furaha sana leo kuweza kusaidia jamii hii ya wazee ambao mara nyingi wamekuwa wanasahaulika, kwani tunaamini wazee ni sehemu muhimu sana ya jamii ndio maana Zantel leo tumeamua kutoa msaada huu ambao unatutofautisha sana na makampuni mengine katika vipaumbele vyetu' alisema Mussa.

Mussa aliongeza kuwa kama kampuni ya simu inayoongoza Zanzibar, Zantel mara zote imekuwa mfano katika shughuli zake za kijamii na vipaumbele vyake kiujumla.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, mgeni rasmi ndugu Msham Abdallah, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar, alisema anaipongeza Zantel kwa kushirikiana na serikali kuyasaidia makundi ya wazee.


‘Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali katika kulisaidia kundi hili la wazee, kwahiyo ni furaha kwetu leo kuona Zantel imekuwa ya kwanza kusaidia kundi hili leo’ alisema bwana Abdallah.

Akitoa neno la shukrani kwa kampuni ya Zantel, naibu mwenyekiti wa jumuiya ya wazee Zanzibar, Bwana Mwadini Kutenga, alisema anawashukuru Zantel kwa msaada huo, akisema umekuja kwa wakati mufaka hasa ukizingatia kuwa wanakaribia kuadhimisha sikukuu ya Idi.

'Kwa misaada hii, Zantel inawafanya wazee nao wajiskie sehemu ya jamii, kwani mara nyingi wamekuwa wakisahaulika sana na kwa hakika hatutawasau kwa ukarimu wao huu' alisema bwana Kutenga.


Kampuni ya Zantel imekuwa msitari wa mbele katika kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani, na msaada huu ni maalumu kwa kundi la wazee ambalo mara nyingi linasahaulika katika jamii.

Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na lengo la kuwaunganisha na kuwasaidia wazee Zanzibar na sasa ina wanachama zaidi ya 1000.





Wednesday, 15 July 2015

AL MARHUM SHEIKH MOHAMMED MAJID;MIONGONI MWA WANAZUONI WALIOITANGAZA VYEMA DINI YA KIISLAMU


“INALILAHI wa Ina Ilayhi Rajiuun yaani hakika sisi ni waja wa Mwenyezi Mungu na sisi kwake tutarejea,”hiyo ni kauli ambayo kila muumini wa dini ya Kiislamu anaifahamu kwa kuwa ina maana ya kukumbuka kila kilichoumwa na Allah (SW) basi hakina budi kurejea kwake kwa maana ya kufa.

Kwa kila muislamu akiisikia kauli hii huwa anafahamu kwamba ameletwa duniani kwa ajili ya kumuabudu Allah (SW) basi iko siku atarudi kwake.

Naweza kuinasibisha kauli hii kwa Al marhum Sheikh Mohammed Majid ambae ni mmoja wa maulamaa wa dini ya kiislamu waliokuwepo hapa Zanzibar katika kuitangaza dini ya Mwenyezi Mungu(Uislamu).

Marehemu Sheikh Mohammed Majid ni miongoni mwa wanazuoni maarufu wenye maarifa makubwa ya dini ya kiislamu waliotangulia mbele ya haki ambao walikuwepo Zanzibar katika kuitangaza dini ya Mwenyezi mungu.

Sheikh Majid atakumbukwa maisha kutokana na uwezo wake na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika kulingania dini ya Kiislamu na kuisambaza kupitia njia tofauti ili iwafikie wale waliokusudiwa.

Marehemu Mohammed Majid alizaliwa Juni 5 mwaka 1956 katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja,ambapo elimu yake ya awali alianza kuipata kisiwani Pemba kijiji cha Mchakaeni.

Marehemu Sheikh Mohammed Majid alikuwa akiishi kisiwani humo kutokana na baba yake kuhamia kwa shughuli za uvuvi akitokea kijijini kwao Matemwe.

Mwaka 1965 marehemu alihamia kisiwani Zanzibar na kuanza elimu yake ya Maahad Islamia ambayo kwa sasa inajulikana kama Chuo cha Kiislamu Mazizini ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni elimu ya sekondari.

Mara baada ya kumaliza elimu ya sekondari Sheikh huyo alikwenda nchini Sudan mwaka 1984 katika chuo kikuu cha kimataifa cha Afrika kuchukua elimu ya dini ya kiislamu pamoja na lugha ya kiarabu .

Baadae alikwenda nchini Saudi Arabia kuchukuwa shahada ya kwanza ya dini ya Kiislamu na Kiarabu.

Mwaka 1992,Marehemu alirudi Sudan kuchukua shahada ya Uzamili yaani ‘Masters Degree’ ya lugha ya Kiarabu na dini ya Kiislamu na mara baada ya kumaliza elimu hiyo alirudini nyumbani Zanzikbar.

Marehemu Sheikh Mohammed Majid hakuwa nyuma katika maswala ya kutafuta elimu ya dini nay a dunia kutokana na kwamba alikuwa akijua umuhimu wa elimu.

Alikaa Zanzibar kwa muda mfupi na baadae alirudi nchini Sudan kuchukuwa elimu ya udaktari wa Falsafa “PHD” ya dini ya Kiislamu pamoja na lugha ya Kiarabu.

Elimu alizozipata nchi mbali mbali na aliyoipata hapa nchini kupitia walimu waliomsomesha dini aliweza kuongeza dini kipaji chake na kuwa na hamu kubwa ya kuitangaza dini ya kiislamu.

Marehemu Dr Mohammed Majid baada ya kumaliza elimu hiyo na kurudi nyumbani alisomesha lugha ya Kiarabu katika kituo cha Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Pia marehemu Dk  Mohammed Majid ni miongoni mwa waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Kiislamu Chukwani na pia aliwahi kuwa msaidizi Mwalimu Mkuu Madrassat Noor mpaka mwaka 2000 baada ya kufariki marehemu Maalim Bakathir.

Marehemu Sheikh Mohammed Majid alitawazwa rasmin kuwa mwalimu mkuu wa Madrassa hiyo iliyopo katika mtaa wa Ukutani mjini Unguja.

Mnamo mwaka 2002 sawa na mwaka 1423,Marehemu Sheikh Mohammed Majid alifariki dunia na kuzikwa kijijini kwao Matemwe Mnazimmoja Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk Mohammed Majid atakumbukwa maisha na waislamu wote wa hapa visiwani Unguja na Pemba kwa ujumla kwa kuwa na changamoto kubwa ya kuanzisha kipindi cha Jiongezee Maarifa kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC).

Kipindi hicho kimeweza kuvutia vijana wengi kutaka kuifahamu na kusoma zaidi mwenendo wa dini yao ya kiislamu pamoja na kitabu kitukufu cha Quraan.

Baadhi ya masheikh waliokuwepo hapa Zanzibar wanamzungumzia kwamba marehemu huyo atakumbukwa sana katika kipindi chake hicho cha Jiongezee Maarifa ambacho hupendwa na waislamu wengi kwa kuwafanya vijana wengi kuwa na hamu ya kuijua dini yao.

“Marehemu Sheikh Mohammed tunamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoyafanya wakati alipokuwa yuhai kwa kuanzisha kipindi cha Jiongezee maarufa ambacho kimewaongoa vijana wengi  wa Kiislamu na kufanya kipindi hicho kikauwa mpaka kufikia kisiwani Pemba.

Katika kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,Marehemu Sheikh Mohammed Majid alikuwa akisomesha somo la Fiqhi na Quraan katika msikiti wa Jongeani na msikiti wa Mchangani yote ya mjini Unguja.

Marehemu ameweza kujijengea jina lake kwa kuweza kuitangaza dini ya Kiislamu kupitia Nyanja mbali mbali kwa vijana na watu wazima ili kuzidi kukuwa kwa jamii ya Kiislamu kwa kufuata maadili mema ya dini yao.

Aidha Marehemu atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri mbali ya kulingania dini ya Kiislamu,lakini pia mapenzi yake kwa watu wote wa rika tofauti,ucheshi na pia hakuwa mtu mwenye majivuno.

Marehemu aliacha wake watatu na watoto 11,wanawake 10 na mwanamme mmoja.

Kwa niaba ya makala haya na mafundisho yake mema  ya hapa duniani kwa ajili ya Akhera, Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amlaze mahali pema peponi Aamin.

Saturday, 4 July 2015

DR OMAR: NGUZO IMARA ILIYOKATIKA GHAFLA


SIKU kama ya leo miaka kumi nan ne iliyopita.Tanzania iligubikwa na simanzi isiyokuwa na mfano baada ya kupokea taarifa za kifo cha aliyekuwa Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Marehemu alifariki ghafla siku moja tu baada ya kushiriki katika ufunguzi wa maduka ya biashara ya sabasaba katika maeneo ya Mtoni jijini Dar es Salaam.

Wananchi wa Tanzania hawatoweza kumsahau marehemu kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kwa Watanzania.

Akiwa katika ufunguzi huo ambapo alionekana kuwa ni mtu wa kawaida kwa kuwa na afya aliwahutubia wananchi kwsa kuwapa moyo wananachi wa Tanzania na Zanzibar kwa jumla kutokana na kupendelea kusema ukweli na hata kupiga vita tabia ya ubaguzi.

Katika hotuba zake ambazo alizowahi kuzitoa katika kazi zake za kawaida ilikuwa ni kukemea tabia ya baadhi ya watu kubaguana kwa misingi ya rangi zao na maeneo ya asili.

Utekelezaji wa majukumu yake katika kukemea tabia hiyo uliweza kumjengea sifa kwa wananchi na watu wengi kwa kuwa na nia ya kutaka na Mikoa mengine ya Tanzania na kuondosha ubaguzi kwani aliamini kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Kwake maumbile au asili tofauti na mwengine kwani halikuwa jambo la kujadiliwa ila watu walipaswa kuwa kitu kimoja kwa ajili ya maendeleo yao kwani wapo kwa kutambuana tu.

Lakini kauli ya marehemu Dr Omar Ali Juma,aliyoitoa mara baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri kiongozi wa Zanzibar alisema kwamba ni vyema Wazanzibari wakasahau yaliopita na kuangalia mbele.

Marehemu aliamini kuwa kauli hiyo ni muhimu kwa kuwaunganisha wananchi wao na ni vyema kukumbukwa kwani amewahi kushuhudia matatizo mengi yanayowakumba watu waliotilia maanani tofauti zao na kuacha kushirikiana katika mambo muhimu ya kimaisha.


Kutojali ukabila,rangina uzawa kutasaidia kuimarika kuimarika kwa Taifa la Zanzibar.

Marehemu atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri na wananchi wa Tanzania kupitia hotuba zake zilizojaa nasaha juu ya watu wa Zanzibar na kuamini kuwa Zanzibar inaweza kuwa imara na mshikamano.

Pia marehemu Dr Omar atakumbukwa sana kutokana na mpango wa kusimamia kujitosheleza kwa chakula uliojulikana kama ‘Mtakula’.

Mpango huo ambao ulianzishwa na Serikali ya awamu ya nne ya Marehemu Sheikh Idrissa Abdulwakil,ambapo ulileta mageuzi makubwa ya kilimo hapa visiwani .

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa makala haya walisema Mtakula ulisaidia sana kuamsha ari ya wananchi kupenda kilimo hapa visiwani na mlezi mkuu alikuwa Dr Omar Ali Juma.

Kwa upande wa siasa,Marehemu alikuwa ni mwanasiasa mashuhuri na mahirina aliwapenda sana watu wote hii inaonesha kuwa kauli zake alikuwa akizitekeleza kwa vitendo na kuwaona watu wote ni sawa bila ya kujali itikadi zao kisiasa na ulua aliokuwa nao.


Dr atakumbukwa kwa mambo yake yote mema ambayo alihakikisha wananchi wanayaendeleza kwa ufasaha na mambo yote amabayo ni msingi wa maendeleo ya nchi.

Alipokuwa Makamo wa Rais marehemu atakumbukwa sana kwa juhudi zake kuimarisha Muungano na pale matatizo yanapoibuka hakuwa nyuma kwa kusaidiana na viongozi wenzake wa ngazi za juu kutatua matatizo hayo.

Pia aliweza kusaidia kuleta umoja kwa wananchi wa Tanzania bila ya woga wowote.
Aidha wananchi wao walizungumza na mwandishi wa makala hii walisema siku zotemarehemu alisimamia maslahi ya Zanzibar kwa wakati wote wa uongozi wake.

“Dk Omar ni mwanangu,alikuwa akija Pemba basin a nyumbani kwangu huwa anakuja namjua vizuri sana alikuwa hodari katika kusimamia maslahi yetu sisi Wazanzibari,”alisema Mzee Kassim Haji mkaazi wa Wawi Pemba.

Saleh Amir ni rafiki wa karibu na marehemu Dr Omar Ali Juma anaeleza kuwa alikuwa ni mtu mwenye kupenda watu na hata kusaidia alikuwa hodari sana.

“Marehemu alikuwa ni mtu wa karibu sana na mimi alikuwa ni mpenda watu,hodari anapenda masihara na mwenye kupenda kusaidia wengine,alisema Saleh Amir.

Dr Omar pia katika uhai wake alikuwa ni mpenzi mkubwa wa michezo hususan mpira wa miguu ambapo alipokuwepo visiwani Unguja huhudhuria katika kiwanja cha Amaan kuangalia mchezo wa soka.

Kwa upande wa burudani Dr Omar alikuwa ni mpenzi mkubwa wa Maulid ya homu na katika shughuli zake nyingi alikuwa lazima yakuwepo maulidi hayo.

Bila shaka hii ni sifa njema ya marehemu katika kudumisha utamaduni,mila na desturi za Kizanzibari.

Marehemu   Dr Omar hatoweza kusahauli hatoweza kusahaulika katika mioyo ya wapenda amani na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hayo yanatokana na juhudi alizokuwa akizichukuwa katika kuhakikisha  maendeleo yanapatikana katika nchi.


Pia  hatoweza kusahaulikwa kwa imanina roho yake nzuri katika kusaidia wananchi katika Nyanja mbali mbali za kutatua matatizo ya kimaisha.

Marehemu alizaliwa Juni26 mwaka 1942 Chake Chake kisiwani Pemba,elimu yake aliianzia mnamo mwaka 1949 hadi mwaka 1957 katika skuli ya Haile Selassie wakati huo ikifahamika kwa jina la Euan Smith Secondary School.

Mwaka 1960 alijiunga katika chuo kikuu cha Moscow nchini Urusi na kupata stashahada ambapo aliendelea na masomo yake katika chuo hicho hicho kwa muda wa miaka saba.

Baadae pia alipata masomo katika vyuo vikuu vyengine katika taaluma ya utibabu wa wanyama ikiwemo chuo kikuu cha Cairo nchini Misri,pia alipata taaluma nyengine katika mwaka 1969 katika vyuo mbali mbali ikiwemo nchini Marekani na kile cha Kivukoni nchini Tanzania.

Mwaka 1988alifanikiwa kushika wadhifa wa Waziri Kiongozi wa Zanzibar hadi mwaka 1995 aliposhika wadhifa wa Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hadi kufariki kwake mwaka 2001 siku kama ya leo.